Mambo ya kufahamu kabla ya mkutano wa UNGA80 kuhusu suala la Palestina
Mambo ya kufahamu kabla ya mkutano wa UNGA80 kuhusu suala la Palestina
Amani na Usalama
Baada ya karibu miaka miwili ya vita huko Gaza, mateso ya wakaazi wake hayajaonesha dalili yoyote ya kupungua.
Wakati Israel inaanza mashambulizi makubwa ya ardhini kaskazini mwa eneo hilo, macho na masikio tena yanageukia Umoja wa Mataifa New York Maarekani.
Leo Septemba 22, katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, mkutano wa viongozi wa nchi na serikali ukiungwa mkono na Ufaransa na Saudi Arabia utajaribu kufufua suluhu ya muda mrefu iliyokwama ya “mataifa mawili”, moja la Kiyahudi yaani Israeli na moja la Kipalestina, yakikaa pamoja ndani ya mipaka salama na inayotambuliwa.
Katika hotuba yake kwa Baraza la Usalama mwezi Aprili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alionya kwamba mchakato huo “uko hatarini kutoweka kabisa.” Akisema ari ya kisiasa ya kufikia lengo hilo “inaonekana iko mbali kuliko wakati mwingine wowote.”
Hata hivyo, katika mazungumzo ya hivi karibuni na waandishi wa habari, kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa alihoji “Je, mbadala ni upi? Ni suluhu ya taifa moja ambapo Wapalestina watafukuzwa au watalazimishwa kuishi katika nchi yao bila haki?”
Akasisitiza kwamba ni “wajibu wa jumuiya ya kimataifa kuendeleza suluhu ya mataifa mawili na kisha kuweka mazingira ya kufanya iwezekane.”
Yanayojadiliwa
- Wazo la kuanzisha taifa moja kwa Wayahudi na moja kwa Wapalestina, wakiishi kwa amani bega kwa bega, lilikuwepo kabla ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa mnamo 1945. Tangu hapo limeandikwa na kuandikwa upya, likiwa limeonekana katika maazimio mengi ya Baraza la Usalama, mazungumzo ya amani kadhaa, na pia katika kikao maalum cha dharura cha kumi cha Mkutano wa Baraza Kuu kilichoendelea tena hivi karibuni.
- Mwaka 1947, Uingereza ilikomesha mamlaka yake katika eneo la Palestina na kupeleka “Suala la Palestina” Umoja wa Mataifa, ambao ulipokea jukumu la kutafuta suluhisho la haki kwa tatizo hilo. Umoja wa Mataifa ulipendekeza kugawanya Palestina katika mataifa mawili huru, moja la Waarabu wa Kipalestina na lingine la Kiyahudi, huku Yerusalemu ikifanywa kuwa ya kimataifa jambo lililoweka msingi wa suluhu ya mataifa mawili.
- Mkutano wa amani uliitishwa Madrid mwaka 1991, kwa lengo la kufikia makubaliano ya amani kupitia mazungumzo ya moja kwa moja katika njia mbili, kati ya Israel na nchi za Kiarabu na kati ya Israel na Wapalestina, kwa misingi ya maazimio ya Baraza la Usalama 242 (1967) na 338 (1973).
- Mwaka 1993, Waziri Mkuu wa Israeli Yitzhak Rabin na Mwenyekiti wa Shirika la Ukombozi wa Palestina Yasser Arafat walisaini Mkataba wa Oslo, ulioweka misingi ya mazungumzo zaidi na kuweka msingi wa serikali ya mpito ya Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi na Gaza.
- Mkataba wa Oslo wa 1993 uliahirisha baadhi ya masuala hadi kwenye mazungumzo ya hadhi ya kudumu, yaliyofanyika 2000 huko Camp David na 2001 mjini Taba, lakini hayakufanikisha suluhu.
Miaka mitatu baada ya Mkataba wa Oslo, lengo kuu la Umoja wa Mataifa linasalia kusaidia Wapalestina na Waisraeli kusuluhisha mzozo na kukomesha ukaliaji kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na makubaliano ya pande mbili, ili kufanikisha maono ya mataifa mawili Israel na taifa huru, la kidemokrasia, lenye muungano, lenye kuendelea na lenye mamlaka kamili la Kipalestina wakiishi pamoja kwa amani na usalama ndani ya mipaka salama na inayotambuliwa, kwa misingi ya mipaka ya kabla ya 1967, huku Yerusalemu ikiwa mji mkuu wa mataifa yote mawili.
Mwanamke Mlowezi akimpita askari wa Israel Mashariki mwa Jerusalemu Mashariki
Nini kinachotarajiwa mkutano wa leo Septemba 22
Mkutano huu unafanyika siku ya ufunguzi wa wiki ya vikao vya ngazi ya juu vya Madala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambao ni mkusanyiko wa kila Septemba wa viongozi wa dunia na unakuja katikati ya hali inayotia wasiwasi sana ya eneo la Palestina kukiwa na operesheni kali za kijeshi za Israel zilizoua zaidi ya watu 60,000 huko Gaza tangu Oktoba 7, 2023, kutangazwa kwa baa la njaa kaskazini mwa Gaza Agosti 22, mashambulizi ya Israel dhidi ya maafisa wa Hamas nchini Qatar Septemba 9 na kuongezeka kwa kasi kwa upanuzi wa makazi katika Ukingo wa Magharibi.
Licha ya hali tete, suluhu ya mataifa mawili inapata tena nguvu za kidiplomasia.
Mnamo Septemba 12, Mkutano wa Baraza Kuu ulipitisha kwa kura nyingi “Tamko la New York,” kufuatia mkutano wa Julai ulioandaliwa pia na Ufaransa na Saudi Arabia. Tamko hilo lilitoa wito wa “amani ya haki na ya kudumu inayotegemea sheria za kimataifa na msingi wa suluhu ya mataifa mawili.”
Ili kumaliza vita, lilihimiza Hamas “kumaliza jukumu lake Gaza, na kukabidhi silaha zake kwa Mamlaka ya Palestina.” Marekani na Israel, ambazo zilikuwa zimegomea mkutano wa Julai, zilipiga kura kupinga maandiko hayo.
Mkutano wa leo Septemba 22 huenda ukaendeleza msukumo huo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatarajiwa kutangaza utambuzi wa Ufaransa kwa Taifa la Palestina, na nchi kadhaa za Magharibi, zikiwemo Uingereza, Canada, Ubelgiji na Australia, zinadaiwa kuzingatia kuchukua hatua hiyo pia.
Kwa kifupi, athari ya mkutano inaweza kuleta msukumo mpya katika juhudi za kuweka ramani ya Umoja wa Mataifa kuelekea mataifa mawili.