Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kushamiri kwa Afrika hakuzuiliki: Katibu Mkuu wa UN

Vijana wa kike hushiriki katika warsha ya teknolojia huko Kigali, Rwanda.
UN Women Vijana wa kike hushiriki katika warsha ya teknolojia huko Kigali, Rwanda.

Kushamiri kwa Afrika hakuzuiliki: Katibu Mkuu wa UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika mkesha wa wiki ya ngazi ya juu ya Mjadala Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa 80 au UNG80 Katibu Mkuu António Guterres amesema kuwa Afrika ipo katikati ya fursa za dunia, akiwataka viongozi na wawekezaji kushirikiana kutumia nguvu ya vijana wake, nishati jadidifu, na uwezo wa kidijitali.

Akihutubia hafla ya Afrika Isiyozuilika “Unstoppable Africa 2025”, jijini New York hii leo kwenye hotel ya Marriot alisema kwa msisitizo kuwa  “Afrika ni fursa, tuwekeze katika watu wa Afrika na uwezo wao, na tufanye kushamiri kwa Afrika kuwa jambo lisilopingika, lisilozuilika, na lisiloepukika.”

Kufungua injini ya uchumi wa Afrika

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa ustawi wa Afrika unategemea utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), lakini akaonya kwamba mafanikio yake yanahitaji miundombinu imara. 
Hii inahitaji barabara, bandari, gridi za umeme, viwango vilivyoharmonishwa, na kanuni zinazotabirika,” amesema. Bila uwekezaji huo, ahadi ya soko la pamoja la Afrika itabaki kuwa ndoto.
Wasichana wakiwa katika mafunzo ya Roboti Rwanda
UN Women/Geno Ochieng Wasichana wakiwa katika mafunzo ya Roboti Rwanda

Kuendesha mapinduzi yanayojali mazingira viwandani

Guterres ameonesha uwezo mkubwa wa Afrika katika nishati jadidifu, akieleza kuwa ukosefu wa usawa katika uwekezaji wa dunia ni dhuluma kubwa. “Afrika inapokea asilimia 2 pekee ya uwekezaji wa dunia katika nishati jadidifu hili lazima libadilike,” amesisitiza. 
Akiwa na kumbukumbu ya zaidi ya watu milioni 600 barani humo wanaoishi bila umeme, ametaka kuongezwa kwa miradi ya jua na upepo, upanuzi wa gridi na hifadhi, na upatikanaji wa nishati kwa wote. “Hii haipaswi kuwa hadithi nyingine ya uchimbaji bila ujumuishaji,” ameongeza, akisisitiza umuhimu wa haki za binadamu katika mchakato wa mabadiliko ya nishati safi.

Kubadilisha mifumo ya chakula

Licha ya kumiliki zaidi ya nusu ya ardhi inayoweza kulimwa duniani, Afrika bado huagiza chakula chenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 100 kila mwaka. Guterres ameiita hali hii kuwa ni kitendawili kinachohitaji kufikia kikomo.
“Lazima tuongeze kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi, kuwekeza katika umwagiliaji na hifadhi, kupunguza hasara baada ya mavuno, na kuwawezesha wakulima wadogo, hasa wanawake,” amesema.
Ameusifu uongozi wa Afrika katika Mkutano wa Tathmini ya Mifumo ya Chakula wa Umoja wa Mataifa uliofanyika Addis Ababa Ethiopia kama ushahidi kuwa suluhu zipo.
Katibu Mkuu wa UN António Guterres
UN Photo/Mark Garten Katibu Mkuu wa UN António Guterres

Mapinduzi ya Kidijitali na Akili Mnemba

Katibu Mkuu pia amesisitiza ukuaji wa kasi wa mfumo wa kidijitali barani Afrika, ambapo zaidi ya watu milioni 570 sasa wako mtandaoni. 
Ametaka jitihada za kimataifa kuhakikisha Afrika inashiriki kikamilifu katika kusimamia Akili Mnemba AI. Uunganishwaji wa bei nafuu, uwezo wa kikanda, na mafunzo vinaweza kufungua ukuaji jumuishi na nafasi za ajira kwa mamilioni ya vijana wa Afrika,” amesema, akiongeza kuwa ubunifu lazima utumike kwa maendeleo na siyo kuongeza pengo la usawa.

Kuwezesha Mustakabali wa kifedha wa Afrika

Amehitimisha, Guterres kwa kutoa wito wenye nguvu wa mabadiliko ya kifedha na ya kimfumo. “Ni kashfa kwamba bado hakuna Mwakilishi wa Kudumu wa Afrika katika Baraza la Usalama,” amesema, akisisitiza haja ya mageuzi ya taasisi za kimataifa. 
Pia ametaka “mageuzi muhimu ya msingi ya taasisi za kifedha za kimataifa” ili kupunguza gharama ya mitaji, kuongeza mara tatu uwezo wa kukopesha wa Benki za Maendeleo za Kimataifa, na kutoa uwakilishi imara zaidi wa nchi za Afrika katika taasisi za kimataifa.