Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN atoa tahadhari juu ya kuzorota kwa hali El Fasher, Sudan

Watoto na familia zilizopoteza makazi yao wamepumzika katika kambi huko Tawila, Kaskazini mwa Darfur, Sudan.
© UNICEF/Mohammed Jamal Familia ambazo zilikimbia mapigano huko Zamzam na El Fasher eneo la Darfur Kaskazini, zinatafuta hifadhi huko Tawila.

Katibu Mkuu wa UN atoa tahadhari juu ya kuzorota kwa hali El Fasher, Sudan

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jumamosi ameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali inayozidi kuzorota kwa kasi katika mji wa El Fasher, amba oni mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini Sudan, akionya juu ya hatari kubwa kwa raia waliokwama katika mji huo uliozingirwa.

El Fasher imekuwa chini ya mzingiro mkali unaofanywa na kikosi cha kijeshi cha Msaada wa Haraka (RSF) kwa zaidi ya siku 500, huku mashambulizi dhidi ya raia yakiongezeka katika wiki za hivi karibuni. Wengi wa wakazi wa kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abu Shouk iliyo karibu wameripotiwa kukimbia kufuatia mashambulizi ya makombora na uvamizi usio na kikomo.
“Mapigano lazima yakome sasa,” Katibu Mkuu António Guterres amesema kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake mjini New York Marekani.
Amerudia wito wake wa “kusitishwa mara moja kwa mapigano El Fasher, kuheshimu na kulinda raia, na kuwezesha upatikanaji wa msaada wa kibinadamu bila vizuizi na kwa usalama na uimara.”
Kiongozi huyo pia amesisitiza kwamba raia wanaotaka kuondoka kwa hiari lazima wahakikishiwe njia salama ya kuondoka.
Mwanamke anayeitwa Amani amembeba mtoto wake mchanga akiwa ameketi na watoto wengine wawili katika makazi ya muda huko Tawila, Kaskazini mwa Darfur, Sudan.
© UNICEF/Mohammed Jamal Familia iliyokimbia makazi yao huko Tawila baada ya kukimbia mapigano huko Al Fasher, Darfur Kaskazini.

Shambulio la msikiti

Onyo la Katibu Mkuu limetolewa baada ya shambulio lililotokea kwenye msikiti mjini El Fasher siku ya Ijumaa, ambalo inaripotiwa liliwaua makumi ya raia wakati wa sala ya asubuhi.
Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Denise Brown, amesema ana “ wasiwasi mkubwa kuhusu shambulio hilo, akisisitiza kwamba sheria ya kimataifa ya kibinadamu inalazimisha kulindwa kwa maeneo ya ibada na wale wanaoabudu ndani yake.”
“Ni kosa la kivita pia kulenga kwa makusudi majengo yaliyowekwa kwa ajili ya dini. Shambulio hili, ambalo linaripotiwa lilifanywa na RSF, lazima lichunguzwe na wahusika wawajibishwe,” amesema katika taarifa tofauti.
Mtoto mdogo amesimama katika kambi ya wakimbizi ya muda huko Sudan, akiwa na mwanamke aliyevaa kitambaa kichwani na makazi mengine ya muda nyuma.
© UNICEF/Mohammed Jamal Mgogoro kati ya majeshi hasimu nchini Sudan umeitumbukiza nchi hiyo, hususan eneo la Darfur, katika janga kubwa la kibinadamu.

Dharura ya kibinadamu

Hali katika mji wa El Fasher na kambi zilizo jirani imezidi kuwa mbaya tangu baa la njaa lilipobainishwa katika eneo hilo mwaka jana.
Hatari ya ghasia zenye misingi ya kikabila pia inazidi kuongezeka huku wapiganaji wakisonga ndani zaidi ya mji huo.
Raia wanaendelea kubeba mzigo wa mapigano kati ya RSF na Jeshi la Sudan (SAF), ambayo yameendelea tangu Aprili 2023, yakiua maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni kufungasha virago na kukimbia makazi yao.
Watu waliokimbia makazi yao, wakiwemo wanawake na watoto, wanaonyeshwa kwenye misafara inayokimbia El Fasher huko Darfur Kaskazini, Sudan, wakitafuta usalama wakati wa mgogoro wa kibinadamu.
© UNICEF/Mohammed Jamal Msafara uliojaa familia zilizofurushwa ukikimbia El Fasher, Kaskazini mwa Darfur, kutafuta usalama. Kote Sudan, zaidi ya watu milioni 12 wamefurushwa kutoka makazi yao.

Wito wa kuchukua hatua za kimataifa

Bwana Guterres amehimiza pande zote mbili kuanza mazungumzo haraka ili kusitisha mapigano na kurejea katika majadiliano kwa ajili ya suluhu ya kisiasa endelevu.
Ametoa pia wito wa “hatua za pamoja za kimataifa kwa ajili ya watu wa Sudan” huku viongozi wa dunia wakikusanyika jijini New York wiki ijayo kwa Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA80.
Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Ramtane Lamamra, “yuko tayari kusaidia juhudi za dhati za kukomesha vita na kuweka mchakato wa kisiasa shirikishi unaodaiwa na watu wa Sudan,” imesema taarifa hiyo ya Katibu Mkuu.