Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UN atoa wito wa haraka wa kukomesha vita katika Siku ya Kimataifa ya Amani

UNPA awametoa stampu mpya kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Aani 2025
UNPA
UNPA awametoa stampu mpya kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Aani 2025

Katibu Mkuu wa UN atoa wito wa haraka wa kukomesha vita katika Siku ya Kimataifa ya Amani

Amani na Usalama

Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Amani leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa onyo kali kuhusu dharura ya kusitisha vita na kujenga ulimwengu wenye utulivu zaidi, akisema binadamu “wanalia kwa ajili ya amani.”

“Ulimwengu wetu unaokumbwa na vita unalia kwa ajili ya amani,” amesema Guterres kupitia ujumbe wake maalumu kwa ajili ya siku hii akiongeza kuwa “Siku ya Kimataifa ya Amani ya mwaka huu inatuhimiza kila mmoja wetu kuupa sauti wito huo wa amani.”
Ametoa taswira ya kusikitisha kuhusu gharama ya kibinadamu inayosababishwa na migogoro, akibainisha kuwa “maisha yanasambaratishwa, utoto unaporwa, na heshima ya msingi ya kibinadamu inatupiliwa mbali, katikati ya ukatili na udhalilishaji wa vita.”

Mlipuko wa migogoro umetawala

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amesema jumuiya ya kimataifa inakabiliana na “mlipuko wa migogoro,” akieleza ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na “idadi ya juu kabisa ya watu kukimbia makazi yao.” Licha ya changamoto hizo, amesisitiza kuwa amani inawezekana na ni ya dharura.
“Wote wanachotaka ni amani,” amesisitiza akiongeza kuwa “Amani ni jukumu la kila mmoja. Madhara ya vita yanaenea duniani kote.”
Guterres amehusisha maendeleo endelevu na ujenzi wa amani, akibainisha kuwa “nchi tisa kati ya kumi zinazokumbwa zaidi na changamoto za maendeleo zinakumbwa pia na migogoro.” Pia ameonya juu ya hatari za ubaguzi wa rangi, udhalilishaji na upotoshaji wa taarifa, akisema mambo hayo “yanamwagia mafuta moto wa migogoro.”
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akipiga Kengele ya Amani wakati wa hafla iliyofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Amani  mwaka 2025.
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akipiga Kengele ya Amani wakati wa hafla iliyofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Amani mwaka 2025.

Kudumisha amani ni jukumu la kila mtu

Badala yake, amewataka watu kila mahali “kuzungumza lugha ya heshima, kufungua mioyo yetu kwa wengine, na kutumia ushawishi wetu kusukuma ajenda ya amani.”
Akieleza kuhusu nguvu ya mabadiliko ya amani, Guterres amesema, “Pale tunapokuwa na amani, tunakuwa na matumaini. Familia zinaungana, jamii zinajijenga upya, watoto wanasoma na kucheza.”
Amehitimisha ujumbe wake kwa wito wa wazi kwa viongozi na wananchi wote, “Lazima tunyamazishe mtutu wa bunduki. Tumalize mateso. Tujenge madaraja. Na tuunde utulivu na ustawi. Amani haiwezi kusubiri kazi yetu inaanza sasa.”