Tamasha la YouthLead lawaweka vijana katika kitivu cha maamuzi ya dunia: UN
Tamasha la YouthLead lawaweka vijana katika kitivu cha maamuzi ya dunia: UN
Malengo ya Maendeleo Endelevu
Umoja wa Mataifa umeweka wazi nguvu ya vijana katika kuleta mabadiliko ya kimataifa kwa leo kuzindua kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Maataifa Tamasha la YouthLead, harakazi za wiki nzima za uongozi wa vijana na mshikamano wa kizazi hadi kizazi.
Tamasha hili limeandaliwa na Ofisi ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Vijana, na linaambatana na maadhimisho mawili ya kihistoria, Kikao cha 80 cha Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA80) na Miaka 30 ya Mpango wa Dunia wa Utekelezaji kwa Vijana (WPAY30).
Zaidi ya mkusanyiko wa kiishara, tamasha hili limekusudiwa kuwa kituo cha mshikamano kwa vijana na washirika wao kutoka sekta mbalimbali. Washiriki ni pamoja na taasisi za Umoja wa Mataifa, wawakilishi wa serikali, asasi za kiraia, vyuo vikuu, na mashirika yanayoongozwa na vijana au yanayohudumia vijana.
Wote kwa pamoja watajifunza na kubadiliisha uzowefu kutokana na mafanikio yaliyopatikana, kushiriki mawazo makubwa na kupanga njia mpya za ushiriki wa vijana katika maamuzi ya kimataifa.
Tamasha linafanyika wakati muhimu
“Tamasha hili linakuja katika wakati nyeti,” wamesisitiza waandaaji wa tamasha hilo. “Duniani kote, vijana wanakabiliwa na changamoto kubwa zilizoingiliana kuanzia mabadiliko ya tabianchi, migogoro, ukosefu wa usawa hadi kupungua kwa imani katika taasisi. Lakini pia vijana ndio wanaoongoza suluhu, wakihimiza uwajibikaji, haki, uendelevu na ujumuishi.”
Tamasha la #YouthLead linatoa msisitizo kwa mambo matatu makuu yanayounda ajenda ya dunia ya leo:
- Vijana si viongozi wa baadaye pekee tayari wanaongoza mabadiliko sasa.
- Harakati za vijana zinaunda upya ajenda za kitaifa na kikanda duniani kote.
- Ushirikiano wa vizazi ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya muda mrefu na endelevu.
Umoja wa Mataifa unasisitiza kwa kukuza sauti za vijana na kuimarisha ushirikiano kati ya vizazi, tamasha hili linakusudia kuhakikisha kuwa vijana hawasikilizwi tu bali pia wanajumuishwa kikamilifu katika mifumo ya uongozi na hatua za kimataifa.
“Hili ni suala la kujenga mifumo inayofanya kazi kwa ajili ya na pamoja na vijana,” Ofisi ya Mjumbe wa Vijana imebainisha. kuwa "matarajio ya baadaye yanategemea hili.”