Tetemeko la ardhi Afghanistan limewaacha wanawake na wasichana katika janga la muda mrefu: UN Women.
Tetemeko la ardhi Afghanistan limewaacha wanawake na wasichana katika janga la muda mrefu: UN Women.
Wanawake na wasichana ambao bado wanateseka kufuatia tetemeko kubwa la ardhi hivi karibuni nchini Afghanistan wanakabiliwa na mateso makubwa zaidi wanapojaribu kujenga upya maisha yao bila msaada wa kutosha kutoka kwa jamii ya kimataifa, amesema Susan Ferguson, Mwakilishi Maalum wa shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya wanawake nchini Afghanistan, UN Women, akizungumza na waandishi wa habari hii leo huko Geneva Uswisi.
Bi. Susan Ferguson amesema, "Ingawa matetemeko ya ardhini yanayofuatia tetemeko hilo kubwa yamepungua, au yamepita kabisa, wanawake katika maeneo yaliyoathirika wanakabiliwa na janga la muda mrefu iwapo hawatapata msaada wa haraka"
Kwa zaidi ya wiki mbili baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.0 kwa kipimo cha Richter kutikisa mashariki mwa Afghanistan, UN Women imesema vikosi vya uokoaji vimekuwa vikikabiliana na mazingira magumu ,mara nyingi kwa kutembea kwa miguu ili kuwafikia watu walioko vijijini kabisa katika mkoa wa Kunar.
Athari zinazoendelea za tetemeko hilo
Takwimu za UN Women zinaonesha kuwa Takribani watu 2,200 wamepoteza maisha baada ya nyumba zilizojengwa kwenye miinuko kuporomoka juu ya nyingine wakati tetemeko hilo lilipotokea usiku wa manane mnamo tarehe 31 Agosti.
Baada ya kukutana na wanawake manusurika wa tetemeko hilo na wanaoishi kwenye mahema ya muda katika wilaya ya Chawkay, katikati ya mkoa wa Kunar, Bi. Ferguson amesema ni wazi kuwa watahitaji makazi imara zaidi hivi karibuni, hasa hali ya hewa inapozidi kuwa ya baridi.
Ameongeza kuwa “Wanawake hawa walikimbia kijiji chao usiku wa manane tetemeko lilipotokea, wakitembea kwa saa kadhaa kutafuta makazi, wamesema wamepoteza ndugu zao, wengi bado wako chini ya kifusi. Wamepoteza nyumba zao, wamepoteza maisha yao na vyanzo vya kipato chao. Kama mwanamke mmoja alivyoniambia, na sasa hawana chochote.”
Wanawake na wasichana walikuwa zaidi ya nusu ya watu waliouawa na kujeruhiwa katika janga hilo. Pia wanawake na wasichana ni asilimia 60 ya wale ambao bado hawajapatikana, huku manusura wengi wakiishi kwenye mahema au nje ya nyumba, kama zilivyoshuhudia timu za tathmini za UN Women.
Kutoa huduma za afya kwa manusura wa janga hilo bado ni kipaumbele, amesema Bi. Ferguson, akiongeza kuwa uharibifu wa miundombinu ya msingi umeongeza hatari ya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, kwani wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za choo au maji, hali inayowaweka katika hatari ya ukatili na mabomu ya kutegwa ardhini.