Amri ya kuhama 'kaa la moto' kwa wananchi Gaza
Amri ya kuhama 'kaa la moto' kwa wananchi Gaza
Baada ya amri iliyotolewa na jeshi la Israel la kuwataka wapalestina walioko katika eneo la mji wa Gaza huko Ukanda wa Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israel kuondoka eneo hilo kwani linataka kufanya mashambulizi, hali imekuwa mbaya kwa wananchi hususan wazee ambao sasa wanafunga safari kilometa nyingi kuondoka eneo hilo.
Video ya Umoja wa Mataifa inaonesha taswira kutoka juu, ni eneo la fukwe katika pwani ya Al Rashid, upepo wa baharí unapiga eneo la Gaza, msururu mrefu wa mamia ya watu wakiwa na mizigo yao wanayoivuta kwa taabu wanahama eneo la Gaza mjini kuelekea Kusini mwa Gaza kwani sasa Israel inatekeleza operesheni za kijeshi katika eneo hilo.
Msururu huo unaonesha magari madogo, malori yakiwa wamejaa magodoro kuukuu na mali nyingine, wananchi wengine wanasukuma mikokoteni na wananchi wengine wakitembea kwa miguu huku wakiwa wamewashika watoto wao, wazee wengine wanashikiliwa huku wakiendelea na safari.
Hawa wote wanaelekea kusini mwa Gaza eneo ambalo kipindi kifupi kilichopita walifurushwa huko na jeshi la Israel na kutakiwa kuja eneo hili la mji wa Gaza lakini sasa wamepewa amri ya kuondoka tena.
Video inaonesha magari mengine yameharibikia njiani, wananchi wengine wamechukua mabomba mawili marefu na kuyafunga Kamba kisha kuweka mizigo juu yake na wanavuta mabomba hayo. Yani kila namna inatumika katika kusaidia kuhama na chochote watakachoweza kwani waendako hakuna lolote lakini kubaki watokapo maana yake, ni kifo.
Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa ambaye naye alikuwa miongoni mwa wanaohama, hali ni mbaya sana njiani kwani hakuna msaada wowote na hata wale wanaotaka kupata huduma ya usafiri gharama ni takriban dola 600 mpaka 700 kitu ambacho wengi hawawezi kumudu.
Wazee na watoto wanalazimika kutembea umbali wa kimometa 25 kwenda eneo ambalo Israel inawataka kuhamia na safari yao haina maelezo mazuri ya kueleza bali ni mateso matupu.
Mwandishi huyo wa UN anasema alimuhoji mkazi mmoja wa Gaza ambaye amepoteza wanafamilia 25 katika mzozo unaoendelea Gaza tangu Oktoba 2023, na sasa amebaki na wanafamilia wawili ambao mmoja wao ni shangazi yake ambaye ni mzee, na shangazi huyu muda wote anamshikilia na kumkumbatia kwani ana hofu asiachwe mwenyewe.