Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres asisitiza viongozi kubadili mwelekeo kuhusu changamoto za dunia wakati wa UNGA80

Katibu Mkuu António Guterres (Kusohoto) akihojiwa na Melissa Fleming Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa DGC
United Nations/Roberta Politi Katibu Mkuu António Guterres (Kusohoto) akihojiwa na Melissa Fleming Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa DGC

Guterres asisitiza viongozi kubadili mwelekeo kuhusu changamoto za dunia wakati wa UNGA80

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito mkali kwa viongozi wa dunia katika mkesha wa wiki ya ngazi ya juu ya Mjadala  Mkuu wa Bazeaza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA80, akionya kwamba mgogoro wa dunia wa vita, mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa usawa na hatari za kiteknolojia unahitaji hatua za haraka na za pamoja.

“Tunakabiliwa na zahma ya dunia. Migogoro inazidi kuongezeka katika muktadha ambao mgawanyiko wa kijiografia hauruhusu kushughulikiwa kwa ufanisi,” Bwana Guterres ameiambia UN News katika mahojiano na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa, Melissa Fleming.

“Kuna hali ya kutoadhibiwa kila nchi inaamini inaweza kufanya chochote itakacho. Kwa upande mwingine, tunaona kwamba nchi zinazoendelea zinakabiliwa na changamoto kubwa. Nyingi zimezama kwenye madeni bila kupata ufadhili wa masharti nafuu wanaohitaji ili kurekebisha uchumi wao. Pengo la kutokuwepo kwa usawa linaongezeka.”

Mabadiliko makubwa ya misimu ya mvua kutokana na janga la mabadiliko ya tabianchi yameathiri kwa kiasi kikubwa kilimo na maisha ya jamii katika eneo hili.
© Unsplash/Bogomil Mihaylov Mabadiliko makubwa ya misimu ya mvua kutokana na janga la mabadiliko ya tabianchi yameathiri kwa kiasi kikubwa kilimo na maisha ya jamii katika eneo hili.

Ushirikiano wa kimataifa ni wa lazima

Katibu Mkuu amebainisha nyanja nyingi ambazo Umoja wa Mataifa unajitahidi kuhamasisha ushirikiano wa kimataifa.

“Mabadiliko ya tabianchi bado hayajakoma. Na tuna dalili kadhaa kwamba huenda ikawa vigumu sana kutimiza lengo letu kuu, ambalo ni kudhibiti ongezeko la joto duniani lisipite nyuzi joto 1.5° C,” amesema, akirejelea makubaliano ya Paris ya mwaka 2015 kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Ameonya pia kwamba wakati teknolojia inaleta matumaini, inaweza pia kuchochea mgawanyiko na kauli za chuki, hivyo uongozi lazima “uhakikishe kwamba uwezo wa kibinadamu unabaki na teknolojia inakuwa nguvu ya manufaa.”

Bwana Guterres amesema kwamba mkutano wa wiki ijayo lazima utoe ahadi katika maeneo muhimu ambayo ni kupunguza hewa chafuzi, mageuzi ya kifedha ya kimataifa, na kuimarisha mshikamano wa kimataifa.

Amewahimiza viongozi “kubadilisha mwelekeo na kukubali mageuzi ya muundo wa kifedha wa kimataifa kwa ajili ya haki na usawa mkubwa zaidi.

Mtazamo juu ya Mashariki ya Kati

Amani na usalama pia vitakuwa kitovu cha mijadala. Katibu Mkuu amesema anatarajia msaada wa wazi kwa suluhu ya mataifa mawili kumaliza mzozo wa Israel na Palestina na hatua za haraka kushughulikia janga la kibinadamu huko Gaza.

“Mauaji yanayoendelea Gaza lazima yakome, tunahitaji kusitisha mapigano mara moja sambamba na kuachiwa kwa mateka wote mara moja pia,” amesema.

Amebainisha pia Sudan na migogoro mingine iitwayo “iliyopuuzwa,” akihimiza Baraza la Usalama kuungana ili kuzuia mateso zaidi.

Kiwanda cha nguvu cha Photovoltaic cha jua kwenye paa la Jumba la UN, New Delhi, India.
© UNDP India Kiwanda cha nguvu cha Photovoltaic cha jua kwenye paa la Jumba la UN, New Delhi, India.

Hatua za tabianchi zahitajika sasa

Bwana Guterres amemwambia Bi. Fleming kwamba dhamira yake ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi kupitia hatua za dharura haijabadilika.

“Kila nchi mwanachama lazima iwasilishe mpango wake mpya wa tabianchi ambao utaleta upunguzaji mkubwa wa hewa chafuzi ili kuepuka hali ya kutodhibitika ambayo italeta maafa makubwa sana kwa watu kote duniani,” amesema, akibainisha kwamba nchi zilizo hatarini zaidi, ikiwemo visiwa vidogo vinavyoendelea na Afrika, zinakabiliwa na hatari kubwa zaidi.

Nimeazimia

Kwa mtazamo binafsi, amesema alikataa ushauri wowote wa kukata tamaa.

“Nina matumaini wala si mtu wa kukata tamaa, bali nimeazimia lazima tujenge matumaini na tusikate tamaa kamwe hadi tufikie malengo yetu.”