Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na CERF waanzisha mpango wa dharura kuimarisha uhakika wa chakula nchini Haiti

Raia wa Haiti wakiwa kwenye foleni kupokea mifuko ya mbegu ya kupanda huko Jeremie, Idara ya Grand'Anse, mojawapo ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na Kimbunga Matthew.
FAO/ Justine Texier
Raia wa Haiti wakiwa kwenye foleni kupokea mifuko ya mbegu ya kupanda huko Jeremie, Idara ya Grand'Anse, mojawapo ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na Kimbunga Matthew.

FAO na CERF waanzisha mpango wa dharura kuimarisha uhakika wa chakula nchini Haiti

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na Mfuko wa Dharura wa Umoja wa Mataifa (CERF), wameanzisha mpango wa dharura katika mikoa ya Kaskazini na Kati ya Haiti ili kutoa msaada muhimu kwa kaya zilizo hatarini zaidi na zinazokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, katikati ya ongezeko la watu waliolazimika kuhama makazi yao, mzozo wa kurejeshwa kwa wahamiaji na athari zinazozidi kuwa mbaya za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa FAO na CERF mpango huu unalenga watu waliopoteza makazi, wahamiaji wanaorejeshwa kutoka Jamhuri ya Dominika, pamoja na jamii zinazowapokea, kwa kuwawezesha familia kuzalisha chakula chao na kuongeza uwezo wao wa kustahimili athari za mara kwa mara za majanga ya asili.

Hali ya sasa ya uhakika wa chakula nchini Haiti

Yamesema msaada huu unakuja wakati muhimu sana. Karibu kila mtu mmoja kati ya wawili nchini Haiti yuko katika Kiwango cha 3 cha IPC cha kutokuwa na uhakika wa chakula au zaidi, kulingana na uchambuzi wa IPC wa Septemba 2024 kuhusu Uhakika wa Chakula. Idadi kubwa ya walioathirika wanaishi vijijini na wanategemea kilimo na ufugaji.

Hii ina maana kuwa familia hulazimika kuruka baadhi ya milo au kula kidogo ili kuendelea kuishi, lakini bado hukabiliwa na upungufu wa chakula na hatari ya utapiamlo, huku wengine wakikumbwa na uhaba mkubwa wa chakula na kulazimika kuchukua hatua za kukata tamaa ili kuendelea kuishi.

Maeneo na kaya zitakazosaidiwa

Kupitia mfuko wa CERF, mpango huu utasaidia kaya 1,500 za vijijini zilizo hatarini, takriban watu 7,500, walioko katika kambi za wakimbizi wa ndani na familia zinazowapokea wahamiaji waliorejeshwa katika tarafa za:

  • Dondon
  • Plaine du Nord (Kaskazini)
  • Belladère
  • Lascahobas (Kati)
FAO inafanya kazi ya kusambaza mbegu bora nchini Haiti ili kurejesha uzalishaji wa mazao.
© FAO/Nour Azzalini
FAO inafanya kazi ya kusambaza mbegu bora nchini Haiti ili kurejesha uzalishaji wa mazao.

Hatua Kuu za Mpango huu

1. Msaada wa dharura wa uzalishaji wa chakula

Kaya 1,200 za vijijini (watu 6,000) wanapokea:

  • Tani 9 za maharagwe meusi
  • Tani 3 za mbegu za karanga zinazofaa kwa maeneo yenye ukame
  • Vipando 600,000 vya majani aina ya elephant grass

Pembejeo hizi zinatarajiwa kuzalisha zaidi ya tani 250 za chakula ndani ya siku 90 — kiasi cha kutosha kulisha kaya 8,000 kwa muda wa miezi sita — na kuboresha utofauti wa lishe.
Familia pia zinapokea msaada wa fedha taslimu usio na masharti ili kukidhi mahitaji ya chakula ya haraka na kuepuka kuuza pembejeo za kilimo walizopewa.

2. Ukarabati wa njia za kujipatia riziki

Watu 300 wanakarabati:

  • Zaidi ya kilomita 19 za mifereji ya umwagiliaji
  • Kurejesha maji kwenye maeneo ya kilimo kati ya hekta 100 hadi 300
  • Kujenga vibanda 200 vya kuhifadhi na kulinda mbuzi 1,200 au wanyama wadogo wengine

Hatua hizi zinaboresha uzalishaji wa chakula na kutoa fursa za mapato, kwa faida ya takriban watu 1,500 kutoka kaya 300.

3. Mafunzo ya kilimo hifadhi na kinachoendana na hali ya hewa

Wakulima 400 watapokea mafunzo ya vitendo juu ya:

  • Mbinu za kilimo hifadhi
  • Njia za kuongeza tija
  • Uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi

Maeneo yaliyoathirika zaidi

Tarafa zinazolengwa ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi na changamoto za kijamii na mabadiliko ya hali ya hewa.

  • Belladère ni lango kuu la zaidi ya nusu ya wahamiaji wanaorejeshwa kutoka Jamhuri ya Dominika na linahifadhi idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani.
  • Katika Lascahobas, ghasia zilizozuka hivi karibuni zimeathiri masoko ya ndani na shughuli za kilimo.

Kauli ya FAO kuhusu umuhimu wa mpango huu

Nchini Haiti, uzalishaji wa dharura wa chakula na maandalizi dhidi ya majanga ya hali ya hewa si tu hatua za haraka za dharura: ndizo njia pekee zenye ufanisi wa kuleta athari za kudumu na kuwawezesha jamii za vijijini,” amesema Pierre Vauthier, Mwakilishi wa FAO nchini Haiti.

“Mpango huu wa dharura unasaidia kukidhi mahitaji ya haraka huku ukiweka msingi wa maandalizi ya muda mrefu dhidi ya majanga katika jamii za eneo husika, ukiwawezesha wakulima kuzalisha chakula, kulinda mali zao na kuendana na mabadiliko ya tabianchi.”

Kuunganisha msaada wa muda mfupi na mipango ya muda mrefu

Kwa kuweka pamoja msaada wa muda mfupi na hatua za muda mrefu za kujiandaa na kukabiliana na majanga, FAO na CERF wanashirikiana moja kwa moja na jamii za vijijini ili:

  • Kulinda njia zao za kujipatia riziki
  • Kuimarisha usalama wa chakula
  • Kuweka msingi wa urejeshwaji wa hali na utulivu wa maisha yao