“Pamoja ni Bora Zaidi” ni kaulimbiu itakayotawala UNGA80: Baerbock
“Pamoja ni Bora Zaidi” ni kaulimbiu itakayotawala UNGA80: Baerbock
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, amewataka viongozi wa dunia kukumbatia mshikamano na kuchukua hatua za dhati wakati kikao cha 80 cha Umoja wa Mataifa kikiendelea kwa kaulimbiu ya “Pamoja ni Bora Zaidi.”
“Hakuna taifa moja, haijalishi ukubwa wake, nguvu au utajiri wake, linaloweza kukabiliana na changamoto tunazokabiliana nazo peke yake,” Bi. Baerbock amewaambia waandishi wa habari leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.
Ameeleza vipaumbele vyake kwa kikao hiki, kuwa ni pamoja na kuendeleza ajenda ya marekebisho ya UN80, kuimarisha ufanisi wa shirika, na kuongoza mchakato wa uteuzi wa Katibu Mkuu ajaye.
SDGs na makataba wa Zama Zijazo
Pia Bi. Baerbock amesisitiza haja ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na utekelezaji wa mkataba wa Zama Zijazo.
“Ndiyo, tupo katika njia panda huu ni wakati wa kufanya maamuzi ya kufanikisha au kushindwa,” amesema kwa msisitizo. “Waasisi wetu walikuwa na unyenyekevu na hekima ya kuweka kando tofauti zao na kushirikiana mwaka 1945, tunahitaji msimamo huo wa msingi leo.”
Rais huyo wa Baraza Kuu ameonya kuwa maneno matupu hayatoshi bila hatua za kweli. “Iwapo tunataka kuufanya Umoja wa Mataifa uwe imara zaidi na ufanisi zaidi, basi tunahitaji ahadi kutoka kwa serikali zote duniani,” amesema, akizitaka nchi wanachama kuzingatia ufadhili wa Umoja wa Mataifa sambamba na vipaumbele vya kimataifa kama vile amani na usalama, hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, haki za binadamu na maendeleo endelevu.
Bi. Baerbock ameongeza kuwa masuala haya ndiyo yatakayoongoza mazungumzo yake ya ana kwa ana na wakuu wa nchi wakati wa wiki ya mjadala wa viongozi wa ngazi ya juu, itakayoanza tarehe 22 Septemba hadi tarehe 30 Septemba.