Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 9 kati ya 10 Afghanistan wanaunga mkono elimu: UN Women

Wasichana na wanawake Afghanistan wanapitia vikwazo lukuki
© UN Women/Sayed Habib Bidell Wasichana na wanawake Afghanistan wanapitia vikwazo lukuki

Watu 9 kati ya 10 Afghanistan wanaunga mkono elimu: UN Women

Utamaduni na Elimu

Miaka minne ya marufuku ya utawala wa Taliban kwa wasicha kupata elimu ya juu zaidi ya darasa la sita imekuwa jinamizi kubwa na hakuna dalili yoyote ya mabadiliko umesema Umoja wa Mataifa ukisisitiza mshikamano wa kimataifa kutatua hali hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake (UN Women), zaidi ya watu tisa kati ya kumi nchini Afghanistan wanaunga mkono elimu ya sekondari kwa wasichana.

Na wakati nchi bado inapambana na athari za tetemeko la ardhi la hivi karibuni jukumu ambalo limekuwa gumu zaidi kutokana na marufuku ya Taliban dhidi ya wafanyakazi wa misaada wa kike mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wake wamerudia wito wao kwamba kila msichana wa Afghanistan aruhusiwe kwenda shule.

Mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa na washirika wao, likiwemo la Elimu Haiwezi Kusubiri ECW, yamelaani marufuku inayoendelea na kuyataka mataifa ya dunia kuungana katika kuunga mkono elimu kwa wasichana wote nchini Afghanistan.

Kwa mujibu wa UN Women kwa sasa, zaidi ya wasichana milioni 2.2 wa Afghanistan wamezuiwa kuhudhuria shule baada ya shule ya msingi, idadi hiyo imeelezwa kwenye takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa. Kwa jumla, hadi watoto milioni saba hawako darasani kwa sababu ya marufuku hiyo na vikwazo vingine.

Wasichana wanafunzi nchini Afghanistan wakitengeneza roboti (Kutoka maktaba)
© UNICEF/Frank Dejo Wasichana wanafunzi nchini Afghanistan wakitengeneza roboti (Kutoka maktaba)

Madhila ya Taliban nimeyaishi-Fatima muathirika

Bi. Fatima Amiri mmoja wa waathirika wa marufuku hiyo  ametoa ushuhuda wake katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva, ambapo alizungumza na Daniel Johnson wa UN News akisema “Mimi ni mfano tu wa wasichana na wanawake wengi nchini Afghanistan ambao wamekataliwa haki. Mimi ni mtu ambaye amehisi kila aina ya maumivu ambayo wasichana katika nchi yangu wanapitia. Jambo pekee ninaloweza kufanya ni kuwa sauti yao, kuzungumza na dunia na kufikisha ujumbe wao kwa watu wengine ili waweze kuwasaidia”.

Athari mbaya kwa haki za wasichana na wanawake kutokana na kurejea kwa Taliban zimelaaniwa kwa upana na jumuiya ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa. Fatima anaeleza  hali hii inamaanisha nini kwa marafiki zake walioko bado Afghanistan

“Imefika miaka minne sasa watu nchini Afghanistan wanakabiliana na matatizo haya, shule zimefungwa, vyuo vikuu vimefungwa na hali kwa wanawake ni ngumu. Shida ni kwamba, tunazungumza tu lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.”

Ameongeza kuwa kwa miaka hiyo minne  anaona “Hakuna mabadiliko nchini Afghanistan kila siku, bado shule zimefungwa, bado vyuo vikuu vimefungwa, bado mwanamke hawezi kutoka nje peke yake. Kwa hiyo, kuzungumza pekee hakutoshi, tumezungumza sana, sasa ni wakati wa kuchukua hatua, tunahitaji vitendo.”