Mjumbe wa UN aonya kuhusu zahma kubwa ya migogoro Afghanistan
Mjumbe wa UN aonya kuhusu zahma kubwa ya migogoro Afghanistan
Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mstaifa nchini humo UNAMA Roza Otunbayeva, ameonya leo mbele ya Baraza la Usalama kuwa Afghanistan inakabiliwa na dhoruba kamili ya migogoro inayochochewa na kuyumba kwa uchumi, kupunguzwa kwa misaada, majanga ya tabianchi, na vizuizi vya Taliban dhidi ya wanawake na wasichana.
Akizungumza kwa njia ya video kwenye kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali ya Afghanistan mjini New York Bi. Otunbayeva ametoa wito wa kuendelea kwa ushirikiano wa kimataifa, licha ya mamlaka za kiimla nchini humo kuendeleza sera za kibaguzi.
Kizazi kizima kiko hatarini
Otunbayeva amesema jambo la kutisha zaidi ni marufuku ya Taliban dhidi ya elimu ya sekondari na ya juu kwa wasichana na vizuizi kwa wanawake wa Afghanistan kufanya kazi katika mashirika yasiyo ya kiserikali NGO na Umoja wa Mataifa.
Ameliambia Baraza la Usalama kwamba “Baada ya zaidi ya miaka mitatu na nusu ya kufungwa kwa shule za wasichana zaidi ya darasa la sita, kizazi hicho kimoja kipo hatarini kupotea. Hii inaleta gharama kubwa na ya muda mrefu kwa nchi na inaleta wasiwasi na huzuni kubwa kwa jamii ya Afghanistan kwa ujumla.”
Mabilioni ya misaada, lakini mafanikio duni
Mjumbe huyo ameongeza kuwa tangu kuchukua madaraka kwa Taliban mwaka 2021, jumuiya ya kimataifa imetoa takribani dola bilioni 13 za misaada, hatua iliyosaidia kuepusha njaa na kuendeleza huduma za msingi.
Lakini Otunbayeva ameonya kuwa vizuizi vipya dhidi ya wafanyakazi wanawake vimekwamisha kazi ya kuokoa maisha.
“Kizuizi hiki kikubwa kinaathiri uwezo wa Umoja wa Mataifa kuwasaidia wananchi wa Afghanistan katika kipindi hiki kigumu,” amesema, akirejelea vizuizi vya kuingia kwa wafanyakazi wanawake kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa kote nchini Afghanistan.
Wakati Afghanistan imeshuhudia kupungua kwa mapigano makubwa na Taliban kutekeleza marufuku ya kilimo cha afyunyi au poppy, Otunbayeva amesema utulivu bado ni dhaifu. “Utekelezaji wa jumla wa msamaha wa jumla uliotangazwa Agosti 2021 ni wa kutia moyo baada ya miongo kadhaa ya vita vya kikatili,” amebainisha akiongeza kuwa “Lakini ukiukaji Mkubwa unaendelea, na kila mmoja ni wa kulaumiwa.”
Changamoto za uchumi na tabianchi
Mjumbe huyo ametaja ongezeko la umaskini, ambapo asilimia 75 ya Waafghanistan wanaishi kwa kiwango cha kujikimu, hali ikizidishwa na ukame, matetemeko ya ardhi, na kurejea kwa wakimbizi zaidi ya milioni mbili kutoka nchi jirani.
Bi. Otunbayeva ameonya kwamba “Kabul, mji wenye takribani wakazi milioni sita, unaweza kuwa mji wa kwanza wa kisasa kuishiwa na maji katika miaka michache ijayo”.
Mjumbe huyo amelikiri kwamba kuna mgawanyiko ndani ya uongozi wa Taliban, kati ya wale wanaotafuta njia ya vitendo na wanaosukuma vizuizi vya kiitikadi. “Ni swali lililo wazi kama kuna uhalisia wa kutosha miongoni mwa mamlaka za kiimla kushughulikia dhoruba hii kamili ya migogoro,” amesema. “Maamuzi yanayoendeshwa na itikadi yanahatarisha kuongeza mateso ya watu wa Afghanistan na kudhoofisha uthabiti uliopo.”
Ujumbe wa kuaga
Akijiandaa kumaliza jukumu lake la miaka mitatu, Otunbayeva amehimiza Baraza la Usalama kusalia na mshikamano. “Waafghanistan wengi wanataka ushirikiano kati ya jumuiya ya kimataifa na nchi yao uendelee, licha ya vikwazo,” amesema. “Ni matumaini yangu makubwa kuwa njia itapatikana ya kuleta matokeo chanya zaidi, hasa kwa wanawake na wasichana wa Afghanistan.”