Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka minne ya kunyima elimu wasichana wa Afghanistan ni “Moja ya uonevu mkubwa wa wakati wetu” - UNICEF

Wanawake wakijifunza kusoma na kuandika kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa unaoungwa mkono na Wanawake wa kusoma na kuandika katika jimbo la Nuristan, mashariki mwa Afghanistan.
© UN Women/Sayed Habib Bidell
Wanawake wakijifunza kusoma na kuandika kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa unaoungwa mkono na Wanawake wa kusoma na kuandika katika jimbo la Nuristan, mashariki mwa Afghanistan.

Miaka minne ya kunyima elimu wasichana wa Afghanistan ni “Moja ya uonevu mkubwa wa wakati wetu” - UNICEF

Haki za binadamu

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, Catherine Russell, ametahadharisha vikali kuhusu marufuku inayoendelea ambayo imewazuia kwa kipindi cha miaka minne sasa wasichana balehe nchini Afghanistan kuhudhuria shule akiiita “tishio kubwa” kwa mustakabali wa taifa hilo.

Kwa mujibu wa UNICEF, kufikia mwisho wa mwaka huu 2025, zaidi ya wasichana milioni 2.2 wa Afghanistan watakuwa wamenyimwa haki ya kupata elimu zaidi ya darasa la sita. Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi kufuatia kurejea kwa zaidi ya Waafghanistani milioni mbili kutoka nchi jirani mwaka huu, hali inayoongeza changamoto za upatikanaji wa elimu.

Watoto wawili wadogo wameketi karibu na mali ya familia yao kwenye kivuko cha mpaka cha Islam-Qala, saa chache baada ya kurejea Afghanistan.
© UNICEF/Osman Khayyam
Watoto wawili wadogo wameketi karibu na mali ya familia yao kwenye kivuko cha mpaka cha Islam-Qala, saa chache baada ya kurejea Afghanistan.

Kupitia ujumbe wake uliochapishwa leo na UNICEF jijini New York, Marekani, Russell amesisitiza umuhimu wa wanawake wenye elimu katika uokoaji na maendeleo ya Afghanistan, hususan baada ya tetemeko la ardhi lililosababisha vifo vya watoto 1,172. “Nafasi ya wahudumu wa afya na kijamii wa kike wenye elimu na mafunzo kamili haijawahi kuonekana wazi kama sasa,” amesema, akibainisha kuwa mgawanyiko wa kijinsia unazuia wanaume kuwahudumia wanawake na familia nyingi zenye uhitaji.

Wakati mamilioni ya watoto kote ulimwenguni wanarejea shuleni mwezi huu, wasichana wa Afghanistan wanaendelea kunyimwa haki ya msingi ya elimu, hali ambayo Russell anaitaja kama “moja ya dhulma kubwa za wakati wetu.” Ameonya kuwa kuzuia elimu kwa nusu ya idadi ya watu kunadhoofisha uthabiti wa muda mrefu na maendeleo ya kiuchumi ya taifa.

Kiongozi huyo wa UNICEF pia ameeleza wasiwasi kuhusu athari za kijamii za marufuku hiyo, akitaja ongezeko la changamoto za afya ya akili, ndoa za utotoni na viwango vya juu vya uzazi miongoni mwa wasichana waliolazimishwa kubaki majumbani.

Baba na mtoto wakiondoa kifusi kufuatia tetemeko la ardhi mapema Septemba katika jimbo la Kunar, Afghanistan.
© UNICEF/Amin Meerzad
Baba na mtoto wakiondoa kifusi kufuatia tetemeko la ardhi mapema Septemba katika jimbo la Kunar, Afghanistan.

“Wasichana wa Afghanistan wanapoteza zaidi ya masomo darasani; wananyimwa mawasiliano ya kijamii, ukuaji binafsi, nafasi ya kuunda mustakabali wao na kutimiza uwezo wao,” amesema Russell.

UNICEF inatoa wito wa haraka kwa mamlaka za Afghanistan kuondoa marufuku hii na kuruhusu kila msichana nchini Afghanistan kupata elimu kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na kuendelea.