Mkuu wa UN aonya kuhusu migawanyiko ya kimataifa kabla ya Mkutano wa UNGA80
Mkuu wa UN aonya kuhusu migawanyiko ya kimataifa kabla ya Mkutano wa UNGA80
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito kwa viongozi wa dunia “kuwa makini na kutekeleza ahadi” wanapowasili jijini New York kwa ajili ya wiki ya ngazi ya juu ya Mkutano wa Baraza Kuu wa 80 wa Umoja wa Mataifa UNGA80.
Wito wa kuchukua hatua
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito kwa viongozi wa dunia “kuwa makini na kutekeleza ahadi” wanapowasili jijini New York kwa ajili ya wiki ya ngazi ya juu ya Mkutano wa Baraza Kuu wa 80 wa Umoja wa Mataifa UNGA80.
Mshikamano wa kimataifa hatarini
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoha wa Mataifa leo Jumanne, Bwana Guterres ameonya kuwa migawanyiko, migogoro na misukosuko ya kimataifa imepeleka mshikamano wa kimataifa katika hali dhaifu zaidi katika miongo kadhaa.
“Wengine huiita kombe la dunia la diplomasia,” amesema. “Lakini hii siyo kuhusu kushindana kwa maneno ni kuhusu kutafuta suluhu. Mambo yaliyoko mezani ni makubwa mno.”
Changamoto kuu duniani
Katibu Mkuu ameelezea dunia kama “imetumbukia kwenye maji yenye dhoruba, isiyojulikana,” akitaja migawanyiko ya kijiografia ya kisiasa, mizozo inayoongezeka, mabadiliko ya tabianchi, maendeleo holela ya teknolojia na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa kama changamoto zinazohitaji hatua za haraka.
Viongozi 150 watarajiwa New York
Takribani wakuu wa nchi na serikali 150 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo, wakiwa pamoja na maafisa na wanadiplomasia maelfu.
Bwana Guterres amesema atafanya zaidi ya mikutano ya pande mbili 150, akiwahimiza viongozi “kupunguza migawanyiko, kupunguza hatari na kupata suluhisho.”
Mada kuu za mkutano
Mada kuu za wiki hiyo ya ngazi ya juu zitakuwa ni amani, mabadiliko ya tabianchi, ubunifu wenye uwajibikaji, usawa wa kijinsia, ufadhili wa maendeleo na mageuzi ya Umoja wa Mataifa.
Amerudia wito wa kusitisha vita Gaza, Ukraine, Sudan na maeneo mengine, na kusisitiza haja ya Suluhu ya mataifa mawili Mashariki ya Kati.
Tabianchi na teknolojia
Kuhusu tabianchi, Bwana Guterres amewataka mataifa kuwasilisha mipango bora zaidi ya kitaifa ili kufanikisha lengo la nyuzi joto 1.5°C kama ilivyowekwa katika Mkataba wa Paris wa mwaka 2015, akionya kuwa lengo hilo liko hatarini.
Pia ametangaza kuanzishwa kwa “Mazungumzo ya Kimataifa kuhusu udhibiti wa Akili Mnemba AI” kuhakikisha teknolojia inatumikia maslahi ya binadamu.
Mikutano ya kifedha na kumbukumbu muhimu
Wiki hii pia itajumuisha mkutano wa kilele wa kwanza wa kila baada ya miaka miwili, utakaozikutanisha taasisi za kifedha za kimataifa na viongozi wa dunia kusukuma mbele utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambayo yamepoteza mwelekeo pamoja na kumbukumbu ya miaka 30 ya mkutano muhimu wa Beijing kuhusu usawa wa kijinsia.
Ujumbe wa mwisho
Amehitimisha akisema “Orodha ni ndefu kwa sababu mahitaji ni makubwa,” amesema. “Lakini dunia haitaki maigizo na ahadi tupu. Inahitaji uongozi na hatua za dhati. Umoja wa Mataifa ndio mahali. Wiki ijayo ndiyo wakati. Viongozi wanapaswa kuwa makini na kutekeleza.”