Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumejipanga vema tayari kuhudumia UNGA80 - Kamishna wa Masuala ya Kimataifa wa jiji la New York, Marekani

Ishara nje ya jengo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inaangazia alama ya reli kwa waliohudhuria kuitumia kuendeleza Mjadala Mkuu.
UN Photo/Kim Haughton Ishara nje ya jengo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inaangazia alama ya reli kwa waliohudhuria kuitumia kuendeleza Mjadala Mkuu.

Tumejipanga vema tayari kuhudumia UNGA80 - Kamishna wa Masuala ya Kimataifa wa jiji la New York, Marekani

Na Monica Grayley
Masuala ya UM

Wakazi wa jiji la New York, Marekani wanakijua vyema kipindi hiki cha mwaka. Wageni huanza kuwasili jijini, usalama huimarishwa, na barabara hufungwa au kubadilishwa matumizi yake, hasa zile zinazoelekea ‘First Avenue’ ya Manhattan, ambako ndiko makao makuu ya Umoja wa Mataifa yalipo.

Katika Mtaa huu wa kwanza, udhibiti ni mkali. Ni magari yenye vibali maalum pekee, yanayobeba ujumbe wa karibu marais na wakuu wa serikali mia mbili kutoka kote duniani, ndiyo yanayoruhusiwa kupita. Huu ni ufunguzi wa Mjadala Mkuu wa Umoja wa Mataifa, unaokusanya viongozi wa kimataifa, wawakilishi wa jamii ya kiraia, na vyombo vya habari vya dunia.

Wanausalama wa kimarekani

Na “jiji lisilolala” linaonekana kupokea kwa kawaida Wiki ya Ngazi ya Juu, ambayo huambatana na ongezeko la milio ya ving’ora na idadi ya polisi, wakiwemo ‘Secret Service’, wanaolinda usalama wa tukio hilo.

Idhaa ya Umoja wa Mataifa kupitia Idhaa ya Kireno imezungumza na  Kamishna wa Masuala ya Kimataifa wa Jiji la New York, Marekani, Aissata Camara, kuhusu ufunguzi wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na namna jiji linavyoshirikiana na Umoja wa Mataifa kuhakikisha mafanikio ya tukio hilo.

Kwa upande wake, akiwa amefanya kazi katika eneo hili kwa zaidi ya muongo mmoja mkutano huu ni miongoni mwa mikutano muhimu zaidi kutokana na muktadha wa kisiasa uliopo sasa.

NYC Mayor's Office of International Affairs/Carolina Nazzaro
Aissata Camara ndiye mwanamke wa kwanza Mwafrika kuwa Kamishna wa Masuala ya Kimataifa wa Jiji la New York. NYC Mayor's Office of International Affairs/Carolina Nazzaro

Dunia iliyogawanyika

Kwa Kamishna wa Jiji la New York, huu ni miongoni mwa Mikutano Mikuu yenye umuhimu mkubwa zaidi, kwa sababu ya changamoto nyingi zinazojitokeza duniani, changamoto zinazowagawanya watu kimataifa. Kwa mujibu wake, Mkutano Mkuu ni mahali ambapo wadau wote watakutana kutafuta suluhu ya pamoja.

Aissata Camara anasema Jiji la New York lina maafisa wa polisi 50,000 walioko kazini masaa 24 kila siku, siku saba kwa wiki. Anaulinganisha Mkutano Mkuu na Super Bowl ya kidiplomasia, akirejelea tukio kubwa zaidi la kila mwaka nchini Marekani.

“Kwa hiyo kwetu, wakati wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, tunataka kuhakikisha kwamba wajumbe wote na kila mtu anayekuja New York anakuwa salama. Na tunafanya hivyo kupitia maandalizi ya pamoja ya wadau mbalimbali, katika ngazi ya jiji tukizungumza na wenzetu, lakini pia kupitia mikutano ya pamoja na taasisi zingine inayofanyika Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Ulinzi wa Umoja wa Mataifa na wadau wengine pia.” Anasema Camara.

Kamishna huyo anasema kwamba UNGA ndiyo Super Bowl ya kila mwaka, na kwa hiyo macho ya dunia yote yako kwa Jiji la New York. Anaongeza kwamba wanadiplomasia na wageni kutoka kote ulimwenguni wanapaswa pia kutumia nafasi hiyo kulitembelea Jiji la New York na kufurahia utajiri wake wa kitamaduni.

Kwa mujibu wa Kamishna, Umoja wa Mataifa ni chanzo kikubwa cha mapato, ukizalisha dola bilioni 4.9 za Kimarekani kila mwaka. Na wiki hizi mbili ndiyo zinazokuwa zenye shughuli nyingi zaidi katika mwaka wa bajeti ya jiji.

 

*Monica Grayley ni Mhariri Mkuu wa Idhaa ya Kireno ya Umoja wa Mataifa