UNMISS yasaidia mahakama kusikiliza mrundikano wa kesi
UNMISS yasaidia mahakama kusikiliza mrundikano wa kesi
Nchini Sudan Kusini ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS unaendelea kuimarisha mfumo wa mahakama ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wote hata maeneo yote ya nchi hiyo.
Mtuhumiwa akiwa rumande inachukua miaka 10 kabla ya kesi yake kuanza kusikilizwa.
Hiyo sio hadithi ni maisha halisi ya baadhi ya watu wa Sudan kusini na sababu kubwa ni uhaba wa majaji na maafisa wa kisheria.
Waswahili husema mficha uchi hazai, mhimili wa mahakama ukabisha hodi kwenye ofisi za ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS ili iwasaidie kupeleka majaji katika maeneo ya mbali ambayo hayajawahi kupata huduma hizo kwa zaidi ya muongo mmoja.
Afisa mwandamizi wa Utawala wa sheria wa UNMISS Samuel Wambugu anasema,“Moja ya malengo makuu ya mahakama ni kuongeza upatikanaji wa haki, na chini ya lengo hilo, moja ya vipaumbele vya kimkakati vya utawala wa sasa ni kuwa na uwezo wa kupeleka majaji, hasa katika maeneo ya mbali katika majimbo ambayo hatujapata majaji kwa muda mrefu. Walitufikia ili tuweze kuwasaidia na katika kuandaa utaratibu wa kupeleka majaji katika maeneo ambayo hawakupewa majaji kwa kipindi cha miaka 10.”
Katika maeneo ya vijijini, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 80 ya mizozo ya kisheria hutatuliwa na mahakama za kimila zinazoongozwa na machifu. Serikali inalenga kufanya mifumo hii miwili ilew rasmi na wakimila ifanyekazi pamoja huku ikizingatia katiba na haki za binadamu.
Afisa Wambugu ataeleza kuwa kwakupelekwa kwa majaji wa kudumu maeneo yasiyo na majaji kunatarajiwa kusaidia kupunguza msongamano wa kesi na wafungwa.
“Kwa kuwa na majaji wa kudumu, tunakwenda kushuhudia kesi nyingi zaidi zikisikilizwa na kwa hilo tutaweza kupunguza tatizo kubwa la msongamano wa wafungwa.”
Kwa muda mrefu changamoto ya ufinyu wa rasilimali imekuwa ikichelewesha mchakato wa kisheria, na kusababisha watuhumiwa wengi kubaki rumande kwa muda mrefu bila kesi zao kusikilizwa.
Samuel Atok ni mwendesha mashtaka kutoka Bentiu, jimboni Unity
“Tunakabiliana na changamoto ya uhalifu wa ndani na nje ya jimbo letu. Watuhumiwa wengine wanashikiliwa katika gereza la Bentiu, na kwa kuwasili kwa majaji hivi karibuni, mashtaka yataanza kusikilizwa. Serikali ya jimbo imemwomba Jaji Mkuu kuteua majaji zaidi ili kupunguza mrundiko wa kesi.”
Kwa sasa, UNMISS inaendelea kushirikiana na mfumo wa mahakama nchini humo ili kuhakikisha majaji na waendesha mashtaka wanateuliwa na kusambazwa katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.