Katibu Mkuu wa UN alaani mauaji ya raia zaidi ya 40 nchini Haiti
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mauaji yaliyotekelezwa na magenge ya wenye silaha tarehe 11 Septemba 2025 katika eneo la Cabaret lililoko Magharibi mwa Haiti na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 40, wakiwemo wanawake, watoto na wazee.
Taarifa iliyotolewa hii leo kutoka jijini New York Marekani na msemaji wake imeeleza kuwa Katibu Mkuu anatuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa tukio hilo, wananchi na Serikali ya Haiti.
“Katibu Mkuu amesikitishwa na viwango vya ghasia zinazoikumba Haiti na kuzitaka mamlaka za Haiti kuhakikisha kuwa wahusika wa ukiukaji huo na ukiukaji wowote wa haki za binadamu wanachukuliwa hatua za kisheria” imesema taarifa hiyo.
Katibu Mkuu anatoa wito kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuharakisha juhudi za kuimarisha ujumbe wa Kimataifa wa Usaidizi wa Usalama (MSS) kwa kutoa vifaa vinavyohitajika, wafanyakazi na ufadhili ili kuwasaidia ipasavyo Polisi ya Kitaifa ya nchi ya Haiti katika kushughulikia ghasia za magenge nchini humo kwa heshima kamili ya sheria za kimataifa za haki za binadamu.