Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afisa wa UN asema mara ya kwanza ndege nyingi zisizo na rubani kupenya kwa kina kwenye anga la nchi jirani

Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Loey Felipe
Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Afisa wa UN asema mara ya kwanza ndege nyingi zisizo na rubani kupenya kwa kina kwenye anga la nchi jirani

Amani na Usalama

Alasiri ya Ijumaa Septemba 12, 2025, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kwenye kikao cha dharura kilichoitishwa na Poland kuhusu ndege zisizo na rubani za Urusi zilizorushwa na taifa hilo la Ulaya Mashariki kuelekea maeneo ya Belarus na hatimaye kuingia anga la Poland usiku wa kuamkia leo.

Rosemary DiCarlo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Masuala ya Siasa na Ujenzi wa Amani, DPPA ametumia fursa ya kikao hicho kueleza wajumbe kwamba tarehe 10 ya mwezi huu, Poland ilimjulisha Rais wa Baraza la Usalama kwamba usiku wa tarehe 9 na 10, ndege 19 za Urusi zisizo na rubani ziliingia katika anga ya Poland. Baadhi ya ndege hizo ziliangushwa mapema kwa tahadhari.

“Hii siyo mara ya kwanza ndege zisizo na rubani kugunduliwa katika nchi jirani wakati wa vita vya wazi nchini Ukraine,” amesema Bi. DiCarlo na kuongeza kwamba, “lakini hii ni mara ya kwanza ndege nyingi kama hizo kupenya kwa kina katika anga ya nchi jirani. Pia ni mara ya kwanza kwa Poland na washirika wake wa umoja wa Kujihami barani Ulaya, NATO kutumia nguvu kuondoa tishio hilo lililodhaniwa kuwepo.”

Ameongeza kuwa Wizara ya Ulinzi ya Urusi imeeleza kwamba Urusi haikuwa na nia ya kushambulia maeneo yoyote ndani ya ardhi ya Poland.

Hata hivyo, ndege hizo ziliripotiwa kusababisha uharibifu katika maeneo ya makazi ya vijiji vya Poland vya Wyryki na Czosnówka, na mabaki ya ndege hizo pia kuripotiwa mjini Czesniki. “Kwa bahati nzuri, mamlaka za Poland ziliripoti kuwa hakukuwa na majeruhi,” amesema Bi. DiCarlo.

Poland ‘haitasalimishwa na vitisho’

Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Marcin Bosaczki, katika hotuba yake, ametoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa “kujibu kwa pamoja, kwa kauli moja na mara moja dhidi ya vitendo vya kihalifu vya Urusi.”

Amesema kuwa hukumu hiyo ya wazi inapaswa kuwa hatua muhimu ya kuzuia, ili kupunguza mivutano na kuzuia matukio kama hayo kutokea tena.

“Kuhusu Urusi, tunatarajia iwajibike kikamilifu kwa kitendo hiki kisicho na msingi wowote, kutoa maelezo kamili juu ya sababu za uvamizi huo, na kuchukua hatua zote zinazohitajika kuhakikisha kuwa matukio kama haya hayajirudii tena katika siku zijazo,” amesema Bosaczki.

Amesisitiza kuwa, “njia ya kufikia lengo hilo ni rahisi: wacha vita vyako vya kikatili dhidi ya Ukraine. Poland haitasalimishwa na vitisho. Uamuzi wetu wa kuiunga mkono Ukraine na kutetea misingi ya mamlaka ya kitaifa na ukamilifu wa ardhi haubadiliki.”

Marekani: “Tutailinda kila nchi ya eneo la NATO”

“Marekani inasimama pamoja na washirika wake wa NATO mbele ya ukiukwaji huu wa kutisha wa anga,” amesema Dorothy Shea, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa.

Amebainisha kuwa Marekani inafanya mashauriano na Poland na washirika wengine wa NATO kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha Mkataba wa NATO.

“Muwe na uhakika, tutailinda kila nchi ya eneo la NATO,” amesisitiza na kuongeza kuwa, tukio hilo halichangii juhudi kubwa ambazo Marekani imekuwa ikifanya katika wiki za hivi karibuni za kumaliza vita.

Urusi haina nia ya kuongeza mvutano na Poland

Mwakilishi wa Kudumu wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Balozi Vasily Nebenzya, amekanusha tuhuma zote dhidi ya nchi yake kuhusiana na tukio hilo. Amesema kuwa usiku wa tarehe 10 Septemba, jeshi la Urusi lilishambulia maeneo ya viwanda vya kijeshi ndani ya ardhi ya Ukraine.

“Hakukuwa na malengo yoyote yaliyopangwa katika ardhi ya Poland,” amesema,na kuongeza kuwa, “umbali wa kuruka kwa ndege zisizo na rubani zilizotumika katika shambulio hilo haukuzidi kilomita 700, jambo linalozuia kimazingira uwezekano wa kuingia kwenye ardhi ya Poland.”