Nepal yateua Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke, huku UN ikionesha mshikamano
Nepal yateua Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke, huku UN ikionesha mshikamano
Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Nepal yamekaribisha uteuzi wa Sushila Karki kuwa Waziri Mkuu wa mpito, wakati nchi hiyo ikikumbwa na mshtuko kufuatia ukandamizaji wenye umwagaji damu dhidi ya maandamano yaliyoongozwa na vijana, ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 50, uharibifu mkubwa wa mali na kujiuzulu kwa mtangulizi wake.
Bi. Karki, ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke nchini Nepal, ameteuliwa Ijumaa Septemba 2025 na Rais Ram Chandra Poudel, ambaye alimwapisha katika hafla iliyohudhuriwa na wawakilishi wa vijana, maafisa wa serikali na wanadiplomasia wa kigeni.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, amepewa jukumu la kuandaa uchaguzi mpya ndani ya miezi sita.
Kabla ya hapo, amehudumu kama Jaji Mkuu wa kwanza mwanamke, akiiongoza Mahakama ya Juu kati ya mwaka 2016 hadi 2017.
Tukio la kihistoria
“Katika kipindi hiki cha mabadiliko muhimu, Umoja wa Mataifa unasimama pamoja na watu wa Nepal katika matarajio yao ya amani, haki, uwazi, uwajibikaji na maendeleo,” amesema Hanna Singer Hamdy, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Nepal.
Kupitia taarifa rasmi, ametambua mchango wa Rais, Mkuu wa Majeshi na viongozi vijana wa kizazi cha "Gen Z", akibainisha kuwa juhudi zao “zimesaidia kufanikisha kipindi hiki cha mpito.”
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na Serikali ya Nepal ili kuunga mkono utulivu, haki za binadamu na maendeleo endelevu.
Mvuto kwa wasichana na wanawake
Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limempongeza Bi. Karki, likisema kuwa uteuzi wake “ni motisha kwa wasichana na wanawake,” na likasisitiza umuhimu wa kuweka haki za watoto katikati ya mchakato wa kuijenga upya Nepal.
Vivyo hivyo, mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, lile la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Masuala ya Wanawake, UN Women, na Afya na IDadi ya watu, UNFPA wameeleza kuunga mkono uongozi wake, wakisisitiza juu ya uongozi jumuishi, usawa wa kijinsia, na ulinzi wa wanawake na vijana.
Soma zaidi hapa