Baraza Kuu laidhinisha Azimio la New York, kuhusu mataifa mawili Mashariki ya Kati
Baraza Kuu laidhinisha Azimio la New York, kuhusu mataifa mawili Mashariki ya Kati
Shangwe na vigelegele vilirindima katika Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani Ijumaa ya Septemba 12, 2025, wakati nchi wanachama zilipoidhinisha Azimio kuhusu suluhisho la amani la hoja ya Palestina na utekelezaji wa suluhisho la uwepo wa mataifa mawili, yaani Palestina na Israel.
Azimio la New York ni matokeo ya mkutano wa kimataifa uliofanyika mwezi Julai katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, ulioandaliwa na Ufaransa na Saudi Arabia, na ambao unatarajiwa kuendelea baadaye mwezi huu.
Baraza Kuu linajumuisha nchi wanachama wote 193 wa Umoja wa Mataifa, na mataifa 142 yalipiga kura kuunga mkono azimio linalounga mkono tamko hilo.
Nchi 10 zapinga azimio
Israel ilipinga azimio hilo, pamoja na nchi 9 nyingine – Argentina, Hungary, Mikronesia, Nauru, Palau, Papua New Guinea, Paraguay, Tonga na Marekani – huku mataifa 12 yakijizuia kupiga kura.
‘Ramani ya njia’ kwa siku zijazo
Kabla ya upigaji kura, Mwakilishi wa Kudumu wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Jérôme Bonnafont alikumbusha kwamba Azimio la New York "linaweka ramani ya njia moja kuelekea utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili."
Hili linajumuisha kusitishwa mara moja kwa mapigano huko Gaza, kuachiliwa kwa mateka wote walioko huko, na kuanzishwa kwa Taifa la Palestina litakalokuwa endelevu na lenye mamlaka kamili.
Azimio hilo linataka Hamas isalimishe silaha na kutengwa kwake kutoka uongozi wa Gaza, kurudishwa kwa mahusiano ya kawaida kati ya Israel na nchi za kiarabu, pamoja na dhamana za usalama wa pamoja.
Kauli ya Israeli
Akizungumza kabla ya kura, Mwakilishi wa Kudumu wa Israeli kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Danny Danon amesema, “Azimio hili lisilo na usawa halitakumbukwa kama hatua kuelekea amani, bali kama ishara nyingine isiyo na maana inayodhoofisha uaminifu wa Baraza hili.”
Amesema Hamas ndio mshindi mkubwa wa aina yoyote ya kuidhinishwa kwa azimio hili leo” na watadai kuwa ni “matunda ya tarehe 7 Oktoba.”
Tarehe 7 Oktoba 2023 ndio kipindi ambacho Hamas ilishambulia Israeli, hali iliyosababisha Israeli kujibu mashambulizi ambayo yamesababisha vita vinavyoendelea hadi leo hii.
Mkutano wa kimataifa wa ngazi ya juu wa mwezi Julai ulifanyika katika muktadha wa vita vya Gaza na hali mbaya inayozidi kuathiri matarajio ya suluhisho la mataifa mawili.
Guterres asisitiza suluhisho la mataifa mawili
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameeeleza kwamba, “swali kuu kuhusu amani ya Mashariki ya Kati ni utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili, ambapo mataifa mawili huru, yenye mamlaka kamili na ya kidemokrasia – Israel na Palestina – yataishi bega kwa bega kwa amani na usalama.”