Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO: Vifo vya kipindupindu vyaongezeka kwa mwaka wa pili mfululizo licha ya kinga na tiba kupatikana

Watoto na watu wazima wanaougua kipindupindu wanapokea matibabu katika kituo cha kujitenga katika hospitali moja mjini Khartoum, Sudan. Hali ni ya kutisha hasa katika eneo la Darfur Kaskazini, ambako zaidi ya watoto 640,000 wako hatarini.
© UNICEF/Ahmed Mohamdeen Elfatih Watoto na watu wazima wanaougua kipindupindu wanapokea matibabu katika kituo cha kujitenga katika hospitali moja mjini Khartoum, Sudan. Hali ni ya kutisha hasa katika eneo la Darfur Kaskazini, ambako zaidi ya watoto 640,000 wako hatarini.

WHO: Vifo vya kipindupindu vyaongezeka kwa mwaka wa pili mfululizo licha ya kinga na tiba kupatikana

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO hii leo limetoa takwimu mpya za kimataifa za ugonjwa wa kipindupindu kwa mwaka 2024, zikionesha ongezeko la wagonjwa na vifo. 

Idadi ya wagonjwa ilipanda kwa asilimia 5 na vifo viliongezeka kwa asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka 2023, huku zaidi ya watu 6,000 wakipoteza maisha kutokana na maradhi ambayo kwa kiasi kikubwa yanaweza kuzuilika na kutibika.

Ripoti hiyo ‘Takwimu za kipindupindu kwa mwaka 2024’ inaonesha kuwa wagonjwa waliripotiwa kutoka katika nchi 60 mwaka 2024, kutoka nchi 45 mwaka uliopita.

Afrika na Asia

Taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wa WHO imeonesha kuwa bara la Afrika, eneo la Mashariki ya Kati na Bara la Asia ndio zilibeba mzigo mkubwa zaidi, zikichangia asilimia 98 ya wagonjwa wote.

Miongoni mwa nchi zilizoathirika vibaya ni zile 12 zilizoripoti zaidi ya wagonjwa 10,000 kila moja, ikiwemo Comoro ambayo ilishuhudia mlipuko wa kwanza baada ya zaidi ya miaka 15.

Kikao cha uhamasishaji kuhusu ugonjwa wa kipindupindu kinafanyika kwa wanafunzi huko Bweremana, katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini DR Congo.
© UNICEF/Jospin Benekire Kikao cha uhamasishaji kuhusu ugonjwa wa kipindupindu kinafanyika kwa wanafunzi huko Bweremana, katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini DR Congo.

Mapungufu huduma za dharura

Kiwango cha vifo barani Afrika kiliongezeka kutoka asilimia 1.4 mwaka 2023 hadi 1.9 mwaka 2024, ishara ya mapungufu katika huduma za dharura za afya na udhaifu wa mifumo ya afya.

WHO imesema robo ya vifo hivyo vilitokea nje ya vituo vya afya, jambo linaloonesha changamoto kubwa ya upatikanaji wa tiba.

Katika kupambana na kipindupindu, WHO inasisitiza umuhimu wa kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama, huduma za usafi, chanjo na matibabu ya haraka, pamoja na ufuatiliaji madhubuti.

Chanjo ya kunywa ya Euvichol-S® iliyoidhinishwa mwaka 2024 japo imeongeza akiba na inasambazwa kimataifa, lakini mahitaji bado yanazidi usambazaji.

WHO inabainisha kuwa mwaka huu 2025 mlipuko wa kipindupindu unaendelea, ukiwa tayari umekumba nchi 31, na wameweka tathmini ya hatari ya kimataifa kuwa “ya juu sana”. Shirika hilo linaendelea kusaidia mataifa kupitia usimamizi wa wagonjwa, kuimarisha ufuatiliaji, kusambaza dawa muhimu na kuratibu kazi na wadau ili kupunguza vifo na kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huu.