Guterres atambua mchango wa mshikamano baina ya nchi zinazoendelea
Guterres atambua mchango wa mshikamano baina ya nchi zinazoendelea
Leo ni siku ya kimataifa ya ushirikiano baina ya nchi zinazoendelea zikijulikana pia kama nchi za kusini ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa tamko lenye msukumo mkubwa likitambua ustahimilivu, ubunifu, na ushawishi unaoongezeka wa nchi zinazoendelea katika kuleta maendeleo ya kimataifa.
“Katika dunia inayozidi kuwa na nguvu nyingi za ushawishi, nchi zinazoendelea zinaonesha ustahimilivu wa kipekee na ubunifu wa hali ya juu,” amesema Guterres. “Sio tu katika kukabiliana na migogoro, bali pia katika kusukuma mbele mageuzi.”
Ubunifu kwenye nchi zinazoendelea
Katibu Mkuu ameeleza jinsi nchi za Kusini mwa dunia zinavyobuni na kubadilishana majawabu bunifu katika maeneo muhimu kama vile kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, teknolojia rafiki kwa mazingira, fedha za kidijitali, na ubunifu katika sekta ya afya. Amesisitiza kuwa mafanikio haya yanajengwa juu ya misingi ya kuheshimu pande zote, kujifunza kwa pamoja, na lengo la pamoja—ambayo ndiyo misingi ya ushirikiano wa Kusini-Kusini na ule wa pembetatu.
Guterres amesisitiza kuwa ushirikiano huu si ishara tu ya mshikamano, bali pia ni nguvu kuu ya maendeleo inayohitajika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Amepongeza juhudi za nchi za Kusini katika kuendeleza Ajenda ya 2030, licha ya changamoto zinazoendelea kama vile ukosefu wa usawa wa kiuchumi na mabadiliko ya tabianchi.
Vilevile, ametoa wito kwa nchi zilizoendelea kutambua na kutekeleza wajibu wao katika kusaidia juhudi za maendeleo duniani.
Je nchi zinazoendelea zina wajibu gani?
"Tunatambua pia wajibu wa nchi zilizoendelea katika kushughulikia ukosefu wa usawa unaozidi kuongezeka na kuendeleza maendeleo endelevu,” ameongeza Guterres.
Katika hitimisho la ujumbe wake, Guterres amehimiza jumuiya ya kimataifa kukumbatia ushirikiano wa nchi za kusini kama kichocheo cha kuhuisha ushirikiano wa kimataifa, akisisitiza haja ya kuchukua hatua kwa pamoja kujenga dunia iliyo jumuishi, yenye usawa, na endelevu kwa wote.
Siku ya Kimataifa ya Ushirikiano baina ya nchi zinazoendelea au nchi za kusini ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 12 Septemba, ni kumbukumbu ya kutambua umuhimu wa mshikamano kati ya nchi zinazoendelea na nguvu ya mabadiliko inayotokana na ubunifu wa pamoja.
Maadhimisho Makao Makuu ya UN
Katika kuadhimishi siku hii tarehe 12 ,mwezi Septemba, katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuanzia saa 9 alasiari hadi saa 12 jioni kutakuwa na Mjadala wa Ngazi ya Juu: Fursa mpya na ubunifu kupitia ushirikiano wa kusini-kusini na pembetatu
Kuelekea Mkutano Mkuu wa miaka 80 ya Umoja wa Mataifa, Siku ya Umoja wa Mataifa ya Ushirikiano wa Kusini-Kusini inaadhimisha mafanikio ya ushirikiano baina ya nchi hizo zinazoendelea na ule wa pembetatu, ikijengwa juu ya maazimio ya kikao cha 22 cha Kamati ya Ngazi ya Juu.
Tukio hili linawakutanisha viongozi muhimu wakiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Baraza Kuu la UN, uongozi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP, mabalozi, na wadau mbalimbali.
Matumaini ya fursa kupitia ushirikiano wa nchi za kusini
Katika mahojiano maalum na Habari za UN, Mkurugenzi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya ushirikiano wa nchi za kusini, UNOSSC, Dima Khatib, amesisitiza kuwa nchi za Kusini zinamiliki "uwezo mkubwa wa kuendeleza maendeleo," kwani ndiko makazi ya asilimia 80 ya watu wote duniani na ni chanzo cha ustahimilivu, ubunifu, pamoja na rasilimali watu na asili ambazo hazijatumika kikamilifu.
Amesema kuwa mada iliyochaguliwa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya mwaka huu – fursa mpya na ubunifu kupitia ushirikiano wa kusini-kusini na ushirikiano wa pembetatu – ni ya wakati muafaka na inafaa sana. Ushirikiano wa Pembetatu ni ule unaohusisha nchi zinazoendelea na wadau kama vile mashirika ya kimataifa na wadau wa maendeleo ya kimataifa.
"Daima tunasema kuwa uhitaji ni mama wa uvumbuzi. Tunaamini kuwa nchi za Kusini si kwamba tu zinakumbwa na changamoto, bali pia zina majawabu na uvumbuzi, na tunapaswa kuzisaidia, kuzitia moyo, na kuonyesha mchango wao wa kipekee katika maeneo haya,” amesema.
Mwelekeo mpya wa ufadhili wa maendeleo
Nchi zinazoendelea zinakabiliana na migogoro mingi inayohusiana na kuungana, ikiwa ni pamoja na mvutano unaoongezeka wa kijiografia, mzigo wa madeni, pengo kubwa la kidijitali, na changamoto za kijamii, huku ufadhili wa kibinadamu na maendeleo kutoka kwa nchi zilizoendelea ukiendelea kupungua.
Uhalisia huu unazisukuma nchi zinazoendelea kutegemeana zaidi kwa ushirikiano wao wenyewe, jambo ambalo limekuwa “moja ya njia muhimu zaidi za kutoa ufadhili wa maendeleo,” kwa mujibu wa Bi. Al-Khatib.
"Ninaamini kuwa hili litakuwa mwelekeo unaokua zaidi kadri misaada rasmi ya maendeleo inavyozidi kupungua na nchi hizi zinapotafuta mbadala wa maana wa kufadhili maendeleo yao. Ushirikiano wa Kusini-Kusini na wa Pembetatu umeonyesha kuwa ni mbinu madhubuti sana katika muktadha huu,” ameongeza.
Afisa huyo wa UN ameeleza kuwa tafiti za karibuni zilizofanywa na ofisi yake zilionesha kuwa ushirikiano wa Kusini-Kusini “una uwezo wa kubadilisha mlinganyo wa kiuchumi, kuunda ajira, na kujenga uwezo wa ndani,” ikiwa ni pamoja na nchini Ethiopia, Paraguay, Rwanda, na nyinginezo.
Ametamatisha kwa kusema kuwa, “hakuwezi kuweko na mgawanyiok wa nchi kati ya zile za kaskazini zilizoendelea na zile za kusini zinazohaha kuendelea. Badala yake “lazima tujenge madaraja. Umoja wa Mataifa una uwezo wa kubeba jukumu hili kwa kuwa ni mfumo muhimu ambao unahudumia nchi zote kwa usawa."