Shambulio la Israel Doha Qatar laleta mshtuko, UN yataka diplomasia iheshimiwe
Rosemary DiCarlo akitoa taarifa kwenye Baraza la Usalama kuhusu shambulio la Israel Doha Qatar
Shambulio la Israel Doha Qatar laleta mshtuko, UN yataka diplomasia iheshimiwe
Amani na Usalama
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo lilipewa taarifa na afisa mkuu wa masuala ya siasa wa Umoja wa Mataifa kuhusu shambulio la anga la Israel mjini Doha Qatar na kusema ni ongezeko la kutisha la mvutano lililolaaniwa kama uvunjaji wa mamlaka ya nchi unaotishia mazungumzo yanayoendelea ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka huko Gaza.
Mkuu huyo wa masuala ya siasa Bi. Rosemary DiCarlo ameelezea shambulio la Jumanne wiki hhii katika eneo la makazi kwenye mji mkuu wa Qatar Doha ambalo lililolenga uongozi wa kisiasa wa Hamas na kuua washirika kadhaa pamoja na afisa wa usalama wa Qatar kama hatua inayoweza kufungua “sura mpya na hatari katika mzozo huu unaoharibu, na kutishia sana amani na uthabiti wa kikanda”.
Shambulio hilo lilitokea tarehe 9 Septemba katika makazi ambayo kwa taarifa yalihusisha wanachama wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, akiwemo mwana wa mkuu wa majadiliano, Khalil al-Hayya.
Ingawa viongozi wa Hamas walinusurika, Kundi hilo limesema tukio hilo limesitisha mazungumzo yanayoendelea kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachilia mateka chini ya usuluhishi wa Marekani ili kumaliza vita vya Gaza.
Mamlaka za nchi lazima ziheshimiwe
“Mamlaka na uadilifu wa ardhi ya nchi yoyote, ikiwemo Qatar ambayo ni mshirika muhimu katika kuendeleza juhudi za amani na utatuzi wa migogoro lazima ziheshimiwe,” Bi. DiCarlo amewaambia wajumbe wa Baraza.
Amezisihi pande zote kujizuia na akasisitiza haja ya kulinda njia za mazungumzo na upatanishi ili kuzuia mateso zaidi Gaza na katika ukanda huo.
Israel ilidai kuwajibika na shambulio hilo, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akilielezea kama “operesheni huru kabisa kufuatia shambulio lililoua raia mjini Jerusalem tarehe 8 Septemba, ambalo Hamas ilisema ililiendesha”.
Qatar, Baraza la Ushirikiano la Ghuba, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa nchi za Kiislamu walilaani kitendo hicho na kueleza wasiwasi juu ya ongezeko zaidi la ghasia.
Moshi ukitanda kutoka kwenye jengo mjini Doha Qatar jengo lililolengwa na shambulizi la Israel
Imani kudhoofishwa
Bi. DiCarlo amewaambia wajumbe kwamba shambulio la Israel lilikuja “katikati ya mashauriano yanayoendelea. Kitendo chochote kinachodhoofisha kazi ya upatanishi na mazungumzo kinadhoofisha imani kwa mifumo yenyewe tunayotegemea katika utatuzi wa migogoro,” amesema, akisisitiza kwamba suluhisho la kudumu Mashariki ya Kati haliwezi kupatikana kwa kuendeleza ghasia zaidi.
Ametoa wito wa kujitolea upya kwa diplomasia, akionya kwamba haja ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka haijawahi kuwa ya dharura zaidi kama ilivyo sasa.
“Naziomba pande zote zinazohusika kujizuia kabisa katika wakati huu nyeti na kujitolea tena kwa ajili ya diplomasia. Dharura ya makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka Gaza haijawahi kuwa kubwa zaidi. Fanyeni makubaliano. Waachieni mateka. Malizeni mateso ya watu wa Gaza.”
Mgogoro wa Gaza wazidi kuharibika
Wakati huohuo, hali ya kibinadamu na kiusalama Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel bado ni ya hatari.
Tangu mzozo wa Gaza ulipozuka Oktoba 2023 kufuatia mashambulio ya Hamas na makundi mengine ya kivita ya Kipalestina katika jamii za kusini mwa Israel makumi ya maelfu ya watu wamefariki dunia, wengi wakiwa raia, miundombinu na huduma za msingi zimeharibiwa vibaya, na eneo lote limesalia maghofu huku mashambulio mapya ya kuteka Jiji la Gaza yakiendelea.
Baraza la Usalama likijadili hali ya mashariki ya kati likiwemo shambulio la Israel Qatar
Taarifa kwa vyombo vya habari
Kabla ya kikao cha leo Alhamisi, Baraza la Usalama lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari likilaani mashambulio mjini Doha na kueleza masikitiko makubwa juu ya vifo vya raia.
Taarifa hiyo ilithibitisha tena kuunga mkono mamlaka na uadilifu wa ardhi ya Qatar na kutambua jukumu muhimu la nchi hiyo katika juhudi za upatanishi kumaliza vita hivi vya maafa, pamoja na Misri na Marekani.
Ilisisitiza kwamba kuachilia mateka wakiwemo waliouawa na Hamas, kusitisha mapigano, na kuhakikisha ulinzi wa raia Gaza, vinasalia kuwa vipaumbele vya juu vya Baraza.
Pia limetoa wito kwa pande zote kutumia fursa zinazopatikana za kidiplomasia kwa ajili ya amani.