Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaonya dharura ya kibinadamu kuelekea msimu wa baridi Afghanistan baada ya tetemeko la ardhi

Mwanakijiji katika jimbo la Kunar Afghanistan akikusanya kifusi kufuatia tetemeko la ardhi
© UNICEF/Amin Meerzad
Mwanakijiji katika jimbo la Kunar Afghanistan akikusanya kifusi kufuatia tetemeko la ardhi

UN yaonya dharura ya kibinadamu kuelekea msimu wa baridi Afghanistan baada ya tetemeko la ardhi

Msaada wa Kibinadamu

Kutokana na maafa yaliyosababishwa na tetemeko kubwa la ardhi katika majimbo ya Mashariki mwa Afghanistan, mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yametoa ombi la msaada la karibu dola milioni 40 kusaidia mamia ya maelfu ya watu walioathirika kwa ajili ya wakati msimu wa baridi unaokaribia.

Zaidi ya watu 2,100 wamefariki dunia kutokana na tetemeko la karibuni, 3,600 kujeruhiwa, karibu nyumba 7,000 kuharibiwa, na nusu milioni ya watu kuathirika. Hii ndiyo tathmini iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM baada ya matetemeko makubwa yaliyokumba Mashariki mwa nchi hiyo Agosti 31 na Septemba 4.
Katika mazingira haya ya uharibifu, wakazi wengi wa Kunar, Nangarhar na Laghman mikoa mitatu iliyoathirika zaidi sasa wanalazimika kuishi katika maeneo ya wazi, wakikabiliwa na baridi ya usiku wa Septemba. “Familia zimepoteza kila kitu na sasa wanalala chinikwenye maeneo ya wazi bila makazi ya kutosha, chakula au maji safi ya kunywa,” ameonya leo Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Ugochi Daniels. Ili kuwasaidia, shirika hilo la Umoja wa Mataifa linatoa ombi la dola milioni 16.8 kusaidia watu 134,000.

Ni jinamizi kwa jamii ya waathirika

Barabara zilizoporomoka na miamba iliyoziba mabonde inachelewesha misafara ya msaada. Katika wilaya za mbali, inachukua saa kadhaa kwa kutumia punda kufika vijijini. Lakini kwa mujibu wa mwakilishi wShirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Afghanistan, upweke siyo kikwazo pekee, “Miundombinu duni na mitazamo ya kijamii yenye msimamo mkali imeifanya dharura hii kuwa moja ya changamoto ngumu zaidi tulizolazimika kushughulikia,” amekiri Dkt. Tajudeen Oyewale.
Pamoja na changamoto hizo, shirika hilo la watoto la Umoja wa Mataifa limewasilisha mpango wa msaada wa dola milioni 22 kwa miezi sita ijayo. Lengo ni kuokoa watu 400,000, wengi wao wakiwa watoto. Timu zinazotembea tayari zinazunguka kwenye mabonde, zikigawa huduma za afya, maji safi ya kunywa, vifaa vya usafi na msaada wa kisaikolojia.
Vituo vya muda vya kujifunzia vinaanzishwa kuchukua nafasi ya shule zilizoharibiwa, huku msaada wa fedha ukiandaliwa kwa familia zaidi ya 13,000 ili wavuke msimu wa baridi.
Kijana akipatiwa matibabu katika jimbo la Kunar baada ya tetemeko la ardhi Afghanistan
© UNICEF/Amin Meerzad
Kijana akipatiwa matibabu katika jimbo la Kunar baada ya tetemeko la ardhi Afghanistan

Hofu ya baridi msimu unapoanza

Uharaka sasa umeongezeka. Mbali na majeraha na mshtuko, kuna tishio la baridi kali. Mikoa iliyoathirika ni makazi ya watu milioni 3.7, wakiwemo karibu 800,000 waliokimbia makazi yao kutokana na maafa haya na pia vita vya miongo miwili Afghanistan.
Wengi wao wamerejea mashariki mwa nchi hiyo baada ya miaka ya ukimbizi, ikiwemo nchini Pakistan jirani. “Msimu wa baridi unavyokaribia, hali yao itazidi kuwa mbaya bila msaada wa dharura,” ameonya Ugochi Daniels wa IOM.
Zaidi ya mahema, blanketi na majiko yanayohitajika kugawiwa ni suala la kuepusha janga la kiafya, milipuko ya kuhara i, ongezeko la utapiamlo, na kuzidi kwa msongo wa mawazo. Katika kambi za muda, msongamano pia unaongeza hatari kwa wanawake na wasichana, ambao wananyimwa faragha na upatikanaji salama wa huduma za msingi.
Watu waliopoteza makazi yao baada ya tetemeo la ardhi Afghanistan
UNOCHA/Ahmad Khalid Khaliqi
Watu waliopoteza makazi yao baada ya tetemeo la ardhi Afghanistan

Wito kwa dunia

Chini ya shinikizo, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasisitiza ujumbe mmoja, bila ufadhili wa haraka, operesheni za kibinadamu haziwezi kukabiliana na ukubwa wa maafa haya. “Tunaiomba jamii ya kimataifa kusimama na watu hawa na kutusaidia kuwalinda watoto kabla ya msimu mkali wa baridi kuanza,” amesema Dkt. Tajudeen Oyewale.
Katika milima hii iliyoharibiwa, muda unayoyoma. Kila siku inayopotea inawakaribia waathirika zaidi na msimu wa baridi kali, ambao unatishia kurefusha janga hili.