Utapiamlo kwa watoto Gaza wafikia kiwango cha kutisha huku huduma zikidorora
Utapiamlo miongoni mwa watoto katika Ukanda wa Gaza unaendelea kuongezeka kwa kasi ya kutisha, huku takwimu mpya zikionesha kiwango cha juu zaidi mwezi Agosti.
Taarifa iliyotolewa hii leo na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF imeeleza kuwa asilimia 13.5 ya watoto waliopimwa walibainika kuwa na utapiamlo mkali, ikilinganishwa na asilimia 8.3 mwezi Julai. Hali ni mbaya zaidi katika eneo la Gaza City, ambako njaa imethibitishwa, na mtoto mmoja kati ya watano ameathirika.
UNICEF imesema, watoto 12,800 waligunduliwa kuwa na utapiamlo mwezi Agosti. Hata hivyo, idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi kutokana na kupungua kwa idadi ya watoto waliopimwa, baada ya vituo 10 vya matibabu kufungwa Gaza City na Kaskazini mwa Gaza kufuatia mashambulizi na maagizo ya kuhamishwa.
Aidha, sehemu kubwa ya watoto waliolazwa wanakabiliwa na unyafuzi, hali iliyo ongezeka maradufu tangu mwanzo wa mwaka huu 2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell, amesema “Mwezi Agosti, mtoto mmoja kati ya watano Gaza City aligundulika na utapiamlo na anahitaji msaada wa dharura. Huduma za lishe lazima zilindwe ili kuokoa maisha ya watoto hawa.”
Pamoja na kuongezeka kwa usambazaji wa chakula tiba, UNICEF inasema bidhaa muhimu kwa watoto wachanga, wajawazito na kina mama wanaonyonyesha bado hazitoshi. Mashirika ya misaada yanaonya kuwa mashambulizi yanayoendelea, ukosefu wa huduma za afya, na bei kubwa za vyakula vinafanya hali kuwa mbaya zaidi.
UNICEF inatoa wito kwa pande zote kulinda raia na miundombinu muhimu, kuruhusu upatikanaji usio na vikwazo wa msaada wa kibinadamu, na kurejesha huduma za afya na lishe ili kuzuia janga kubwa zaidi la kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Wanaosaka chakula wanauwawa
Wakati njaa ikizidi kuchukua maisha ya wengi wale wanaosaka chakula kwa udi na uvumba nao wanaweka maisha yao rehani
Kupitia mtandao wa kijamii wa X Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia wakimbizi wa kipalestina UNRWA Philippe Lazzarini, amesema takriban watu 2,000 waliokata tamaa na wenye njaa wameuawa walipokuwa wakitafuta msaada wa chakula. “Wengi wao waliuawa karibu na maeneo ya kile kinachoitwa "msingi wa kibinadamu wa Gaza".
Lazzarini amesema ili kushughulikia njaa huko Gaza kunahitaji kufikisha misaada bila katazo, kwa kiwango na salama kwa watu wanaohitaji popote walipo.
Kamishna huyo amesema waachwe wafanye kazi yao kwani UN, ikiwa ni pamoja na UNRWA na wadau wengine wana rasilimali na utaalamu wa kutekeleza jukumu hilo.