UN kuzindua mradi wa kukabiliana na ugaidi Afrika Mashariki
Umoja wa Mataifa umeanzisha mradi mpya wa miaka mitatu wenye lengo la kusaidia nchi za Afrika Mashariki kukabiliana na matumizi ya kigaidi ya vilipuzi. Mradi huo unaitwao “Kusaidia Afrika Masharikiki katika kukabiliana na matumizi ya kigaidi ya vilipuzi (IEDs)” unasimamiwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kukabiliana na Ugaidi, UNOCT chini ya ufadhili wa Canada.
Kupitia mradi huo, Kenya, Somalia na Uganda zitasaidiwa kuimarisha sheria, pamoja na kujengewa uwezo wa kitaasisi ili kuzuia na kukabiliana na vitendo vya kigaidi vinavyohusisha mabomu.
Hafla ya uzinduzi wa mradi huo inalenga kuongeza uelewa kuhusu hatari na madhara ya IEDs katika ukanda wa Afrika mashariki na kuonesha mshikamano wa kikanda katika kupambana na ugaidi.
Takwimu
Kwa mujibu wa UNOCT takwimu zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2020 na 2024, matumizi ya IEDs barani Afrika yaliongezeka kwa wastani wa asilimia 12 kila mwaka, na yamekuwa silaha kuu ya makundi mengi ya kigaidi. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025 pekee, matukio yaliyohusiana na mabomu hayo yameonesha kwamba mwenendo huu utaendelea.
Afrika Mashariki ni miongoni mwa maeneo yenye matukio mengi, huku mbinu za magaidi kupata na kutumia mabomu zikibadilika kila mara.
Katika mapitio yake ya nane ya Mkakati wa Kimataifa wa Kukabiliana na Ugaidi, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitaka nchi wanachama kuhakikisha magaidi hawapati silaha na likatoa wasiwasi juu ya matumizi makubwa ya IEDs katika mashambulizi ya kigaidi duniani.