Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili wa magenge, njaa na hali ya kutokuwa na utulivu vinaendelea kuitikisa Haiti: Fletcher

Mwanamke akifua ngua katika moja ya makazi ya wakimbizi wa ndani mjini Port-au-Prince, Haiti.
© UNOCHA/Matteo Minasi Mwanamke akifua ngua katika moja ya makazi ya wakimbizi wa ndani mjini Port-au-Prince, Haiti.

Ukatili wa magenge, njaa na hali ya kutokuwa na utulivu vinaendelea kuitikisa Haiti: Fletcher

Amani na Usalama

Hali nchini Haiti inaendelea kuzorota, sehemu kubwa ya nchi inadhibitiwa na magenge yenye silaha, nusu ya idadi ya watu wanakabiliwa na upungufu wa chakula, na idadi ya watu waliofurushwa kutoka kwenye makazi makazi yao imefikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa kikiongezeka mara tatu ndani ya mwaka mmoja uliopita na kufikia zaidi ya watu milioni moja amesema mratibu wa misaada na masuala ya dharura wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher.

Akiwa ziarani nchini Haiti Fletcher, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada kwa watu wa Haiti ili kuwanusuru na changamoto hizo..
"Ninajisikia aibu kwa niaba ya dunia nzima, kwamba hatuwezi kuonesha huruma zaidi, wema zaidi, kwamba hatutaki kukubali kile watu hawa wanachokipitia," amesema Fletcher akiongeza kuwa
"Nimesikiliza simulizi za watu waliovurugiwa maisha yao na ukatili. Wanahitaji kwa haraka kurejeshewa hali ya usalama, heshima na matumaini. Nakataa kuamini kuwa hatuwezi kufanya zaidi kwa ajili yao".

Magenge ya uhalifu yanaendelea kushika hatamu

Zaidi ya mwaka mmoja sasa, magenge ya uhalifu yenye silaha yamehodhi sehemu kubwa ya mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince na maeneo jirani. Yanahusika katika mauaji, ubakaji, uporaji wa shule na hospitali, na hata kuwateka watoto ili washiriki katika mapigano amesema Fletcher.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dhrarua OCHA, leo hii hadi nusu ya wanachama wa magenge hayo ya uhalifu ni watoto.
Fletcher binafsi amesema amekutana na familia zilizopitia ukatili na kulazimika kuishi kwenye makambi ya muda.
"Wanataka kuishi kama kila mtu mwingine anavyoishi. Hawataki kuwa hapa. Wanataka kujenga upya maisha yao, wanataka watoto wao wapate elimu, huduma za afya na maji safi," alisema.
Watu wakikimbia machafuko katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince
© UNFPA Watu wakikimbia machafuko katika mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince

Nilipoteza kila kitu nimebaki mtupu-Muathirika

Kashmina Jean-Michel alipoteza saluni yake ya urembo baada ya kushambuliwa na genge la wahalifu.Anakumbuka iilivyotokea "Saa kumi na moja alfajiri milio ya risasi ilianza. Nilipoteza kila kitu, mali na biashara. Lakini muhimu zaidi kwangu ilikuwa kuwaokoa watoto. Sikuwa na chaguo jingine ila kukimbia mara moja," anasema.
Ameongeza kuwa "Leo ninaishi kwenye chumba kidogo kwa umaskini mkubwa. Ni mtoto mmoja tu anayeweza kuwa nami, wengine wanalazimika kuishi kwa marafiki".
Kwa mujibu wa Fletcher, familia nyingi alizozungumza nazo tayari zimeshalazimika kuhama mara mbili au tatu.
Msimamizi wa moja ya makambi ya watu waliokoseshwa makazi, Innocent Fangeot, ameeleza changamoto zilizopo kuwa ni pamoja na "Eneo hili halikuandaliwa kwa watu wengi kiasi hiki. Kuna tatizo la chakula, chakula kinatosha kula mchana pekee, lakini watu wafanye nini saa tisa au kumi jioni? Hata wao pia wanahitaji kula."
Mratibu Mkuu wa Misaada wa Un Tom Fletcher akikutana na baadhi ya familia za waathirika Haaiti
UNOCHA/Marvens Compere Mratibu Mkuu wa Misaada wa Un Tom Fletcher akikutana na baadhi ya familia za waathirika Haaiti

Elimu kwa vijana

Fletcher amesema pamoja na hali ngumu, kuna mashirika nchini Haiti yanayoendelea kusaidia wananchi. Kituo cha Vijana cha OCCED’H mjini Port-au-Prince kinafanya kazi na vijana kutoka maeneo yaliyoathirika ambapo upatikanaji wa elimu na mafunzo ni mdogo mno.
Karibu wanafunzi 300 hupata ujuzi wa vitendo katika kituo hicho. Mmoja wao, ni Fani Sagesse, anajifunza kutengeneza bidhaa za ngozi anasema "Ninapenda kukuza ubunifu wangu, na ukiuchukulia kwa umakini, ukaweka moyo na bidii, unaweza kukusaidia kuwa huru kiuchumi".
Muathirika wa ukatili wa kijinsia na kingono mjini Port-au-Prince, Haiti alibakwa na magenge ya uhalifu
© UNFPA/Wendy Desert Muathirika wa ukatili wa kijinsia na kingono mjini Port-au-Prince, Haiti alibakwa na magenge ya uhalifu

Lazima tufanye juhudi zaidi kuisaidia Haiti

Alipotembelea kituo hicho, Fletcher amesema: "Tunaweza kupata njia za kukabiliana na mgogoro, hali ya kukata tamaa na kuporomoka kwa maisha, hapa Vijana wanajifunza kunyoa nywelekutengeneza kucha, kutengeneza mikufu, kukarabati pikipiki na mengine. Lakini muhimu zaidi ni kwamba wanajenga upya maisha yao."
Almeisitiza kuwa dunia lazima inyooshe mkono wa msaada kwa Haiti na akatoa wito wa kuongezwa kwa ufadhili wa operesheni za kibinadamu nchini humo. Kati ya dola milioni 908 zinazohitajika ili kukidhi mahitaji ya dharura zaidi, ni milioni 108 pekee zilizopatikana.
"Siwezi kuamini kwamba ni vigumu kiasi hiki kwetu kukusanya fedha. Lazima tufanye juhudi zaidi," amesema Fletcher.