Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa mlo shuleni wanufaisha watoto wengine milioni 80 duniani kote – WFP

Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Limuru X Bibirioni nchini Kenya wakiwa wameshikilia kamba za mikononi zenye rangi ya chungwa.
UN News/Thelma Mwadzaya Wanafunzi wa shule ya msingi ya Bibirioni Limuru nchini Kenya wakionyesha mikanda ya mkononi inayotumika kulipia chakula .

Mradi wa mlo shuleni wanufaisha watoto wengine milioni 80 duniani kote – WFP

Malengo ya Maendeleo Endelevu

​Watoto wengine zaidi wapatao milioni 80 duniani kote sasa wanapata mlo wa shuleni kupitia programu zinazoongozwa na serikali, ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 tangu mwaka 2020, imesema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP iliyotolewa leo Roma, Italia. Kenya, Rwanda zinazongoza kwenye programu hizi.

Taarifa ya WFP inasema ongezeko hilo linafanya idadi kamili ya watoto wanaonufaika na program hiyo kufikia milioni 466.

Ripoti hiyo inanukuu toleo la hivi karibuni la ripoti ya "Hali ya upatiaji watoto mlo shuleni duniani kote, ambayo hutolewa na WFP kila baada ya miaka miwili.

Maendeleo makubwa katika nchi zenye kipato cha chini

​Maendeleo makubwa yanaonekana kutokea mahali panapohitajika zaidi, ambapo nchi zenye kipato cha chini zimeongeza idadi ya watoto wanaopatiwa milo ya shuleni kwa asilimia 60 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Afrika inaongoza katika ongezeko hili, na idadi ya watoto milioni 20 wa kiafrika sasa wanalishwa kupitia programu za kitaifa za milo ya shuleni – huku nchi kadhaa kama Kenya, Madagascar, Ethiopia, na Rwanda zikionesha maendeleo makubwa.

​Mafanikio haya adimu katika sekta ya maendeleo yanaongozwa na serikali kote ulimwenguni. Ripoti inaonesha ushahidi thabiti kwamba programu za milo ya shuleni si tu zinasaidia ustawi wa watoto, bali pia zina faida pana kwa wakulima wadogo na ajira za ndani. Vilevile, zinahimiza lishe rafiki duniani na kupunguza uzalishaji wa kaboni.

​Kauli ya Mkurugenzi Mtendaji wa WFP

​Akizungumza kuhusu ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Cindy McCain, amesema, "Mlo shuleni ni zaidi ya sahani ya chakula chenye lishe – ingawa hiyo ni muhimu. Kwa watoto walio hatarini wanaopokea milo hii, ni njia ya kutoka katika umaskini na kuingia katika ulimwengu mpya wa kujifunza na fursa."

​Amesema serikali kote ulimwenguni, hasa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, zinaonesha uongozi halisi kwa kuchagua kipaumbele programu za milo ya shuleni. Programu ziimeonekana kuwa moja ya uwekezaji wenye busara na gharama nafuu zaidi ambao taifa linaweza kufanya ili kuboresha afya ya muda mrefu, elimu, na ustawi wa kiuchumi wa vizazi vijavyo.

“WFP inashukuru kwa ushirikiano wa mabadiliko uliojengwa kupitia Muungano wa Milo ya Shuleni na tunahimiza serikali zaidi kujiunga na harakati hii ya kimataifa," ameongeza Bi. McCain.

Amina Mohammed na mwanamke mwingine wamesimama wakitabasamu katika kituo cha kusambaza chakula, wakiwa wameshika mboga mbichi.
© UNEP/Ahmed Nayim Yussuf Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed atembelea Jiko la Food4Education Giga jijini Nairobi, Kenya.

Uwekezaji mara mbili katika miaka minne

​Ripoti hiyo imebainisha kuwa ufadhili wa kimataifa kwa mlo shuleni umeongezeka zaidi ya mara mbili, kutoka dola bilioni 43 mwaka 2020 hadi dola bilioni 84 mwaka 2024. Asilimia 99 ya ufadhili huu sasa inatoka katika bajeti za kitaifa. 

Hii inaashiria mabadiliko makubwa ambapo milo ya shuleni haionekani tena kama programu ya misaada ya kigeni, bali kama sera yenye nguvu ya umma inayoweza kuendesha maendeleo ya kitaifa. Hata hivyo, ufadhili wa ndani ni mdogo katika nchi zenye kipato cha chini, ambapo rasilimali bado ni chache na mahitaji ni makubwa zaidi.

​Ukuaji wa programu za milo ya shuleni ni wa haraka zaidi katika nchi zilizo wanachama wa Mtandao wa Programu za mlo Shuleni, ambao ni mtandao wa kimataifa unaoongozwa na serikali zaidi ya 100, mashirika sita ya kikanda, na kuendeshwa na WFP kama sekretarieti yake.

Mtandao huu unaungwa mkono na washirika zaidi ya 140 kutoka sekta mbalimbali. Watoto 2 kati ya 3 wapya walionufaika na mlo shuleni wanatoka katika nchi wanachama wa Muungano huo.

Ripoti hiyo imeeleza jinsi Muungano unavyosherehekewa kama mfumo wa ushirikiano wa kisasa – na kupitia juhudi zake, idadi ya nchi zenye sera za kitaifa za milo ya shuleni imeongezeka karibu mara mbili tangu mwaka 2020, kutoka 56 hadi 107.

​"Serikali zinaonesha uongozi halisi kupitia Muungano wa Milo ya Shuleni, unaoongozwa na Brazil,Finland, na Ufaransa, na kuendeshwa na WFP, wanapowekeza katika watoto na jamii zao," amesema Carmen Burbano, Mkurugenzi wa Programu ya Mlo Shuleni na Ulinzi wa Jamii wa WFP na Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Mtandao wa Mlo Shuleni, inayoendeshwa na WFP,

Burbano ameongeza ​"ongezeko la programu za mlo shuleni zinazofadhiliwa kitaifa ni ishara yenye nguvu ya kile kinachowezekana, hata katika nyakati ngumu. Lakini katika nchi zenye kipato cha chini, ambapo mahitaji ni makubwa zaidi, maendeleo bado yako hatarini kwani misaada ya kimataifa inabadilika na rasilimali za ndani hazitoshi."

​Ripoti hii imetolewa wiki moja kabla ya mkutano wa pili wa kimataifa wa MTandao wa Programu ya Mlo Shuleni nchini Brazil, utakaoanza tarehe 18-19 mwezi Septemba, ambapo viongozi watakutana kutathmini maendeleo na kuhamasisha hatua zaidi.

​Programu inaweza kukabiliana na 'changamoto katika kujifunza'

​Ushahidi mpya unaoibuka, uliochapishwa kwa mara ya kwanza katika ripoti ya Hali ya Ulishaji Shuleni Duniani Kote, unaonesha jinsi milo ya shuleni inavyoweza kuchangia katika kukabiliana na 'changamoto katika kujifunza' za hivi karibuni, kwa kuongeza uwezo wa kujifunza na stadi za utambuzi, na kupata mafanikio katika hisabati na kusoma na kuandika.

Maendeleo kwa watu na dunia nzima

​Zaidi ya elimu, ripoti ya hali ya mgao wa mlo shuleni duniani kote pia imeangazia athari pana za sekta mbalimbali zinazohusiana na programu za milo ya shuleni:

● ​Programu za mlo shuleni ni mtandao mkubwa zaidi wa usalama wa jamii duniani, zinazosaidia nchi kukabiliana na mishtuko – kutoka mabadiliko ya hali ya hewa hadi magonjwa ya janga hadi vita – na kuwafikia watoto walio hatarini zaidi.

​● Programu za mlo shuleni zina gharama nafuu na ni uwekezaji wenye athari kubwa kwa sababu zinaleta faida katika sekta mbalimbali (elimu, afya, ulinzi wa jamii, na kilimo): Kwa kila Dola 1 inayowekezwa, zinaleta kati ya Dola 7 na Dola 35 katika faida za kiuchumi.

● ​Mlo shuleni pia unaweza kuwa injini yenye nguvu ya kuunda ajira za ndani. Kutoa milo ya shuleni kwa idadi ya watoto milioni 466 kunazalisha ajira milioni 7.4 za wapishi duniani kote, na ajira zaidi katika usafirishaji, kilimo, na minyororo ya usambazaji, ikisababisha uundaji wa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

● Mifumo endelevu ya mlo shuleni, kama vile programu za mlo shuleni inayotokana na mazao ya nyumbani, inaweza kukuza lishe bora, rafiki kwa mazingira, na kutumika kama vichocheo vya kuunda mifumo ya chakula iliyo na mizizi ya ndani inayokuza uchumi wa ndani na kitaifa.

​● Wasichana wananufaika zaidi kuliko wavulana na mlo shuleni kwa upande wa matokeo ya elimu na afya. Pamoja na faida sawa zinazoonekana kwa wanawake pia, kwani programu hizi zinawezesha wanawake kiuchumi kwa kupanua majukumu yao katika minyororo ya usambazaji wa chakula na ajira za kijamii, kwa mfano kama wapishi shuleni.