Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Operesheni za ulinzi wa amani za UN ziko njiapanda Baraza la Usalama lajidili hatma

Wajumbe wakihudhuria mkutano wa Baraza la Usalama UN katika Ukumbi wa Baraza katika makao makuu ya UN jijini New York.
UN Photo/Loey Felipe Baraza la Usalama likijadili hatma ya operesheni za ulinzi wa amani za UN

Operesheni za ulinzi wa amani za UN ziko njiapanda Baraza la Usalama lajidili hatma

Amani na Usalama

Operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa ni chombo muhimu cha juhudi za kimataifa za kudumisha amani. Zinauwezesha Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kwa ufanisi kukabiliana na vitisho vikubwa dhidi ya amani na usalama.

Mwaka 2024, kulikuwa na migogoro 61 duniani, na zaidi ya walinda amani 60,000 kutoka nchi wanachama 115 wakifanya kazi muhimu katika misheni 11 Mkuu wa Operesheni za Kulinda Amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix ameliambia Baraza la Usalama.

“Akiwa na zaidi ya walinda amani 60,000 kutoka nchi wanachama 115 wakifanya kazi muhimu kwa ujasiri katika misheni 11, ulinzi wa amani ndiyo shughuli kubwa zaidi na inayoonekana zaidi ya Umoja wa Mataifa katika maeneo yenye mizozo,” amesema.

Msafara wa kijeshi wa magari ya UNIFIL na Jeshi la Lebanon ukishika doria barabarani Kusini mwa Lebanon.
© UNIFIL Walinda amani wa UNIF nchini Lebanoni kwakiwa katika doria

Operesheni zinahudumu katika mazingira magumu

Leo Rosemary DiCarlo ambaye ni mkuu wa  masuala ya kisiasa katika Umoja wa Mataifa kwa upande wake alisisitiza mbele ya Baraza la Usalama kwamba operesheni hizo zinafanya kazi katika mazingira ya kugawanyika kijiografia na kisiasa.

Ameongeza kuwa “Migogoro inazidi kuingiliwa kimataifa, ikihusisha wahusika wa kikanda na kimataifa, huku idadi ya makundi yenye silaha ikiongezeka. Wengi wao hutumia mbinu za kigaidi na kuharibu mbinu za jadi za ulinzi wa amani”.

Kwa mujibu wake, teknolojia mpya kuanzia akili akili Mnemba AI hadi ndege zisizo na rubani au droni zinatumika zaidi kama silaha. Hii inaongeza uwezo wa uharibifu wa vurugu na hatari ya kuchochea mapigano.

Sababu nyingine amesema ni uhalifu wa kimataifa, ambao umekuwa sehemu ya kudumu ya migogoro ya kisasa.

“Mitindo hii inafanya ulinzi wa amani na utatuzi wa migogoro kuwa mgumu zaidi leo. Nchi wanachama, hasa katika Baraza la Usalama na nchi wenyeji, hawakubaliani kuhusu jinsi na madhumuni ya kutuma operesheni za kulinda amani, pamoja na masharti ya kufanikisha. Hii ndiyo sababu kuangalia upya mustakabali wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa ni jambo la dharura,” amesema Bi. DiCarlo.

Walinda amani wa MONUSCO kutoka vikosi vya Nepal na Bangladesh wakimbeba raia aliyejeruhiwa kwenye machela wakati wa uokoaji wa kimatibabu huko Gina, Ituri, DR Congo.
© MONUSCO Walinda amani wa MONUSCO wakiwahamisha raia wanne waliojeruhiwa vibaya hadi hospitali ya Bunia baada ya shambulio la silaha.

Historia na mafanikio

Akiangazia historia, amekumbusha kwamba Umoja wa Mataifa umewahi kusaidia kumaliza vita na kusaidia mabadiliko ya kisiasa.

Nchini Nepal, kwa mfano, amesema kati ya mwaka 2007 na 2011, mpango wa Umoja wa Mataifa ulisaidia kubadilisha makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya serikali na Chama cha Kikomunisti cha Nepal kuwa amani ya kudumu.

DiCarlo pia ametaja uzoefu wa safari ya diplomasia wakati wa Vita Baridi. Mwakilishi wa Katibu Mkuu kwa Afghanistan wakati huo alifanya mazungumzo Moscow, Washington, Islamabad na Kabul, ambayo yalipelekea kutiwa saini kwa Mkataba wa Geneva wa 1988 na kumaliza uwepo wa Kisovyeti nchini Afghanistan.

Baada ya kupitia historia ya ulinzi wa amani, Umoja wa Mataifa umetambua sifa kadhaa za operesheni iliyofanikiwa. Misheni hiyo ilikuwa na mamlaka wazi yenye muda maalumu, ilikuwa nafuu na yenye uhamaji.

Majukumu yao yalikuwa mafupi na bayana, yakitoa uwazi na kubadilika. Pia yalitumia sana rasilimali za makao makuu yaliyopo na uwezo wa Katibu Mkuu katika upatanishi.

Walinda amani wawili UNMISS wa Bangladesh waliovalia kofia za bluu wakipeana mikono na mwanamume wa eneo hilo mbele ya kundi la watoto huko Tonj, Sudan Kusini.
© UNMISS Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, (UNMISS) ulianzishwa na kupatiwa majukumu yake na Baraza la Usalama la UN.

Vipaumbele vya Sasa

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani Jean Pierre-Lacroix ametaja vipaumbele vya sasa katika ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa kuwa ni

  1. Majukumu ya awali ya operesheni za ulinzi wa amani yanapaswa kupunguzwa katika hali zisizo na makubaliano ya amani ya kina.
  2. Uratibu na timu za Umoja wa Mataifa katika nchi husika unapaswa kuimarishwa, ukiunganisha vipengele vya kisiasa, kibinadamu na haki za binadamu.
  3. Na mamlaka ya operesheni yanapaswa kuzingatia utofauti wa hali na kuepuka mbinu za aina moja kwa wote.

    Luteni Kanali Josefina Patlan Rodarte wa Kikosi cha Wanajeshi cha Mexico akiwasiliana kupitia redio akiwa ndani ya gari wakati wa misheni ya MINURSO katika jangwa la Sahara Magharibi.
    MINURSO/Josefina Patlan Luten Kanali Josefina Patlan Rodarte mlinda amani wa mpango wa Umoja wa Mataifa wa MINURSO Sahara Magharibi

Msaada wa kisiasa ni muhimu
Lacroix amemalizia kwa kusema kuwa kuna upungufu wa msaada wa kisiasa kwa operesheni za kulinda amani.

Amesisitiza kuwa ili kuendeleza suluhu za kisiasa za muda mrefu na kuondoa vikosi vya kulinda amani bila kurejea kwenye mapigano, msaada wa Baraza la Usalama ni muhimu.