Annalena Baerbock raia wa Ujerumani ameapa rasmi kuanza Urais wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Alichaguliwa mwezi Juni mwaka huu 2025 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa baada ya kupendekezwa na kundi la nchi za Ulaya Magharibi na nchi nyinginezo ambazo ndio zamu yao mwaka huu kushika Urais wa Baraza Kuu. Alipata kura 167 kati ya nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Annalena Baerbock anakuwa mwanamke wa tano pekee katika miaka 80 ya Umoja wa Mataifa kushika wadhifa huu wa Rais wa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mkutano na waandishi wa habari
Akizungumza na waandishi wa habari nje tu ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mara baada ya kula kiapo kwa kutumia Katiba asili ya Umoja wa Mataifa, Baerbock amesema urais wake utalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika wakati ambapo chombo hicho cha dunia kinakabiliwa na migawanyiko ya kisiasa na changamoto za kifedha.
“Kuapishwa kwa kutumia Katiba ya asili ya Umoja wa Mataifa kunatukumbusha kile ambacho dunia inaweza kufanikisha kwa pamoja. Lakini tukitazama Gaza, Ukraine, Sudan na Haiti, kunatukumbusha pia ni mara ngapi tumeshindwa kutekeleza ahadi zake,” amewaambia waandishi wa habari.
Baerbock ameeleza Mkutano wa 80 kama “Mkutano usio wa kawaida,” akisisitiza kwamba Umoja wa Mataifa lazima uoneshe kwa “watu bilioni 8 kwa nini taasisi hii bado ina umuhimu.” Ameahidi kuwa “mtetezi asiyeegemea upande wowote lakini mwenye shauku” wa taasisi hiyo, akiongozwa na Katiba na kauli mbiu: “Tutakuwa Bora Tukishikamana.”
Kuhusu shambulizi la leo la Israel kwa Qaatar
Mkutano wa kwanza wa Baerbock na waandishi wa habari wa umeguka kwa haraka na kuangazia matukio ya dharua Mashariki ya Kati, baada ya ripoti kuibuka kwamba Israel imefanya mashambulizi ya anga katika eneo la Qatar mapema leo na hivyo waandishi wakataka maoni yake.
“Kuongezeka kwa hali ya leo kunatia wasiwasi, na ninatoa wito kwa pande zote kujizuia kadri inavyowezekana,” amesema, akionya kwamba uhuru na mipaka ya kijiografia ya wanachama wa Umoja wa Mataifa lazima viheshimiwe.
Amesisitiza haja ya “kuimarisha juhudi za kidiplomasia kuelekea usitishaji mapigano wa haraka na wa kudumu, kuboresha hali ya kibinadamu kwa raia wa Gaza, na kuachiliwa kwa mateka wote wanaoshikiliwa na Hamas.”
Kuhusu ushiriki wa Palestina katika UNGA
Alipoulizwa iwapo Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ataweza kuhutubia Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video wiki ijayo, Baerbock amesisitiza jukumu la Umoja wa Mataifa kama jukwaa shirikishi.
“Taasisi hii, ambayo tunapaswa kuisherehekea kwa kumbukumbu ya miaka 80, ilianzishwa kama mahali ambapo mataifa yote ya dunia yanaweza kukutana na kushirikiana,” amesema. Amebainisha kwamba kwa mujibu wa Makubaliano ya Makao Makuu, nchi mwenyeji inapaswa kutoa ruhusa kwa ujumbe wote “kama ilivyo desturi ya miaka themanini iliyopita.”
Kuhusu mipango yake SOMA ZAIDI HAPA