Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio la Urusi laangamiza zaidi ya watu 20 wakiwa kwenye foleni ya mafao ya uzeeni Donetsk, UN yalaani

Lori la zimamoto limeegeshwa mbele ya jengo la ghorofa lililoharibika vibaya huku moshi ukitoka kwenye ghorofa za juu na vifusi vikianguka chini.
© Humanitarian Mission Proliska Jengo likiteketea katika ji mmbo la DonetskUkraine baada ya kupigwa kombora na Urusi

Shambulio la Urusi laangamiza zaidi ya watu 20 wakiwa kwenye foleni ya mafao ya uzeeni Donetsk, UN yalaani

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio la Urusi lililotokea lililofanyika leo katika kijiji cha Yarova, mkoa wa Donetsk, ambalo limeua zaidi ya watu 20 na kuwajeruhi karibu wengine 20.

Kwa mujibu wa duru za habari waathirika wengi walikuwa ni wazee waliokuwa wamekusanyika ili kuchukua malipo yao ya uzeeni wakati shambulio lilipotokea. “Tumepokea picha za kutisha za shambulio la Urusi asubuhi ya leo. Wengi wa walioathirika ni wazee waliokuwa wakichukua mafao yao ya uzeeni ” amesema Matthias Schmale, Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine.

Licha ya kuongezeka kwa mapigano, wazee wengi wameendelea kubaki kwenye vijiji vya vilivyo mstari wa mbele wa mapigano, ama kwa kutoweza kuondoka au kwa kuwa hawawezi kuacha nyumba zao.

Shambulio hilo la hivi karibuni linaonesha namna raia walio hatarini zaidi wanavyoendelea kubeba mzigo mkubwa wa vita.

Mashambulizi yanazidi kusambaratisha raia

“Ukatili huu unaendelea kusambaratisha maisha ya watu,” Schmale ameonya, akibainisha kuwa katika siku za hivi karibuni mkoa wa Donetsk umeshuhudia ongezeko kubwa la vifo na majeruhi miongoni mwa raia pamoja na uharibifu wa mali.

Kwa niaba ya Umoja wa Mataifa na washirika wa kibinadamu, Schmale ametoa pole kwa familia za waathirika na kuonesha mshikamano na wote waliojeruhiwa, akisisitiza, “Mashambulizi yanayowaathiri raia wakiwa katika shughuli zao za kila siku hayawezi kukubalika. Vita vina sheria zake. Msivue utu au kujeruhi raia. Msiharibu nyumba, shule na miundombinu mingine ya kiraia.”

Kwa mujibu wa Schmale shambulio hilo la Yarova linaongeza wasiwasi mkubwa wa kimataifa kuhusu kuongezeka kwa mapigano mashariki mwa Ukraine, ambako raia wanaendelea kubeba gharama kubwa ya mzozo huu.

Raia wanalipa gharama kubwa ya vita Ukraine: IOM

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limeungana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA na mratibu wa Umoja wa Mataifa Ukraine kulaani shambulio hilo la kikatili Donetsk Ukraine.

IOM imesema Idadi kubwa ya raia nchini Ukraine inaendelea kubeba mzigo mzito wa vita, huku mashambulizi ya Urusi yakipiga miji na vijiji vilivyoko mstari wa mbele wa mapigano na hata maeneo mengine.

Mwezi Julai 2025 pekee, limesema  vifo 286 na majeruhi 1,388 vilirekodiwa na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu OHCHR, ikiwa ndiyo idadi kubwa zaidi ya kila mwezi tangu Mei 2022.

Ufurushwaji wa watu umeendelea kuwa sifa kuu ya mzozo huu. Kwa mujibu wa takwimu za IOM, takribani watu milioni 5.7 bado wamehamishwa kimataifa, huku watu milioni 3.8 wakiwa wamehamishwa ndani ya Ukraine, na watu milioni 4.1 wakirudi aidha kutoka uhamisho wa ndani au kutoka ughaibuni.