Dunia inatumia matrilioni ya dola kuchochea vita badala ya kudumisha amani, UN yaonya
Dunia inatumia matrilioni ya dola kuchochea vita badala ya kudumisha amani, UN yaonya
Bajeti zamatumizi ya kijeshi duniani zimepanda hadi kufikia dola trilioni 2.7 mwaka 2024, zikigeuza mwelekeo wa rasilimali kutoka kwenye masuala ya maendeleo zikiwa zimeongezeka kwa zaidi ya asilimia tisa kutoka mwaka 2023, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inayoonya kuwa mwelekeo huu unadhoofisha amani na maendeleo endelevu.
Ripoti hiyo iliyotolewa leo mjini New York Marekani imesisitiza kuwa endapo matumizi hayo hayatazuiliwa, yanaweza kufikia dola trilioni 6.6 ifikapo mwaka 2035.
“Ushahidi uko wazi, matumizi ya kijeshi kupita kiasi hayaleti amani,” amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wakati wa kuzindua ripoti hiyo iliyopewa jina “Usalama Tunaohitaji: Kurekebisha Matumizi ya Kijeshi kwa Mustakabali Endelevu na wa Amani”.
Guterres ameongeza kuwa “Mara nyingi matumizi haya hutia doa amani yakichochea mashindano ya silaha, kuongeza hali ya kutoaminiana na kuondoa rasilimali kutoka kwenye misingi halisi ya uthabiti.”
Gharama na hatari zinazoongezeka
Ripoti hiyo inaonesha kitendawili hatari, wakati mataifa yanamwaga rasilimali nyingi katika ulinzi, dunia iko mbali katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo 2030.
Pengo la kila mwaka la ufadhili wa SDGs ni dola trilioni 4 na linaweza kupanuka hadi trilioni 6.4. imesema ripoti hiyo.
“Kipaumbele cha dunia kimepotoshwa,” ripoti inaonya, ikibainisha kuwa tangu mwaka 2022 matumizi ya kijeshi yameongezeka kutoka asilimia 2.2 hadi 2.5 ya Pato la Taifa la Ulimwengu (GDP), na sasa yanatumia zaidi ya asilimia 7 ya bajeti za serikali kote duniani. Zaidi ya nchi 100 ziliongeza matumizi ya ulinzi mwaka 2024 pekee.
Maendeleo yanabaki nyuma
Wakati huo huo, misaada rasmi ya maendeleo inapungua. Ripoti inaonesha kuwa ongezeko la asilimia moja la bajeti za ulinzi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati linaendana karibu sawa na upungufu wa asilimia moja katika huduma za afya za umma ni hatari kwa maandalizi ya magonjwa ya milipuko na programu za uhai.
“Tunahitaji mtazamo mpya wa usalama unaomlenga binadamu na unaojengwa juu ya Katiba ya Umoja waMataifa,” amesema Izumi Nakamitsu, Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Mata9ifa wa Masuala ya Udhibiti wa Silaha.
Ameongeza kuwa “Mtazamo unaolinda watu siyo mipaka pekee, unaoweka mbele taasisi, usawa na uendelevu wa sayari. Kurekebisha vipaumbele vya dunia si chaguo ni sharti la kuendelea kuishi kwa binadamu.”
Dunia iko katika hatua nyeti
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza kuwa mwenendo wa sasa unatokea wakati ambapo hofu za kiusalama zinaongezeka, ukosefu wa usawa unazidi, na hatari mpya za kimataifa zinajitokeza.
Mwelekeo huu, wanasema, unazifunga nchi kwenye madeni ya kudumu huku ukinyima uwekezaji katika maeneo yanayoweza kuzuia migogoro.
“Tupo katika dunia yenye mpasuko unaoongezeka, misaada ya maendeleo rasmi ikipungua, na maendeleo ya binadamu yakisuasua,” amesema Haoliang Xu, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika laUmoa wa Mataifa la mpango wa Maendeleo UNDP.
“Lakini tunajua kuwa maendeleo ni kichocheo cha usalama. Watu wanapoboreshewa maisha yao, wakipata elimu, afya, fursa za kiuchumi na kuishi kwa heshima, jamii zitakuwa na amani zaidi na dunia pia itakuwa yenye amani zaidi.” ameongeza
Gharama za vipaumbele visivyowekwa sawa
Ripoti inaonyesha kuwa hata mgao mdogo tu wa matumizi ya kijeshi unaweza kubadilisha mustakabali wa dunia.
Chini ya asilimia nne ya matumizi ya kila mwaka takriban dola bilioni 93 ingetosha kumaliza njaa ifikapo mwaka 2030. Zaidi kidogo ya asilimia 10, au dola bilioni 285, zingetosha kuwachanja watoto wote duniani. Kwa dola trilioni 5, kila mtoto katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati angepata elimu bora kwa miaka 12. Imeainisha ripoti hiyo
Wakati huo huo, matumizi ya kijeshi hayazalishi ajira nyingi kulinganisha na sekta za kiraia. Imesema ripoti kwani kila dola bilioni 1 inayotumika kijeshi huunda ajira 11,200, ikilinganishwa na ajira 26,700 katika elimu, 16,800 katika nishati safi na 17,200 katika huduma za afya.
Changamoto za tabianchi na amani
Ripoti pia inaangazia athari za mazingira za matumizi ya kijeshi. Kila dola inayotumika kwenye jeshi huzalisha zaidi ya mara mbili ya gesi chafuzi ikilinganishwa na dola inayowekezwa kwenye sekta za kiraia.
Pia imesema kuelekeza upya asilimia 15 pekee ya matumizi ya kijeshi duniani takriban dola bilioni 387 kungeweza kugharamia kikamilifu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika nchi zinazoendelea kila mwaka.
“Hii siyo kuhusu uchumi pekee,” amesema Guterres. “Ni kuhusu kuendelea kuishi. Mustakabali wa binadamu unategemea kuwekeza katika amani, watu na sayari si katika silaha zaidi.”
Msingi katika Katiba ya UN
Ripoti inahitimisha kwa kuwakumbusha mataifa kwamba Katiba ya Umoja wa Mataifa yenyewe inataka “kuepusha matumizi makubwa ya rasilimali za binadamu na kiuchumi kwa silaha.”
Inasisitiza kuwa kugeuza mwenendo wa matumizi ya kijeshi yaliyovunja rekodi si suala la hiari tu, bali ni wajibu wa msingi chini ya sheria za kimataifa.
“Wakati umefika wa kuoanisha maneno na vitendo,” amehimiza Katibu Mkuu. “Lazima turekebishe matumizi ya dunia ili kuhakikisha mustakabali endelevu na wenye amani kwa wote.”