Usiku Milima Ilipotikisika: Daktari katika mapambano baada ya tetemeko la ardhi Afghanistan
Mshtuko wa kwanza ulimtoa Dkt. Abdul Mateen Sahak kitandani, wa pili ulimpeleka kwenye simu yake ilikuwa ni kabla tu ya saa sita usiku, Jumapili ya tarehe 02 Septemba 2025 milima ya mashariki mwa Afghanistan ilikuwa imepigwa na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.0 katika kipimo cha richa, lililofuatwa mara moja na mitikisiko midogo ya baada ya tetemeko.
Katika nyumba yake huko Jalalabad, takriban kilomita 50 kutoka kiini cha tetemeko, Dkt. Sahak na mkewe walikimbia kutoka chumbani mwao na kuwakuta watoto wao wanane tayari wako kwenye korido
Mara moja nilifikiria kuhusu Herat,” alisema daktari huyo wa Kiafghan aliye na umri wa kati ya miaka ya 40 na 50, akirejelea matetemeko ya ardhi yaliyoharibu kabisa mkoa wa magharibi wa nchi hiyo mwaka wa 2023. “Nilijua kuwa madhara yangekuwa makubwa vilevile.”
Akiwa mzaliwa wa eneo la Jalalabad, alielewa vyema athari ambazo janga hili lingekuwa nazo kwa kaskazini-mashariki mwa nchi, ambako familia kubwa huishi pamoja kwenye nyumba moja katika maeneo ya mbali na magumu kufikiwa. Ndani ya sekunde chache, nyumba zao zilizojengwa kwa udongo na mawe yasiyo imara zingebomoka. Barabara zingefunikwa na kifusi. Familia zingezikwa hai wakiwa wamelala.
Jambo la kwanza
Dkt. Sahak, ambaye ni kiongozi wa ofisi ya dharura ya Shirika la Umoja wa Mataifa la afya Duniani (WHO) katika eneo hilo, mara moja alituma ujumbe kwenye kundi la mtandao wa kijamii la WhatsApp, kundi linalounganisha hospitali, kliniki na mashirika ya misaada katika kanda hiyo.
Ripoti zilianza kuingia kutoka Asadabad, mji mkuu wa Mkoa jirani wa Kunar eneo lililoathiriwa zaidi karibu na mpaka wa Pakistan. Hospitali kuu ya jiji hilo ilimjulisha kwamba tetemeko lilihisiwa kwa nguvu sana. Baadhi ya wakazi huenda walikuwa wamejeruhiwa.
Ilipofika saa 7 usiku, simu zilikuwa za dharura zaidi. “Tumepokea majeruhi wengi kutoka maeneo tofauti na hali si nzuri. Ikiwezekana, tusaidieni haraka!”
Kukimbizana na mvua za Monsoon
Dkt. Sahak aliagiza timu yake ya WHO kukutana naye kwenye ghala la shirika hilo huko Jalalabad. Walipokuwa wakielekea huko usiku huo, mvua ilianza kunyesha ,mvua za monsoon ambazo zingevuruga kila kitu, kutoka kutua kwa helikopta hadi huduma za magari ya kubebea wagonjwa katika saa za kwanza za mwitikio wa kusaidia wenye wenye uhitaji.
Muda mfupi baadaye, mfumo wa misaada ulianza kufanya kazi. Lori lilijazwa vifaa vya matibabu kutoka ghala la WHO, likapelekwa hadi uwanja wa ndege wa Jalalabad kabla ya helikopta ya Wizara ya Ulinzi kuinua mizigo kuelekea Wilaya ya Nurgal ambako ndiko kulikuwa kiini cha tetemeko hilo, katikati ya Asadabad na Jalalabad.
“Kwa bahati nzuri, tuliweza kufika haraka katika eneo lililoathiriwa zaidi,” anasema Dkt. Sahak.
Ndani ya wilaya ya Nurgal
Timu ya kwanza ya Dkt. Sahak ilikuwa na watu wanne tu: yeye mwenyewe, mshauri wa kiufundi, mratibu wa dharura na msaidizi wa usalama. Ndani ya saa chache, walijiunga na mashirika mawili ya kitaifa, na kuunda kikosi cha watu 18 wakiwemo madaktari, wauguzi na mafamasia. “Wanne kati yao walikuwa madaktari wanawake na wakunga,” anasema.
Siku ya kwanza tu, WHO iliweza kupeleka tani 23 za dawa kwa helikopta hadi Nurgal. Wakati timu zikifanya kazi, idadi ya waliokufa ilikuwa ikiongezeka.
“Tulipata taarifa kuwa huenda watu 500 hadi 600 walikufa. Kulikuwa na maelfu ya majeruhi na nyumba nyingi zilizoharibiwa,” ana kumbuka Dkt. Sahak. Siku tano baadaye, taarifa rasmi zilikuwa mbaya zaidi: watu zaidi ya 2,200 wamekufa, 3,640 wamejeruhiwa, na nyumba 6,700 zimeharibika.
Walipofika Nurgal alasiri ya Jumatatu kwa gari la kivita, walikuta barabara nyingi zimefungwa kutokana na maporomoko ya mawe kutoka milimani.
Mtoto wangu yuko wapi!
Walipowasili, Dkt. Sahak, mfanyakazi wa misaada mwenye uzoefu mkubwa, hakuwa amejiandaa kwa kiwango cha uharibifu alichokiona.
“Tuliona miili barabarani. Zilikuwa zikingoja watu waje kuzika,” anasema.
Waokoaji wa kujitolea walimiminika kutoka wilaya jirani kuondoa kifusi, kuwabeba majeruhi, na kuwahifadhi marehemu.
Miongoni mwa walionusurika alikuwa mwanaume mwenye umri wa miaka 60 aitwaye Mohammed, ambaye nyumba yake ilikuwa imeharibiwa kabisa. “Alikuwa akiishi na jumla ya jamaa 30 wa familia yake… 22 kati yao walifariki kwenye tetemeko la ardhi, hili lilinishangaza sana. Sikuweza hata kumtazama usoni. Alikuwa akibubujikwa na machozi.” anasema Dkt. Sahak.
Katika kliniki ya eneo hilo, kuta zikiwa zimepasuka, wahudumu walikuwa wakihudumia majeruhi chini ya mahema. Dkt. Sahak alikutana na mwanamke aliyejeruhiwa vibaya alipasuka nyonga, majeraha kichwani na mbavu zilizovunjika.
“Alikuwa anashindwa kupumua na hakuweza kuacha kulia,” anasema Sahak.
“Alikuwa anasema tu: ‘Mtoto wangu yuko wapi! Nipe mtoto wangu! Tafadhali niletee mtoto wangu! kisha akasita kwa huzuni.“La hasha… alikuwa amempoteza mtoto wake. Familia yake yote ilikufa.”
Wanawake walijitokeza mstari wa mbele kusaidia waathirika
Katika nchi yenye masharti makali ya kijinsia, tetemeko la ardhi lilivunja mipaka ya kijamii kwa muda mfupi. “Katika siku za kwanza, kila mtu, wanaume kwa wanawake walikuwa wanasaidia kuokoa watu,” anasema Dkt. Sahak.
"Katika siku za kwanza, kila mtu, wanaume kwa wanawake walikuwa wanasaidia kuokoa watu,”
Madaktari wanawake na wakunga bado wanaweza kufanya kazi, lakini tu wakiwa na mwanaume wa familia. Hakuna mgonjwa mwanamke aliyenyimwa huduma.
Lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa wataalamu wanawake baada ya Taliban kurudi madarakani mwaka wa 2021.
“Madaktari bingwa wengi, hasa wanawake, waliondoka nchini... sasa ni vigumu kupata wafanyakazi wa kitaalamu.”
Athari hiyo ilimfikia hata nyumbani kwake. Binti yake mkubwa alikuwa mwaka wa tano wa chuo cha udaktari kabla ya wanawake kupigwa marufuku kusoma.
“Sasa kwa bahati mbaya, yuko nyumbani. Hawezi kufanya chochote. Hana nafasi ya kumaliza masomo yake.”
Hofu ya Familia
Kazi ya WHO ilikuwa kuhakikisha kliniki zinaendelea kutoa huduma ,miongozo ya kitaalamu, vifaa vya matibabu na motisha. Tuliwaambia, ‘Ninyi ni mashujaa!’. Wakati Dkt. Sahak aliwatia moyo madaktari, familia yake huko Jalalabad walikuwa na wasiwasi mkubwa wakifuatilia taarifa.
Siku hiyo ya kwanza alipopata nafasi ya kurudi nyumbani, mama yake mwenye umri wa miaka 85 ndiye aliyemlaki kwanza.
“Alinikumbatia kwa zaidi ya dakika 10,” anasema.
Alimkemea kwa upole na kumwomba asiende tena kwenye maeneo yaliyoathiriwa. Lakini maeneo ya maskini kama Nurgal, Chawkay, Dara-i-Nur na Alingar walitegemea msaada wa WHO. Asubuhi iliyofuata, alirudi tena kazini.
Hesabu ya dharura
Ifikapo Ijumaa alasiri, takwimu kwenye daftari la Dkt. Sahak zilieleza hadithi ya janga hilo:
Tani 46 za vifaa vya matibabu zilisambazwa, Chupa zaidi ya 15,000 za vifaa na tiba (glucose, lactate, sodium chloride) ziligawiwa, timu 17 za ufuatiliaji wa magonjwa zilitumwa kufuatilia milipuko inayotarajiwa kutokana na uharibifu wa vyanzo vya maji na mfumo wa usafi wa mazingira.
WHO iliomba dola milioni 4 kusaidia huduma muhimu za afya na kupanua huduma za afya ya simu.
Maneno ya mama
Nje ya hospitali, waliona manusura wawili mama mzee na binti yake waliokuwa wamepigwa jua, wakitafuta kivuli pembeni ya ukuta. Wote wawili walikuwa wametoka hospitalini, wakiwa peke yao.
“Walikuwa hai, lakini ndugu zao wote 13 walikuwa wamekufa,”
“Walikuwa hai, lakini ndugu zao wote 13 walikuwa wamekufa,” anasema Dkt. Sahak. “Binti, aliyekuwa na miaka ya ishirini, hakuweza hata kuongea .
Akiwa ameguswa na mateso yao, Dkt. Sahak aliomba hospitali iwahifadhi kitandani kwa wiki moja au mbili. Mkurugenzi alikubali. Usiku huo, aliporudi nyumbani, aliwasimulia familia yake tukio hilo. “Wote walikuwa wanalia, na hata hawakuweza kula chakula cha jioni,” anasema. Wakati huo, hata mama yake hakuendelea kumsihi abaki nyumbani. “Tafadhali nenda ukawasaidie watu,” alimwambia.