Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya kujua kusoma na kuandika katika zama za kidijitali

Picha ya karibu ya mikono ya mtu ikiandika kwenye daftari kwa kalamu ya bluu.
UN News/George Musubao Espérance Bialogire, Mkimbizi katika kambi la wakimbizi wandani ya Bulengo mashariki mwa DRC aliye nufaika kwa mradi wa WFP akifanya mazoezi ya kuandika na kusoma.

Siku ya kujua kusoma na kuandika katika zama za kidijitali

Na Sabrina Saidi
Utamaduni na Elimu

Ikiwa leo tarehe 8 Septemba ni siku ya Kimataifa ya kujua kusoma na kuandika ambapo Umoja wa Mataifa ulianzisha siku hii ili kuwakumbusha watunga sera, walimu, wadau wa elimu, na jamii juu ya umuhimu wa ujuzi wa kusoma na kuandika katika kujenga jamii yenye elimu, haki, amani na endelevu,  Sabrina Saidi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa anaiangazia kauli mbiu ya mwaka huu  "Kukuza ujuzi wa kusoma na kuandika katika zama za kidijitali" akiwashirikisha baadhi ya wadau wa elimu nchini Tanzania

Amezungumza na baadhi ya wadau kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, SAUT kilichoko jijini Mwanza, kaskazini-magharibi mwa Tanzania.

Dismas Nziku ni mwalimu wa masomo ya Biashara na Ujasiriamali  anazungumza kuhusu ni kwa jinsi gani ufundishaji wa zama hizi za kidijitali unavyochochea na kukuza ujuzi wa kusoma na kuandika. "Kwenye dunia ya sasa ujuzi wa kusoma na kuandika kidijitali ni msingi mkubwa kwa mwanafunzi, na miongoni mwa juzi hizi muhimu ni kama vile kujua kutumia vifaa vya kidijitali kama kompyuta, simu janja kwa ajili ya kujisomea na kutafuta maarifa, lakini pia kama mwalimu ninawafundisha wanafunzi kwa njia ya vitendo,kuandaa maswali ya utafiti kwa kutumia internet,kufanya kazi na kufanya kazi ya kikundi mitandaoni."

Kuhusu umuhimu wa siku hii kwake na inachangia vipi katika kukuza uelewa wa umuhimu wa kusoma na kuandika shuleni na katika jamii Mwalimu Nziku amesema, "Siku ya Kimataifa ya kujua kusoma na kuandika ni kumbusho muhimu kwamba elimu ni haki ya msingi, na ni msingi wa maendeleo kwa kila mmoja kujua kusoma na kuandika hasa hasa kidijitali, inanipa hamasa kama mwalimu kuendelea kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kusoma na kuandika si kwa ajili ya mitihani tu, bali kwa maisha yao ya kila siku."

Didas Karoli ni mwanafunzi katika chuo hicho cha SAUT akisoma shahada ya kwanza ya Mawasiliano kwa Umma, ameeleza kuhusu siku hii na jinsi maendeleo ya kidijitali yanavyochagiza katika kujifunza kwake akisema "Zana za kidijitali zimebadilisha sana upeo wangu katika suala la kujifunza,kutokana na zamani nilikuwa nategemea vitabu lakini hivi sasa natumia tu smartphone au kompyuta na kutengeneza notisi zangu mwenyewe za kujifunzia.Siku ya hii ya kujua kusoma na kuandika ni siku ambayo ni muhimu inafanya watu waweze kujua umuhimu wa kusoma na kuandika."