WHO yaongeza orodha ya dawa muhimu: Zipo za Saratani, kisukari na unene uliopitiliza
WHO yaongeza orodha ya dawa muhimu: Zipo za Saratani, kisukari na unene uliopitiliza
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO limefanya mabadiliko muhimu katika orodha yake ya dawa muhimu duniani au Essential Medicines List – EML na orodha ya dawa muhimu kwa watoto (EMLc) ikijumuisha dawa za kisasa za saratani, kisukari, unene uliopitiliza na magonjwa mengine sugu.
Orodha za WHO za dawa muhimu ni nyenzo za mwongozo zinazotumiwa na zaidi ya nchi 150 kupanga ununuzi, bima za afya na upatikanaji wa dawa. Kwa lugha rahisi, dawa zinazoorodheshwa hapa huwa na nafasi kubwa zaidi ya kununuliwa na kutolewa kwa wagonjwa kupitia huduma za umma kwani wanachama wa WHO wanaziweka dawa hizi kama kipaumbele cha kiafya kwa mamilioni ya watu duniani.
WHO wakati wakitangaza orodha hiyo mpya waliweka bayana kuwa dawa hizi mpya si za majaribio, bali ni zile ambazo zimethibitishwa kitabibu kuwa zinaokoa maisha, kupunguza madhara ya magonjwa na kuboresha maisha ya wagonjwa.
Nini maana yake?
Kuongezwa kwa dawa hizi ni hatua ya mbele katika safari ya kuhakikisha afya bora kwa wote. Inamaanisha wagonjwa zaidi wa saratani, kisukari na magonjwa mengine sugu wanaweza kuwa na matumaini ya maisha marefu na bora. Pia ni wito kwa mataifa kuchukua hatua ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa unakuwa wa haki na usawa, bila kumwacha mtu yeyote nyuma.
Changamoto ya bei na usawa wa kiafya
Changamoto kubwa sasa ni bei kubwa ya dawa hizi mpya, ambazo zinaweza kufanya wagonjwa wengi kushindwa kuzipata.
WHO inapendekeza mikakati ya kupunguza gharama na kuhakikisha dawa hizi zinapatikana kwenye ngazi ya huduma za msingi za afya.
Deusdedit Mubangizi, Mkurugenzi wa Sera na Viwango vya Dawa WHO, anasema “Sehemu kubwa ya matumizi ya nje ya mfuko wa magonjwa yasiyoambukiza yanaelekezwa kwenye dawa, ikiwa ni pamoja na zile zinazoainishwa kama muhimu na ambazo kimsingi, zinapaswa kupatikana kwabei rahisi kwa kila mtu. Ili kufikia upatikanaji sawa wa dawa muhimu kunahitajika mwitikio madhubuti wa mfumo wa afya unaoungwa mkono na dhamira dhabiti ya kisiasa, ushirikiano wa sekta nyingi na programu zinazozingatia watu ambazo hazimwachi mtu nyuma.”
Kwa maneno mengine, dawa hizi haziwezi kuwa za matajiri pekee lazima mifumo ya afya, serikali na sekta binafsi zishirikiane kuhakikisha kila mtu anayehitaji anapata dawa kwa gharama nafuu.
Saratani, kisukari na unene uliopitiliza ni changamoto
Saratani na kisukari ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo na ulemavu kwa mamilioni ya watu duniani kila mwaka. Kwa mfano, saratani pekee inaua karibu watu milioni 10 kila mwaka.
Kuongeza dawa mpya za saratani kama pembrolizumab na atezolizumab, ambazo zinasaidia kinga ya mwili kushambulia chembe chembe za saratani, kunaleta matumaini mapya hasa kwa wagonjwa katika nchi zenye rasilimali chache.
Kwa upande mwingine, dawa za kundi la GLP-1 receptor agonists kama semaglutide na tirzepatide zimeingizwa kwenye orodha ili kusaidia wagonjwa wa kisukari cha aina ya pili wanaoishi pia na unene uliopitiliza au matatizo ya moyo na figo. Dawa hizi husaidia kudhibiti sukari, kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na figo, na pia kusaidia kupunguza uzito.