Shambulio kubwa la Urusi Ukraine, Umoja wa Mataifa watoa msaada wa dharura
Wazima moto wanafanya kazi katika vifusi vya jengo la makazi huko Kyiv lililoharibiwa katika mgomo wa kombora mnamo Agosti 28. (Maktaba)
Shambulio kubwa la Urusi Ukraine, Umoja wa Mataifa watoa msaada wa dharura
Amani na Usalama
Mtoto mchanga ni miongoni mwa waliouawa usiku wa kuamkia Jumapili ya Septemba 8 katika kile kilichoripotiwa kuwa shambulio kubwa la anga la Urusi dhidi ya Ukraine tangu uvamizi wake wa mwaka 2022 uanze kwa ukubwa.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, zaidi ya ndege zisizo na rubani 800 (drones) zilirushwa kwa wimbi lililolenga kuzidi uwezo wa ulinzi wa anga wa Ukraine, na jengo la Serikali mjini Kyiv likapigwa kwa mara ya kwanza.
Mamlaka za Ukraine zimeripoti vifo vya watu wanne na majeruhi 44. Kelele za ving’ora vya mashambulizi ya anga ziliendelea kwa saa 11 mfululizo katika mji mkuu, na ingawa idadi kubwa ya ndege hizo zilidunguliwa, zaidi ya ndege 50 na makombora tisa yalifikia malengo yake.
“Kwa mara nyingine tena, mashambulizi yameathiri nyumba za raia, jengo la Serikali, shule ya chekechea na miundombinu mingine ya kiraia katika miji ya Kyiv, Chernihiv, Kharkiv, Kremenchuk, Kryvyi Rih, Odesa, mkoa wa Sumy na Zaporizhzhia yakiacha nyuma majonzi, uharibifu na maangamizi,” amesema Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine, Matthias Schmale, kupitia chapisho kwenye mitandao ya kijamii.
Afisa huyo mwandamizi wa misaada amesema kuwa kwa kushirikiana na mamlaka, Umoja wa Mataifa na washirika wa kibinadamu wamechukua hatua za dharura kusaidia raia na maeneo ya kiraia yaliyopata madhara.
Raia hawapaswi kulengwa
“Raia na miundombinu ya kiraia inalindwa chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu siyo shabaha,” ameendelea.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema kuwa taarifa za mtoto mchanga kuuawa pamoja na mama yake kijana katika shambulio la jengo la makazi mjini Kyiv ni “zinasikitisha sana.” Mtoto mwingine amejeruhiwa wakati wa mashambulizi katika mkoa wa Sumy.
“Ukraine imeshuhudia tena usiku wa kutisha wa mashambulizi yaliyoathiri miji mingi. Maisha zaidi ya vijana yamekatishwa kikatili,” shirika hilo liliandika kwenye mtandao wa kijamii.
Mashambulizi hayo yamekuja baada ya wiki kadhaa za diplomasia za juu kutoka kwa washirika wa Magharibi wa Serikali ya Ukraine katika jitihada za kusaka makubaliano ya amani ya kudumu kati ya Kyiv na Moscow.
Rais Volodymyr Zelenskyy amesema kupitia chapisho la mtandao wa kijamii baada ya mashambulizi hayo kwamba “mauaji kama haya sasa, wakati ambapo diplomasia ya kweli ingeweza kuanza tangu zamani, ni uhalifu wa makusudi na njia ya kuendeleza vita.”