Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa UN wataka matumizi ya teknolojia yenye uwajibikaji katika ulinzi wa usalama

Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) akikabidhi Tuzo ya Afisa Polisi Mwanamke Bora wa Umoja wa Mataifa kwa Kamishna Zainab Gbla wa Sierra Leone. (Maktaba)
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) akikabidhi Tuzo ya Afisa Polisi Mwanamke Bora wa Umoja wa Mataifa kwa Kamishna Zainab Gbla wa Sierra Leone. (Maktaba)

Viongozi wa UN wataka matumizi ya teknolojia yenye uwajibikaji katika ulinzi wa usalama

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Katika maadhimisho ya tatu ya Siku ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Polisi inayoadhimishwa kila Septemba 7, viongozi wakuu wa Umoja wa Mataifa wameangazia fursa na changamoto zinazotokana na akili mnemba (AI) na teknolojia za kidijitali katika kazi za utekelezaji wa sheria, wakisisitiza kwamba ubunifu lazima uzingatie haki za binadamu, uwajibikaji na uaminifu.

Katibu Mkuu António Guterres amesisitiza kwamba ingawa AI na nyenzo nyingine za kidijitali zinaweza kuimarisha uchunguzi, kupanua upatikanaji wa haki na kusaidia kuzuia uhalifu na ugaidi, haziwezi kamwe kuchukua nafasi ya maamuzi ya kibinadamu. “Katika maamuzi ya kila siku ya polisi ambayo yanaathiri maisha, ubinadamu lazima ubaki kiini,” amesema, akihimiza ushirikiano ili kuhakikisha teknolojia inahudumia manufaa ya umma.
 
Jean-Pierre Lacroix, Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa, yeye anataja maendeleo kama vile jukwaa la Situational Awareness Geospatial Enterprise (SAGE) na Unite Aware linalounganisha taarifa ili kuboresha hatua za walinda amani. Hata hivyo, anaonya kwamba vikosi vingi vya polisi bado vinakabiliwa na changamoto za miundombinu na rasilimali, na hivyo zinahitaji suluhu za pamoja ili kuhakikisha matumizi yenye uwajibikaji.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC), Ghada Waly, anaonya kuhusu hatari za upendeleo, ufuatiliaji kupita kiasi na kupungua kwa imani ya wananchi, akisisitiza kwamba “usalama wa umma haupaswi kuja kwa gharama ya haki na uhuru.”
Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Utafiti wa Kimataifa wa Uhalifu na Haki (UNICRI) kwa upande wake inasisitiza dhamira yake, ikibainisha kazi yake na INTERPOL ya kuandaa Zana ya Ubunifu wa Uwajibikaji wa Akili Mneba katika Utekelezaji wa Sheria ili kusaidia matumizi ya maadili ya teknolojia mpya.
 
Wakati huohuo, Vladimir Voronkov, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kukabiliana na Ugaidi (UNOCT), anasisitiza jukumu muhimu la polisi katika kukabiliana na ugaidi. Anaeleza programu zinazotoa mafunzo kuhusu usalama wa mtandao na AI, akibainisha kuwa zaidi ya maafisa 280 barani Afrika walifundishwa mwaka jana pekee.
 
Kwa kutambulisha mada ya mwaka huu  Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na AI katika Ulinzi wa Polisi viongozi wa Umoja wa Mataifa wamethibitisha tena kwamba usasa lazima uendane na uwazi, uangalizi, na mtazamo unaomweka mwanadamu katikati ya huduma za polisi.