Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

“Maisha yetu yamekatizwa,” wasema wakulima wa Ukingo wa Magharibi kabla ya msimu wa mavuno ya zeituni

Mavuno ya mizeituni katika Ukingo wa Magharibi.
© UNRWA
Mavuno ya mizeituni katika Ukingo wa Magharibi.

“Maisha yetu yamekatizwa,” wasema wakulima wa Ukingo wa Magharibi kabla ya msimu wa mavuno ya zeituni

Amani na Usalama

Msimu wa kuvuna zeituni ni chanzo kikuu cha riziki kwa maelfu ya familia na pia ni sehemu muhimu ya urithi wa Wapalestina. Katika kijiji cha Kufr Qaddum kilichoko katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel, Yousef anasimama nyuma ya lango la chuma lililofungwa, akiwa ametenganishwa na miti ya zeituni ambayo imekuza familia yake kwa vizazi kadhaa.

Kama maelfu ya wakulima wa Palestina, Yousef  anakumbwa na vizuizi vinavyozidi kuongezeka kutoka kwa majeshi ya Israel na walowezi, ambao wamegeuza msimu wa mavuno ya zeituni  unaofanyika kati ya Septemba na Novemba kuwa kipindi cha wasiwasi na mateso.

Katika miaka ya hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limekuwa likiwasaidia wakulima wa zeituni na vyama vya ushirika kuboresha upatikanaji na usimamizi wa ardhi na rasilimali za maji, kuanzisha mbinu endelevu kama vile upandaji wa mazao mchanganyiko, na kuwasaidia kuongeza uzalishaji wa chakula na kipato kwa kutumia rasilimali asilia kwa ufanisi zaidi.

Msimu wa mavuno ya zeituni ni chanzo kikuu cha mapato kwa maelfu ya familia na pia ni sehemu ya urithi wa Wapalestina.

Hata hivyo, mashambulizi dhidi ya mavuno hayo yanatishia urithi huo na kuzuia kazi na maisha ya wakulima wa Palestina huku mashambulizi ya walowezi yakifikia kiwango cha juu zaidi katika takribani miongo miwili, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, (OCHA).

Hatari zisizokuwa za kawaida

“Kadri Ukingo wa Magharibi unavyojiandaa kwa msimu wa kila mwaka wa kuvuna zeituni, ujumbe kutoka kwa wakulima ni wazi, msimu wa mwaka huu umejaa mashaka na maisha ya watu yako kwenye hatari ya kipekee,” amesema Ciro Fiorillo, Mkuu wa Ofisi ya FAO katika Ukanda wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.

Mchanganyiko wa sera za serikali na vurugu za walowezi umezuia Wapalestina kufikia makumi ya maelfu ya dunumu za mashamba na maeneo ya malisho  ambapo dunumu moja ni sawa na mita 1,000.

Vizuizi hivi vimechangia uharibifu wa uchumi wa ndani na kusababisha maelfu ya wakulima na wafugaji wa Kipalestina kufurushwa katika hali ambazo huenda zinafikia kiwango cha kuhamishwa kwa lazima, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu (OHCHR).

“Maisha yetu yamekatizwa, mazao ya zeituni ndiyo chanzo kikuu cha mapato kwa wakulima,” anasema mkulima wa Kipalestina kutoka kijiji cha Kufr Qaddum alipoongea na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Kunyimwa haki ya ardhi

“Kwa miaka miwili sasa, tumenyimwa haki ya ardhi yetu,” anasema Yousef, mkulima wa Kipalestina kutoka Kufr Qaddum alipoongea na Idhaa ya Umoja wa Mataifa. Eneo lote la kaskazini la kijiji hilo limefungwa kwa lango la chuma kufuatia mvutano wa hivi karibuni kati ya Iran na Israel.

Familia ya Yousef inamiliki zaidi ya dunumu 300 za ardhi, nyingi ikiwa na miti ya zeituni, iliyoko karibu na makazi ya walowezi wa Israeli ya Kedumim katika Mkoa wa Qalqiliya. Tangu shambulio la Hamas dhidi ya Israel mwaka 2023, hawajapata tena fursa ya kufikia ardhi yao  hata wakati wa msimu wa mavuno.

“Maeneo haya yana ukubwa wa takriban elfu nne hadi elfu tano za dunumu. Tumekatazwa kuyafikia,” alisema Yousef, na kuongeza kwamba “tatizo hili limewaathiri wakulima wote katika Ukingo wa Magharibi.”

Mohammed, mkulima wa Kipalestina kutoka kijiji cha Kifl Harris, kilicho karibu na makazi ya walowezi ya Ariel katika Mkoa wa Salfit, amezuiwa kufikia zaidi ya dunumu 3,000 za ardhi yenye miti ya zeituni iliyopo ndani ya mipaka ya makazi hayo. Kizuizi hiki kimewanyima wakulima wa Kifl Harris uwezo wa kuitunza na kuivuna miti yao.

“Msimu wa zeituni ndio njia yetu kuu ya kujikimu kiuchumi kwa wakulima pamoja na wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi,” alisema Mohammed kwa UN News, na kuongeza kuwa wakulima wa Palestina hawakupewa sababu yoyote ya kuzuiwa kufikia mashamba yao.

“Baada ya walowezi kuweka kibanda kwenye ardhi ya familia yetu, tulinyimwa haki ya kufikia zaidi ya dunumu 200 za ardhi ya kilimo nyingi zikiwa zimepandwa miti ya zeituni,” alisema Ahmed, mkulima kutoka Khalet Al Luza alipoongea na OCHA.

Unyanyasaji kutoka kwa walowezi

“Tumevumilia kila aina ya unyanyasaji kutoka kwa walowezi na jeshi la Israel,” anasisitiza Yousef

Katika maoni ya ushauri yaliyochapishwa Julai 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ilihitimisha kuwa uwepo wa Israel katika Ardhi ya Palestina inayokaliwa Israeli  ni kinyume cha sheria, na kwamba ina wajibu wa kumaliza uwepo huo “haraka iwezekanavyo.”

“Mashambulizi ya walowezi yamewaathiri wakulima wote. Mimi binafsi nimezuiwa kufikia ardhi yangu, na tumekuwa tukishambuliwa mara kwa mara na walowezi na jeshi, ikiwa ni pamoja na wizi wa mazao ya zeituni, vifaa vya kuvunia, uharibifu wa magari, kukatwa kwa miti ya zeituni, na vitisho,” alisema Yousef.

Katika taarifa iliyotolewa tarehe 30 Julai, Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) ilionya juu ya ongezeko la vurugu kutoka kwa walowezi wa Kiyahudi “kwa ridhaa, msaada, na katika baadhi ya matukio ushiriki” wa majeshi ya Israeli.

Taarifa hiyo ilisema kuwa sera na hatua za kisheria za Serikali ya Israeli “zinaonekana kulenga kuwaondoa Wapalestina kutoka maeneo fulani ya West Bank, kuendeleza makazi ya walowezi, na kuimarisha hatua za kinyakuzi” za sehemu kubwa ya ukingo wa Magharibi.

“Tunaomba mfanye kazi na taasisi za kimataifa kwa njia za amani ili tupate suluhisho litakalotuwezesha kufikia mashamba yetu kwa usalama na kuvuna matunda ya miti yetu ya zeituni,” anasihi Yousef.

“Pamoja na washirika wetu wa rasilimali, FAO imejizatiti kuendelea kusaidia kilimo cha zeituni cha ndani, ambacho ni muhimu kwa maisha na usalama wa chakula sawa na jinsi kilivyo muhimu kwa utamaduni na urithi wa Wapalestina,” anasema Bwana Fiorillo.