Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko mpya wa Ebola watangazwa katika jimbo la Kasai DRC, WHO na IOM wachukua hatua

Wahudumu wa afya wakivaa vifaa vya kujikinga katika kituo ambacho watu wanaoshukiwa kuwa na Ebola wamewekwa katika karantini kuweza kufanyiwa uchunguzi na uangalizi na kisha kupatiwa matibabu nchini DRC (kutoka maktaba)
World Bank/Vincent Tremeau
Wahudumu wa afya wakivaa vifaa vya kujikinga katika kituo ambacho watu wanaoshukiwa kuwa na Ebola wamewekwa katika karantini kuweza kufanyiwa uchunguzi na uangalizi na kisha kupatiwa matibabu nchini DRC (kutoka maktaba)

Mlipuko mpya wa Ebola watangazwa katika jimbo la Kasai DRC, WHO na IOM wachukua hatua

Afya

Mamlaka za afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC zimethibitisha mlipuko mpya wa ugonjwa wa Ebola katika Mkoa wa Kasai, huu ukiwa ni mlipuko wa 16 tangu virusi hivyo vilipotambulika kwa mara ya kwanza mwaka 1976 limesema leo Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO

Timu ya pamoja ya kitaifa ya DRC ya masuala ya dharura ikisaidiwa na wataalamu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, imetumwa kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huo na kuimarisha maandalizi ya dharura.

WHO imesema imetuma zaidi ya tani mbili za vifaa muhimu kwenda Kasai, vikiwemo mavazi ya kujikinga, vifaa vya tiba na maabara tembezi. “Hadi sasa, visa 28 vinavyoshukiwa na vifo 16 vimeripotiwa, wakiwemo wahudumu wa afya wanne,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, akiwaeleza waandishi wa habari mjini Geneva.

Alibainisha pia kuwa dozi 2,000 za chanjo ya Ebola, zilizohifadhiwa awali mjini Kinshasa, zitatolewa mara moja kwa ajili ya kuwachanja watu waliokaribiana na wagonjwa pamoja na wahudumu wa afya. Ameongeza kuwa “Huu ni mlipuko wa 16 wa Ebola katika taifa la DRC, na serikali ina uzoefu mkubwa kutokana na milipuko iliyopita”.

Uhamasishaji wa wahudumu wa afya kabla ya kuanza kazi ya kupiga dawa za kusafisha nyumba huko  nchini DRC kujikinga na  mlipuko wa Ebola.
WHO
Uhamasishaji wa wahudumu wa afya kabla ya kuanza kazi ya kupiga dawa za kusafisha nyumba huko nchini DRC kujikinga na mlipuko wa Ebola.

IOM yataka kipaumbele kiwekwe kwa watu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM limethibitisha kuwa limepeleka timu jimboni Kasai kufanya utafiti wa mienendo ya watu na kubaini maeneo hatarishi ya uenezaji wa virusi, kama vile masoko, vituo vya basi na makanisa.

“IOM ipo pamoja na jamii zilizoathirika katika wakati huu muhimu,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope. “Kukabiliana na mlipuko huu kunahitaji hatua za haraka, uratibu wa karibu, na zaidi ya yote, mtazamo unaoweka watu mbele, unaolinda wahudumu wa afya, kuzuia maambukizi zaidi, na kuhakikisha kila mtu anapata huduma na taarifa wanazohitaji.”

Maafisa wa afya wa DRC wamesema mlipuko huu ulibainika kupitia ufuatiliaji makini wa kitabibu na uchunguzi wa maabara. Kisa cha kwanza kilikuwa cha mwanamke mjamzito aliyelazwa hospitali tarehe 20 Agosti. Yeye na wahudumu wa afya wawili waliomhudumia wamo miongoni mwa waliopoteza maisha.

Mamlaka za kitaifa sasa zimeanzisha Kituo cha dharura cha afya ya umma na zinaendesha hatua za haraka, ikiwemo ufuatiliaji wa waliokaribiana na wagonjwa, kampeni za chanjo, na matibabu ya wagonjwa.

Shughuli za mazishi ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa wa Ebola katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini DR Congo (kutoka maktaba)
UN/Martine Perret
Shughuli za mazishi ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa wa Ebola katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini DR Congo (kutoka maktaba)

Uangalifu na utulivu vyahitajika

Maafisa wa afya nchini DRC wanawahimiza wananchi kuepuka kugusana na wagonjwa au marehemu, kutochukua wanyama waliokufa, kudumisha usafi wa hali ya juu, na kuripoti mara moja visa vinavyoshukiwa kupitia namba ya bure 151.

“DRC ina uzoefu mkubwa wa kudhibiti milipuko ya Ebola, na ujuzi huu unatumiwa tena sasa,” amesisitiza Dkt. Tedros. WHO na IOM zote zimesisitiza kujitolea kwao kusaidia mamlaka za DRC kudhibiti mlipuko huu, kulinda wahudumu wa afya, na kuwalinda wananchi walio katika hatari.

Jana Alhamisi WHO ndio ilitangaza rasmi mlipuko huo mpya wa Ebola DRC baada ya kupokea taarifa za uthibitoshi kutoka kwenye mamlaka ta taifa hilo .