Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhalifu wa kivita watamalaki Sudan, SAF na RSF wote wahusika: OHCHR

Kufuatia mashambulizi kwenye kambi za Zamzam na Abu Shouk, makao ya zaidi ya watu 700,000, watu wengi wamelazimika kuyahama makazi yao.
© UNICEF/Mohammed Jamal
Kufuatia mashambulizi kwenye kambi za Zamzam na Abu Shouk, makao ya zaidi ya watu 700,000, watu wengi wamelazimika kuyahama makazi yao.

Uhalifu wa kivita watamalaki Sudan, SAF na RSF wote wahusika: OHCHR

Haki za binadamu

 

Raia wa Sudan wanakumbwa na ukatili mkubwa unaojumuisha uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu imesema Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi kuhusu haki za binadamu Sudan ilitoteuliwa na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR.

Tume hiyo imebaini kuwa pande zote mbili katika mzozo yaani Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka RSF zimekuwa zikiwalenga raia kwa makusudi kama sehemu ya mkakati wao wa vita.

Hayo yamo kwenye ripoti ya tume hiyo, iliyowasilishwa kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa leo hii huko Geneva Uswisi.

Ripoti kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, yenye maudhui “Vita vya Kikatili” imebaini kuwa jeshi la Sudan SAF na Kikosi cha Msaada wa Haraka RSF wote wamehusika na  mashambulizi ya moja kwa moja na ya kiwango kikubwa dhidi ya raia, pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu muhimu , ikiwa ni pamoja na vituo vya afya, masoko, mifumo ya chakula na maji na makambi ya wakimbizi wa ndani hali inayoathiri mamilioni ya watu.

Oumalis Abdraman na mtoto wake mwenye umri wa miezi sita waliwasili kutoka Darfur Magharibi huko Koulbus ambako walipokea matibabu ya WFP dhidi ya utapiamlo.
© WFP/Lena von Zabern
Oumalis Abdraman na mtoto wake mwenye umri wa miezi sita waliwasili kutoka Darfur Magharibi huko Koulbus ambako walipokea matibabu ya WFP dhidi ya utapiamlo.

RSF wametekeleza mauaji, ubakaji na utumwa

Ripoti hiyo pia imebaini kuwa RSF, wakati wa kuzingira mji wa El Fasher na maeneo ya jirani, wametenda uhalifu mbalimbali dhidi ya ubinadamu ikiwa ni pamoja na:

  • Mauaji
  • Mateso
  • Utumwa na ukatili wa kingono
  • Ubakaji na ukatili wa kijinsia
  • Na kuwafurusha raia kwa misingi ya kabila, jinsia, na siasa

Kwa mujibu wa tume hiyo walikusudia kuwanyima raia mahitaji ya msingi kwa kuzuia chakula, dawa, na misaada, jambo linalofikia kiwango cha uhalifu wa maangamizi.

Watoto na familia wakikimbia kwa miguu kutoka Wad Madani, jimbo la Al Jazirah kufuatia mapigano ya hivi karibuni.
© UNICEF/UNI492302/Mohamdeen
Watoto na familia wakikimbia kwa miguu kutoka Wad Madani, jimbo la Al Jazirah kufuatia mapigano ya hivi karibuni.

Raia walengwa kwa sababu za kikabila na kisiasa

Ripoti hiyo ya tume imesema raia wamekuwa wakilengwa kutokana na fikra kwamba wanashirikiana na upande wa pili. Katika eneo la El Fasher na maeneo ya jirani, RSF na washirika wao wametekeleza mauaji ya kiwango kikubwa ya mamia ya raia, wakilenga kwa makusudi jamii zisizo za Kiarabu, zikiwemo Zaghawa, Fur, Masalit na Tunjur  na kuwafurusha kwa nguvu. Katika kambi ya Zamzam mwezi Aprili mwaka huu, watu kati ya 300 na 1,500 wengi wao wakiwa wanawake na watoto waliuawa kikatili.

Huko Gezira, SAF na washirika wao walilenga jamii ya Kanabi baada ya kuukomboa mji mwezi Januari, wakiua  watu na kusababisha wengi kufunga virago na kukimbia.

Uharibifu wa kijeshi usiojali raia

Ripoti ya tume imesisitiza kuwa pande zote mbili zimekosa kuchukua hatua za kutosha kupunguza athari za mashambulizi ya anga na makombora kwa raia na miundombinu yao.

Matokeo yake, miji, vijiji, makambi ya wakimbizi, masoko, hospitali na makazi yameharibiwa kwa mfumo au kufanywa yasiyofaa kwa matumizi ya kibinadamu na kupelekea watu milioni 12.1 kufurushwa makwao na zaidi ya nusu ya taifa kukumbwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Ni kituo kimoja tu cha afya kati ya vinne kilichobaki kikifanya kazi katika maeneo yaliyoathirika zaidi imesema tume.

Lori la WFP likiwa na msaada wa chakula lawasili kambi ya Zamzam Sudan
United Nations
Lori la WFP likiwa na msaada wa chakula lawasili kambi ya Zamzam Sudan

Kushambuliwa kwa wafanyakazi wa misaada na vizuizi kwa misaada

Misaada ya kibinadamu imezuiwa, misafara ya misaada inashambuliwa na wafanyakazi wa misaada kulengwa kwa mujibu wa ripoti.

Ikiongeza kuwa kati ya Aprili 2023 na Aprili 2025, zaidi ya wafanyakazi 84 wa kibinadamu wa Sudan waliuawa, huku wengine wakikamatwa kiholela.

Ripoti imebaini kuwa pande zote mbili zimewakamata kiholela, kuwatesa na kuwaweka kizuizini raia kutokana na kabila lao, maoni yao ya kisiasa, taaluma au madai ya kushirikiana na upande pinzani.

Wafungwa wanashikiliwa bila chakula cha kutosha, huduma za usafi au matibabu. Vituo vya vizuizi vya RSF vimeelezewa na manusura kama “machinjioni” ambapo baadhi ya wafungwa walipigwa hadi kufa au kuuawa papo kwa hapo.

Baadhi walilazimishwa kufanya kazi au kushikiliwa kwa ajili ya fidia, huku familia zao zikilazimika kulipa ili waachiliwe.

Ukatili wa kijinsi kwa wanawake na wasichana

Ukatili wa kijinsia na wa kingono, ikiwa ni pamoja na ubakaji  wa makundi, ndoa za kulazimishwa na utumwa wa kingono umetendwa na wapiganaji wa RSF.

Wanawake na wasichana kutoka jamii zisizo za Kiarabu baadhi yao wakiwa na umri wa miaka 12, wamelengwa kwa kiasi kikubwa. Wapiganaji wa SAF na washirika wao pia wamehusishwa na vitendo vya mateso ya kingono katika vituo vya vizuizi.

“Nyuma ya kila simulizi iliyotolewa kuna familia iliyovunjika, jamii iliyofurushwa, na manusura wa ukatili usioelezeka,” amesema Joy Ngozi Ezeilo, Mjumbe wa Tume ya Uchunguzi.

“Tumewahoji raia wengi waliopitia mateso makubwa na kushuhudia au kuathiriwa na mauaji, njaa, ukatili wa kingono, mateso, na uharibifu wa huduma muhimu. Mzunguko wa kutowajibika umewatia nguvu wakatili hao kwa miongo kadhaa. Waathiriwa hasa wanawake na watoto  wanahitaji haki na fidia.” Joy Ngozi Ezeilo amesisitiza

Jaji Mohamed Chande Othman wa Tanzania mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Sudan
UN News
Jaji Mohamed Chande Othman wa Tanzania mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Sudan

Dunia yatakiwa kuchukua hatua za haraka

Tume ya Uchunguzi imetoa wito wa:

  • Utekelezaji wa marufuku ya silaha
  • Kuwezesha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC kutekeleza wajibu wake
  • Kuweka chombo huru cha kimahakama kwa ajili ya Sudan
  • Kutumia mamlaka ya kimataifa kuwawajibisha wahusika
  • Kuweka vikwazo vya moja kwa moja dhidi ya wahalifu

Wito: Uwajibikaji siyo hiari, ni wajibu wa kisheria

Tume hiyo ya Uchunguzi imezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka na za pamoja kusitisha mapigano, kuwalinda raia, kuondoa mizingiro na kusitisha ukatili wa kikabila na wa kijinsia.

Pia imezitaka nchi zote hasa zile zenye ushawishi kwa pande husika katika mzozo, kuheshimu marufuku ya silaha, kuacha kuwasaidia kwa vifaa, na kuongeza misaada ya kibinadamu.

“Sudan inapitia moja ya migogoro mikubwa ya kibinadamu duniani na hali mbaya ya njaa, huku sehemu ya watu wake wakikumbwa na uhalifu wa kivita, mateso na maangamizi,” alisema Othman Chande mwenyekiti wa tume hiyo  akiongeza kuwa “Jumuiya ya kimataifa ina zana za kuchukua hatua. Kushindwa kufanya hivyo siyo tu usaliti kwa watu wa Sudan  bali ni usaliti kwa misingi yenyewe ya sheria za kimataifa.”