Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hewa chafuzi haina mipaka, hatua zimepigwa lakini hali bado inazorota - WMO

Uwanja wa michezo wa shule huko Kleszczow, Poland, wenye uwanja wa mpira wa kikapu na uwanja wa mpira wa miguu mbele, na moshi wa kiwanda cha umeme cha Belchatow kinachotumia makaa ya mawe ukitoa moshi nyuma chini ya anga lenye mawingu.
Climate Visuals/Anna Liminowicz Uwanja wa michezo wa shule katika kitongoji cha Belchatow, Kleszczow, Poland, karibu na kiwanda cha kuzalisha umeme kwa makaa ya mawe.

Hewa chafuzi haina mipaka, hatua zimepigwa lakini hali bado inazorota - WMO

Tabianchi na mazingira

Wakati mabilioni ya watu wakiendelea kuvuta hewa chafu inayosababisha zaidi ya vifo vya mapema milioni 4.5 kila mwaka, leo Ijumaa ya Septemba 5, wataalamu wa tabianchi wa Umoja wa Mataifa wamebainisha madhara ya chembechembe ndogo za moshi kutoka kwenye moto wa nyika ambazo husafiri umbali mrefu duniani kote.

Lorenzo Labrador, Afisa wa Kisayansi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani (WMO) anasema, “Ubora wa hewa hauna mipaka. Moshi na uchafuzi unaotokana na moto wa nyika katika msimu huu wa kihistoria katika Rasi ya Iberia tayari umegunduliwa huko Ulaya Magharibi [na]… unaweza kusafiri kimsingi kote barani Ulaya.”
 
Akiwasilisha Taarifa ya Hewa Safi na Mabadiliko ya Tabianchi ya WMO iliyokusanya data kutoka takwimu  mbalimbali za kimataifa, Bwana Labrador ametangaza kuendelea kwa mwenendo wa kuzorota kwa hali ya hewa duniani.
 
Ameonesha ramani ya dunia ya mwaka 2024 inayoonesha alama za chembechembe ndogo zinazojulikana kama “PM 2.5” kutokana na moto wa nyika, zilizojitokeza kwa rangi nyekundu kwenye maeneo ya Chile, Brazil na Ecuador, pamoja na Canada, Afrika ya Kati na Siberia.
 
Takwimu hizo zinathibitisha mwenendo wa kutisha wa kupungua kwa ubora wa hewa uliokwisha kuonekana katika miaka iliyopita.
 
“Tunajua kwamba msimu wa moto wa nyika huwa na tabia ya kuwa mkali zaidi na mrefu kila mwaka, kutokana na mabadiliko ya tabianchi,” Ameeleza Bwana Labrador.
 

China, Ulaya zatoa matumaini


Habari njema, amesema mwanasayansi wa WMO, ni kupungua kwa utoaji wa hewa chafuzi katika baadhi ya maeneo ya dunia, “hasa mashariki mwa China na Ulaya, mwaka hadi mwaka.”
 
“Tukiangalia pale ambapo nchi au miji inachukua hatua za kupambana na ubora duni wa hewa, matokeo yanaonekana,” anasema Paolo Laj, Mkuu wa Kitengo cha Hewa Duniani katika WMO.
 
Mfano mzuri ni mashariki mwa China, katika miji kama Shanghai, ambako hatua zimechukuliwa kuboresha ubora wa hewa kwa kufungua bustani nyingi na kupanda miti zaidi.
 
Na ingawa bado kuna msongamano mkubwa wa magari, mengi sasa ni ya umeme, anasema msemaji wa WMO Clare Nullis.
 
Licha ya mafanikio hayo, miji michache sana duniani ina viwango vya ubora wa hewa chini ya vile vinavyopendekezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), anasisitiza Bwana Laj wa WMO. “Hii inamaanisha kuwa, licha ya maboresho ya karibuni, ubora wa hewa bado ni tatizo kubwa la afya ya umma.”
 
Ameeleza kuwa ingawa vichafuzi vikuu kama vile (SO₂) (NOₓ) vinaendelea kupungua kutokana na udhibiti wa utoaji hewa, viwango vya ozoni ardhini kiungo kikuu cha smogi, havijashuka.
 
“Hii kwa sehemu ni matokeo ya ongezeko la joto duniani, kwa kuwa ozoni ni kichafuzi cha pili kinachoundwa kutokana na michakato ya kemikali angani inayohitaji mwanga wa jua,” aliendelea kueleza Bw. Laj.
 
Kwa kufunika moto wa nyika, ukungu wa msimu wa baridi, moshi wa meli na uchafuzi katika maeneo ya mijini, taarifa ya ubora wa hewa ya WMO inasisitiza uhusiano wa karibu kati ya ubora wa hewa na mabadiliko ya tabianchi.
 
“Mabadiliko ya tabianchi na ubora wa hewa haviwezi kushughulikiwa pekee. Vinakwenda sambamba na lazima vitatuliwe kwa pamoja ili kulinda afya ya sayari yetu, jamii zetu na uchumi wetu,” amesema Naibu Katibu Mkuu wa WMO Ko Barrett.
 
Umoja wa Mataifa unaongoza juhudi za kupambana na uchafuzi wa hewa majumbani ambao ni mojawapo ya vitisho vikubwa zaidi kwa afya ya umma duniani na hasa ni hatari kwa watoto.
 
“Habari njema ni kwamba teknolojia safi ya kupikia ipo kwa wingi, ni nafuu kiasi, na tayari inasaidia kuokoa maisha,” amesisitiza Martina Otto, Mkuu wa Sekretarieti ya Muungano wa Tabianchi na Hewa Safi unaoendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP) na anaongeza akisema, “Changamoto sasa ni kuhakikisha teknolojia hii inawafikia watu wengi zaidi.”