Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baa la njaa limepora utoto wa maelfu Gaza: UNICEF

Watoto huko Gaza wanasubiri kuwekewa chakula
UN News
Watoto huko Gaza wanasubiri kuwekewa chakula

Baa la njaa limepora utoto wa maelfu Gaza: UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Sasa twende Gaza, hii ni hadithi ya maisha, ya watoto wa Gaza wanaokabiliana na baa la njaa, hofu, na kuporomoka kwa kila kitu kinachowaweka hai. 

Ni hadithi inayoelezwa kupitia macho ya wale wanaoshuhudia mateso kila siku wakiwemo madaktari, akina mama, na wahudumu wa kibinadamu wanaopiga kengele ya tahadhari. Miongoni mwa wahudumu hao ni Tess Ingram afisa mawasiliano wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ofisi ya Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini. 

Tess aliyefunga safari na kushuhudia hali halisi Gaza akizungumza na waandishi wa habari kutoka mji wa Al Mawasi amesema mwenye macho haambiwi tazama na alichokishuhudia ni cha kutisha kwani jiji hilo sasa linazidi kuzama kwenye lindi la baa la njaa, vituo vya lishe vimefungwa, familia zinalia na kuhaha na watoto wanakufa kila uchao bila msaada.
“Jiji la Gaza, kimbilio la mwisho kwa familia za Kaskazini, linakuwa mahali ambapo utoto hauwezi kuishi. Ni jiji la hofu, wakimbizi na mazishi.”

Msichana aliyedhoofika sana kwa utapiamlo huko Gaza. Mashirika ya misaada yamekuwa yakiitaka Israel mara kwa mara iruhusu misaada zaidi kuingia Gaza ili kuzuia janga la kibinadamu linaloendelea.
© WHO
Msichana aliyedhoofika sana kwa utapiamlo huko Gaza. Mashirika ya misaada yamekuwa yakiitaka Israel mara kwa mara iruhusu misaada zaidi kuingia Gaza ili kuzuia janga la kibinadamu linaloendelea.

Anasema zaidi ya nusu ya vituo vya lishe vya watoto vimefungwa na kina mama wanapofika hospitalini wakiwa wamebeba watoto wao unaoweza kuhesabu mbavu sababu ya kukonda wanaambulia patupu kwani msaada ni haba na kwengine hakuna kabisa.
“Kilichokuwa hakifikiriki si jambo lijalo ni hali ambayo iko hapa tayari. Kuanguka kwa huduma muhimu na kunawaacha watoto wasiojiweza Gaza wakihaha kusalia uhai.”
Tess anasema ukiingia katika vituo vya msaada ndio utatambua wanachokipitia watoto wa Gaza kwani, mateso yanaonekana bayana
“Saa moja tu ndani ya kliniki ya lishe inatosha kuondoa shaka na shuku yoyote uliyonayo ya endapo Gaza kuna baa la njaa.”
UNICEF inasisitiza wito wake kuwa raia walindwe, msaada wa chakula na dawa upelekwe kwa wahitaji bila vizuizi. Kwa sababu watoto wa Gaza bado wako hai na dunia ina uwezo wa kuamua endapo wasalie hai.