UN yaonya kuhusu athari za ongezeko la mashambulizi ya Israel Gaza na Ukingo wa Magharibi
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR leo imeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa operesheni za kijeshi za Israel kaskazini mwa Gaza kama sehemu ya “mpango wa Israel wa kuchukua udhibiti kamili wa Jiji la Gaza, uliotangazwa tarehe 8 Agosti.”
Ajith Sungai, mkuu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu na Israel, amesema kuwa ripoti za ofisi hiyo zinaonesha kuwa ongezeko hilo limehusisha uharibifu mkubwa wa majengo ya makazi katika maeneo ya kusini mwa kaskazini mwa Gaza na kaskazini mashariki mwa Jiji la Gaza, hali iliyopelekea vifo vya raia na uhamisho wa kulazimishwa.
Sungai ameambia UN News kwamba Wapalestina 813 waliuawa, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, kati ya Agosti 26 na Septemba 1.
Amesema ripoti zinaonesha kuwa takribani Wapalestina milioni moja bado wako kaskazini mwa Gaza, “sasa wakisukumwa katika maeneo yanayozidi kupungua magharibi mwa Gaza chini ya hali mbaya za kibinadamu.”
Amebainisha kuwa wengi hawawezi kuhamia kwingine kwa sababu ya ukosefu wa maeneo salama na hatari kubwa zinazohusiana na kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Aliongeza kuwa wengine wamenaswa mashariki mwa Jiji la Gaza na hawawezi kufikiwa na wahudumu wa misaada.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya wanaotafuta misaada yanaendelea kote Gaza, huku malori ya misaada yakikumbana na changamoto za kuingia Ukanda wa Gaza.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imerekodi vifo zaidi ya 2,146 katika maeneo yanayozunguka vituo vya msingi wa kibinadamu vya Gaza na kando ya njia za misafara ya usambazaji.
Ukingo wa Magharibi
Sungai amebainisha kuongezeka kwa taarifa katika siku za hivi karibuni kuhusu “mipango ya serikali ya Israel ya ‘kutekeleza mamlaka,’ au kwa maneno mengine, kuhalalisha na kuthibitisha zaidi hatua ya kisheria ya kisheria ya kutwaa Ukingo wa Magharibi au sehemu zake chini ya sheria za Israel.”
Amesema tangazo lolote la kutekeleza mamlaka katika Ukingo wa Magharibi litakuwa na madhara makubwa kwa Wapalestina, “bila shaka kwa haki yao ya kujitawala, lakini pia kwa maisha yao ya kila siku.”
Amesema utekelezaji wa mamlaka na sheria za Israel katika Ukingo wa Magharibi utarahisisha upanuzi mkubwa zaidi wa makazi ya walowezi, kuhalalisha vituo vilivyopo, na kuipa Israel udhibiti kamili bila vizuizi vyovyote juu ya rasilimali za asili za Wapalestina.
Wito kwa nchi za kiarabu
Katika hotuba yake mbele ya Baraza la Umoja wa Nchi za Kiarabu, Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wapalestina UNRWA ametoa wito wa mshikamano na shirika hilo, kuhifadhi nafasi yake ya kulinda haki za wakimbizi wa Kipalestina, na kutumia kila chombo kukomesha mateso yasiyokubalika Gaza.
Wito wa Kamishna Mkuu huyo Philippe Lazzarini ulitolewa katika kikao cha 164 cha Baraza la Umoja wa Nchi za Kiarabu, kilichofanyika kwa ngazi ya mawaziri mjini Cairo, Misri.
Lazzarini amezungumzia hali mbaya inayoendelea Gaza na kutokea kwa “baa la njaa iliyosababishwa na binadamu” katika Ukanda wa Gaza ambayo inatarajiwa kusambaa haraka.
“Hii ni matokeo ya moja kwa moja na yanayotarajiwa ya mzingiro na vizuizi vinavyowekwa makusudi dhidi ya mashirika ya kibinadamu yenye misingi ya kimaadili ikiwemo UNRWA katika mfumo unaotumia chakula kama silaha. Watu wa Gaza sasa wanalazimika kuchagua kati ya kufa kwa njaa au kuuawa katika jitihada zao za kukata tamaa za kutafuta chakula,” amesema.
Kamishna Mkuu wa UNRWA ameongeza kuwa waandishi wa habari Gaza wanashambuliwa na kuuawa ili kunyamazisha sauti za mwisho “zinazofichua uhalifu wa kimataifa.”
Lazzarini amezungumzia pia Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, akisema kuwa jeshi la Israel na walowezi wenye silaha wanatenda vitendo vya kikatili dhidi ya Wapalestina, na kwamba “utwaaji sasa ni lengo la kisiasa lililotangazwa wazi.”
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kutojali kwa dunia na kushindwa kuchukua hatua ni jambo la kushangaza, linachukuliwa kama ushirikiano, na linatishia utulivu wa eneo lote.
Kampeni ya upotoshaji dhidi ya UNRWA
Lazzarini amesema kuwa mateso ya Wapalestina yanazidishwa na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi na majengo ya UNRWA, pamoja na mashambulizi katika ngazi za kisiasa na kisheria dhidi ya shirika hilo.
Amebainisha kuwa zaidi ya wafanyakazi 360 wa UNRWA wameuawa Gaza, na kwamba majengo mengi ya shirika hilo yameharibiwa au kuangamizwa kabisa.
Amesema sheria za Israel zinakataza uwepo wa wafanyakazi wa kimataifa katika maeneo ya Palestina yaliyokaliwa kwa mabavu, na kuongeza kuwa “kampeni kali ya upotoshaji duniani imeharibu heshima ya shirika na kukatisha ufadhili muhimu kwa kazi zake za maana.”
Licha ya changamoto hizi zote, wafanyakazi wa Kipalestina wa shirika hilo wameonesha “ujuzi na kujitolea kwa hali ya juu, jambo lililoruhusu UNRWA kuendelea kutoa huduma zake muhimu,” ikiwemo huduma za afya na elimu Gaza na Ukingo wa Magharibi.
Philippe Lazzarini ameonya kuwa hali ya kifedha ya UNRWA ni mbaya sana. Amesema hatua za kubana matumizi zitasaidia kulipa mishahara ya Septemba, lakini hali ya kifedha kwa kipindi chote kilichobaki cha mwaka 2025 haijulikani.
Ametoa wito wa mambo matatu:
- Kwanza, amezitaka nchi za Kiarabu kuonesha mshikamano na UNRWA, si kwa msaada wa kisiasa pekee, bali pia kwa msaada wa kifedha wa nguvu. Michango ya kifedha kutoka eneo hilo mwaka huu imefikia asilimia 3 pekee ya jumla ya michango yote iliyopokelewa na shirika, ikiwa ni upunguwa wa zaidi ya asilimia 90 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
- Pili, amehimiza kulindwa kwa nafasi ya UNRWA katika kulinda haki za wakimbizi wa Kipalestina.
- Tatu, amezitaka nchi za Kiarabu kutumia kila nyenzo za kisheria, kisiasa, kidiplomasia na kiuchumi walizonazo kukomesha mateso yasiyokubalika Gaza.
Amesema kusitisha mapigano ni jambo la lazima na amesisitiza umuhimu wa kuruhusu UNRWA kutumia utaalamu wake na mtandao wake wa kipekee wa usambazaji wa misaada kushughulikia njaa na kutoa msaada muhimu wa kibinadamu.
Amesisitiza kuwa wakati umefika wa kuchukua hatua, kuokoa maisha na kulinda mustakabali wa Palestina na eneo lote.