Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti ya UN kuhusu masuala ya haki za fidia kwa Waafrika na wenye asili ya Kiafrika

Makaburi ya Kitaifa ya Waafrika (African Burial Ground National Monument) yana mabaki ya zaidi ya Waafrika 419 waliokuwa wamezikwa mwishoni mwa karne ya 17 na karne ya 18, katika sehemu ya makaburi makubwa zaidi ya kipindi cha ukoloni kwa watu wenye asil…
UN News/Elizabeth Scaffidi
Makaburi ya Kitaifa ya Waafrika (African Burial Ground National Monument) yana mabaki ya zaidi ya Waafrika 419 waliokuwa wamezikwa mwishoni mwa karne ya 17 na karne ya 18, katika sehemu ya makaburi makubwa zaidi ya kipindi cha ukoloni kwa watu wenye asili ya Kiafrika.

Ripoti ya UN kuhusu masuala ya haki za fidia kwa Waafrika na wenye asili ya Kiafrika

Haki za binadamu

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Septemba 03, imetoa ripoti ikizitaka nchi wanachama na wadau wengine kuongeza juhudi katika kuhakikisha upatikanaji wa haki za fidia kwa Waafrika na watu wenye asili ya Kiafrika. Hii ni pamoja na msamaha wa dhati, kutafuta ukweli, kuenzi kumbukumbu, kutoa msaada wa kiafya na kisaikolojia pamoja na fidia ya kifedha.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa haki za fidia kutokana na urithi wa utumwa, biashara ya Waafrika katika utumwa na ukoloni ni msingi muhimu wa kuvunja ubaguzi wa rangi wa kimfumo unaoendelea kuwaathiri Waafrika na watu wenye asili ya Kiafrika.
 
Hata hivyo, ripoti imesema licha ya baadhi ya hatua chache zilizochukuliwa, bado kuna udhaifu mkubwa katika utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na serikali, mashirika ya biashara, taasisi za dini, vyuo vikuu, na makumbusho.
 
“Ubaguzi wa rangi wa kimfumo umejikita sana katika urithi wa kihistoria. Ili kufanikisha haki za fidia, mataifa na wadau wengine wanapaswa kutekeleza mkakati mpana unaojumuisha fidia katika sura mbalimbali,” amesema Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk. “Ili kuwa na ufanisi, mkakati huu lazima uhusishe uhusiano kati ya historia na hali ya sasa, katika maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla, ili kubomoa mifumo dhalimu iliyoundwa na historia.”
 
Ameongeza kuwa hakuna suluhisho la aina moja pekee, bali hatua na michakato inapaswa kujengwa katika historia na muktadha wa eneo husika, kujibu mahitaji yanayobadilika ya jamii na kuzingatia kwa dhati uzoefu mahsusi wa wanawake wenye asili ya Kiafrika.
 
Ripoti imesisitiza kwamba Waafrika na watu wenye asili ya Kiafrika wanapaswa kushirikishwa moja kwa moja katika kubuni na kutekeleza hatua hizi kwa ushiriki wa maana, jumuishi na salama.
 
Aidha, imetoa wito kwa mataifa kurejea katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, kutambua madhara makubwa yanayoendelea hadi sasa kutokana na ukoloni na utumwa, na kuwalinda wanaopinga ubaguzi wa kimfumo huku wakisukuma mbele haki za fidia.
 
Miongoni mwa hatua chanya zilizochukuliwa, ripoti imeeleza kuhusu ukaguzi wa maeneo ya umma ili kuondoa au kutoa muktadha mpya kwa majengo na alama zinazohusiana na utumwa na ukoloni katika baadhi ya nchi za Ulaya, ambapo pia makumbusho yameanza kushughulikia historia ya makusanyo yao. Hatua za kurudisha urithi wa kitamaduni, ikiwemo urejeshaji wa “sanamu za shaba za Benin,” zinaendelea.
 
Taasisi za elimu zimefadhili tafiti juu ya historia zao, kutoa msamaha wa hadharani, kuongeza nafasi za kielimu kwa jamii za warithi wa utumwa na kuanzisha maeneo ya kumbukumbu. Baadhi ya mashirika ya biashara yamekubali uwajibikaji kwa kuhusiana na historia zao, huku mashirika ya kidini yakianzisha mchakato wa kusimulia ukweli na kutoa misaada ya kifedha.
 
Aidha, madai ya fidia yamefikishwa mahakamani katika nchi mbalimbali na hoja zilizowasilishwa zimeimarisha harakati za kijamii na shinikizo la kisiasa.
 
Ripoti imependekeza tafiti za kina zaidi na mapendekezo ya sera kuhusu changamoto pana za kimuundo, zikiwemo haki za mazingira na tabianchi, pamoja na mageuzi ya mfumo wa misaada ya maendeleo na miundo ya kifedha na kiutawala ya kimataifa.
 
“Mataifa na wadau wengine wanapaswa kuonesha manufaa ya haki za fidia kwa jamii nzima na umuhimu wake katika kuvunja ubaguzi wa kimfumo,” amesema Türk.
 
Türk ameongeza “Viongozi wa kisiasa wana wajibu wa kutoa majibu bunifu, madhubuti na ya kina kwa wito wa haki za fidia. Kwanza kabisa, ni jukumu la mataifa kuchukua hatua, lakini pia mashirika ya dini, biashara na wadau wengine wanapaswa kukabiliana na historia zao na kutafuta njia za kweli za fidia.”