Mkuu wa UN aahidi msaada baada ya tetemeko la ardhi Afghanistan
Athari za tetemeko la ardhi Afghanistan (Kutoka maktaba)
Mkuu wa UN aahidi msaada baada ya tetemeko la ardhi Afghanistan
Msaada wa Kibinadamu
Tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 6.0 lilikumba maeneo ya mbali mashariki mwa Afghanistan usiku wa kuamkia leo na kuua takriban watu 800 huku likifagia kabisa vijiji kadhaa, kwa mujibu wa taarifa za awali.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo ameahidi “kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha msaada unawafikia waathirika.”
“Ninasimama bega kwa bega na watu wa Afghanistan baada ya tetemeko hili la kutisha lililoikumba nchi hiyo leo,” amesema Bwana Guterres kupitia ujumbe wake uliochapishwa mtandaoni.
“Nawapa pole za dhati familia za waathirika na kuwatakia wapate nafuu ya haraka majeruhi wote. Timu ya Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan imeimarishwa na haitabaki nyuma katika kuwasaidia wahitaji kwenye maeneo yaliyoathirika.”
Athari za tetemeko hilo
Tetemeko hilo limesababisha uharibifu mkubwa katika mikoa minne ya mashariki mwa Afghanistan , ikiwemo Nangarhar na Kunar, ambako wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na washirika wa kibinadamu tayari wanaunga mkono juhudi za misaada ya dharura.
Mamia ya nyumba zimeripotiwa kuporomoka katika vijiji vya milimani, nyingi zikishuka na kubomoka juu ya zingine zilizojengwa kwenye miteremko ya chini.
“Wakati tetemeko la ukubwa huu linapotokea, nyumba zinaporomoka na kuangukiana juu kwa juu,” amesema Salam Al-Jabani kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF.
Ameongeza kuwa “Na kwa kuwa lilitokea usiku sana, familia zilikuwa nyumbani zimelala, ndiyo maana tunaona vifo na hasara kubwa kiasi hiki.”
Ili kuongeza kasi ya hatua za dharura, Huduma ya Usafiri wa Anga ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imepanga safari za ndege za ziada kati ya Kabul na Jalalabad kwa ajili ya kupeleka wafanyakazi na vifaa vya misaada.