Mkuu wa UN aitaka SCO kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na changamoto za dunia
Mkuu wa UN aitaka SCO kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na changamoto za dunia
Malengo ya Maendeleo Endelevu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo ameitaka Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai (SCO) kuongoza katika kujenga mfumo wa haki na amani duniani, akionya kuwa dunia inakabiliwa na “ukosefu wa haki na mgawanyiko unaopanuka” kadri inavyosogea kwenye ulimwengu wa nguvu nyingi.
Akizungumza hii leo kwenye mkutano huo unaofanyika mjini Tianjin Guterres amesema “Mataifa yanazoinukia yanabadilisha biashara, diplomasia na maendeleo,” akiongeza kuwa “Lakini tunahitaji uongozi wenye misingi thabiti ili kuimarisha mshikamano wa kimataifa, kudumisha utawala wa sheria, na kutekeleza wajibu kwa watu kama ilivyoonyeshwa kwenye Mkataba wa Mustakabali.”
Amani na usalama: hakuna visingizio tena
Katibu Mkuu amebainisha kuwa mizozo ya Gaza na Ukraine ni maeneo yenye uhitaji wa haraka wa hatua za pamoja, akitaka hatua madhubuti za kimataifa. “Kiwango cha vifo na uharibifu Gaza ni cha kutisha na sasa baa la njaa imekuwa ikiwamaliza wananchi,” alisema.
Ameongeza kuwa “Tunahitaji usitishaji mapigano wa kudumu mara moja, kuachiliwa huru bila ya masharti yote kwa mateka na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu bila vizuizi, kwa amani na usalama wa kudumu. Hakuna vikwazo zaidi. Hakuna visingizio zaidi. Hakuna uongo zaidi.”
Kuhusu Ukraine, amesisitiza umuhimu wa “amani ya haki, jumuishi na endelevu kwa mujibu wa Katiba ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa,” huku akitaka pia kulindwa kwa raia nchini Sudan, Myanmar, Sahel na Afghanistan. “Uongozi wenu katika diplomasia na kupunguza migogoro ni muhimu,” amewaambia viongozi wa SCO.
Maendeleo Endelevu na fedha
Akigeukia masuala ya kiuchumi, Guterres ameonya kuwa madeni na pengo la usawa vinapunguza maendeleo yaliyopatikana duniani. “Hatuishi tena kama mwaka 1945 taasisi zetu lazima ziakisi hali halisi ya sasa,” amesema, akisisitiza mageuzi ya mfumo wa kifedha wa kimataifa.
Ameonya kuwa mageuzi yanayohitajika ni yale yatakayoweza “kuongeza mara tatu uwezo wa kukopesha wa benki za maendeleo ya kimataifa, kutoa nafuu ya kweli ya madeni, na kuhamasisha mtaji binafsi kwa kiwango kikubwa.”
Amesisitiza kuwa “Sauti ya pamoja ya SCO inaweza kusaidia kuyafanya mageuzi haya kuwa hali halisi”.
Mabadiliko ya tabianchi: Hatua zahitajika
Akiangazia zaidi ya watu bilioni tatu wanaoishi katika maeneo yenye hatari ya tabianchi ndani ya ukanda wa SCO, Guterres ameonya juu ya “joto kali, kuyeyuka kwa barafu, mafuriko na ukame” vinavyosukuma jamii kwenye hali ya hatari.
Amezitaka nchi wanachama wa G20 wanaohusika na asilimia 80 ya uzalishaji wa gesi chafuzi kuongoza mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
“Wote lazima wafanye juhudi za ziada,” amesisitiza, akihimiza mataifa kuwasilisha ahadi mpya za hali ya hewa zinazolingana na kikomo cha nyuzi joto 1.5 na malengo ya dunia ya “kuongeza mara mbili ufanisi wa nishati na kuongeza mara tatu vyanzo vya nishati jadidifu ifikapo 2030.” Pia ametaka “mpango wa haki wa kuondokana na mafuta ya kisukuku huku tukiharakisha mapinduzi ya nishati mbadala.”
Uongozi wa Kidijitali na ushirikiano wa kimataifa
Katibu Mkuu pia amesisitiza haja ya ushirikiano wa kimataifa katika teknolojia ya akili mnemba AI na usimamizi wa kidijitali. Amepongeza kuanzishwa kwa Jopo Huru la Kimataifa la Kisayansi na Majadiliano ya Kimataifa kuhusu Usimamizi wa AI chini ya Umoja wa Mataifa.
“Mifumo hii ni hatua kubwa ya ushirikiano wa kimataifa kuhusu AI,” amesema, akibainisha umuhimu wa ushirikishwaji, mshikamano na haki za binadamu.
Akimshukuru Rais Xi Jinping kwa kuzindua Mpango wa Utawala wa Kimataifa wa China, Guterres amesema hatua hiyo “imejikita kwenye mshikamano wa kimataifa na inalinda mfumo wa kimataifa unaoongozwa na Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.”
Alihitimisha akisema “Pamoja, tuifanye ahadi ya Katiba ya Umoja wa Mataifa kuwa hai, na tufanye kazi kwa ajili ya mustakabali wa amani, heshima na mshikamano.”