UNICEF: Maelfu ya watoto wako hatarini baada ya tetemeko kubwa la ardhi Mashariki mwa Afghanistan
Watoto katika kijiji cha Shade Bara jimboni Herat nchini Afghanistan
UNICEF: Maelfu ya watoto wako hatarini baada ya tetemeko kubwa la ardhi Mashariki mwa Afghanistan
Msaada wa Kibinadamu
Tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 6.0 katika kipimo cha Richter lilikumba mashariki mwa Afghanistan usiku wa kuamkia Jumapili, na kitovu chake kikiwa karibu na Jalalabad jimbo la Nangarhar.
Taarifa za awali zinaonesha mamia ya watu wamefariki dunia na maelfu kujeruhiwa, huku watoto wakiwa miongoni mwa waathirika wakuu limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF.
Limeongeza kuwa uharibifu ni wa kutisha huku nyumba na miundombinu katika jimbo la Nangarhar na jimbo jirani la Kunar zimeharibiwa vibaya, na maafisa wanatahadharisha kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka kadri juhudi za uokoaji zinavyoendelea. Duru za awali zinasema zaidi ya watu 600 wamepoteza maisha wakiwemo watoto.
UNICEF yaeleza masikitiko makubwa
Mwakilishi wa UNICEF nchini Afghanistan, Dkt. Tajudeen Oyewale, ametoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, akieleza athari kubwa ya janga hili kwa watoto na jamii. “Fikra zetu ziko kwa watoto na familia zilizoathirika, nyingi zikikosa makazi na wapendwa wao,” amesema, akisisitiza haja ya msaada wa dharura mara moja.
Timu za dharura zapelekwa kulikoathirika zaidi
UNICEF imethibitisha kuwa timu zake ziko tayari mashinani katika wilaya za Chawkay na Nurgal, jimbo la Kunar, zikitoa huduma ya kwanza na matibabu kupitia vitengo vya afya vinavyohamishika.
Shirika hilo pia linashirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na washirika wa ndani kufanya tathmini ya kina ya uharibifu huku likiendelea kusaidia hospitali za Nangarhar na Kunar ambazo zimeelemewa na idadi kubwa ya majeruhi.
Msaada muhimu watumwa kwa waathirika
Ili kukidhi mahitaji ya haraka, UNICEF imeanza kusambaza vifaa vya dharura ikiwa ni pamoja na dawa, vifaa vya usafi, nguo za kupasha joto, mablanketi, na vifaa vya hifadhi kama mahema na mabasha. Hospitali pia zinapatiwa msaada wa ziada ili kukabiliana na wimbi la majeruhi, huku shughuli za uokoaji na misaada zikiendelea kupanuka.
Kipaumbele kwa ulinzi wa watoto na msaada
Mbali na misaada ya haraka, UNICEF imesisitiza kuwa itazingatia pia suala la lishe, maji safi, usafi wa mazingira, hifadhi ya muda, ulinzi wa watoto na msaada wa kisaikolojia.
Dk. Oyewale amesema shirika hilo litaendelea kuongeza kiwango cha misaada ya kibinadamu, likishirikiana kwa karibu na jamii kuhakikisha kuwa watoto na familia wanapata msaada wa kuokoa maisha haraka iwezekanavyo.