Tetemeko la ardhi Afghanistan, juhudi za UN kusaidia zinaendelea
Tetemeko la ardhi Afghanistan, juhudi za UN kusaidia zinaendelea
Msaada wa Kibinadamu
Baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6 katika vipimo vya richa kutokea usiku katika maeneo ya mbali mashariki mwa Afghanistan na kuripotiwa kuua takribani watu 800 na kufuta vijiji, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo Jumatatu Septemba Mosi ameahidi “kufanya kila linalowezekana kusaidia walioathirika.”
“Ninasimama kwa mshikamano kamili na wananchi wa Afghanistan baada ya tetemeko la ardhi lililokumba nchi leo,” Katibu Mkuu amesema kupitia ujumbe mtandaoni. “Nawapa pole za dhati familia za waathirika na kuwatakia majeruhi kupona haraka. Timu ya Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan imehamasika na haitabaki nyuma katika kuwasaidia wahitaji katika maeneo yaliyoathirika.”
Katika eneo la tukio, mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa yameripoti uharibifu mkubwa katika mikoa minne ya mashariki mwa Afghanistan ikiwemo Nangarhar na Kunar, ambako wafanyakazi na washirika wa kibinadamu tayari wanasaidia katika juhudi za misaada.
Wamekwama ndani
Mashuhuda wameripoti kwamba tetemeko hilo lilitokea karibu saa sita usiku wa Agosti 31 kwa saa za huko, jambo lililoibua hofu kuwa Waafghanistani wengi bado wanaweza kuwa wamekwama chini ya vifusi vya nyumba zao.
Kitovu cha tetemeko hilo kinakadiriwa kuwa kilikuwa umbali wa kilomita 8 pekee chini ya ardhi kwa na kusababisha majengo kutikisika katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, na pia katika mji mkuu wa Pakistan, Islamabad.
Miongoni mwa wanaotoa msaada ni Ujumbe wa Msaada wa Umoja wa Mataifa Afghanistan (UNAMA), Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu (OCHA), Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) na mengine mengi.
“Kutokana na taarifa za vifo na majeruhi kutokana na tetemeko katika eneo la mashariki mwa Afghanistan kuendelea kuibuka, timu za WHO Afghanistan ziko hospitalini na vituo vya afya, zikisaidia kutibu majeruhi na kutathmini mahitaji ya haraka ya kiafya,” Imeeleza WHO kupitia mtandao wa X.
WHO imeongeza ikisema, “tunafikisha dawa muhimu na vifaa na kutuma timu za afya katika maeneo yaliyoathirika kusaidia kuokoa maisha.”
Wito wa kimataifa
Pia wakiwa Afghanistan kutoa msaada, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limebainisha kuwa zaidi ya watu 2,000 huenda wamejeruhiwa katika mkoa wa Kunar pekee. Kuna hofu kuwa jiji la kibiashara la Jalalabad linaweza kuwa na “idadi kubwa ya vifo,” amesema msemaji wa UNHCR Babar Baloch.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa wanaokimbilia kufikisha msaada wa kuokoa maisha katika maeneo yaliyoathirika ikiwa ni pamoja na vifaa vya matibabu, makazi, maji safi, hema na blanketi.
Bwana Baloch amesisitiza kuwa ukubwa wa janga hili “umepita uwezo wa sasa wa mamlaka za eneo na jamii… Tunatoa wito kwa jumuiya ya wafadhili duniani kote kuunga mkono kwa dharura juhudi za misaada. Waafghanistani wanahitaji msaada wetu sasa, kabla haijawa kuchelewa kwa wengine wengi.”
Timu za msaada italazimika kushinda changamoto za kijiografia ili kuwafikia jamii za mbali zaidi ambazo zinaweza kufikiwa tu kwa miguu, OCHA imebainisha.
Imesema kuwa mamlaka za de facto zimepeleka mitambo mikubwa katika wilaya za Nurgal na Chawkay kuondoa vizuizi vya barabara na baadhi ya sehemu zimeripotiwa kufunguliwa tena. Watu waluojeruhiwa mno pia wamepelekwa kwa helikopta katika hospitali za Jalalabad na Asadabad ambazo sasa ndizo vituo vikuu vya rufaa kwa waathirika katika mikoa ya Nangarhar na Kunar.
Lakini zilizo pembezoni zinaweza kufikiwa tu kwa miguu na safari inachukua hadi saa tatu kutoka eneo la kizuizi, OCHA imeongeza, ikibainisha maeneo ya Bonde la Dewagal katika wilaya ya Chawkay na Bonde la Mazar katika wilaya ya Nurgal, mkoa wa Kunar.
Tetemeko hili ni miongoni mwa mabaya zaidi kuwahi kuikumba Afghanistan na linatokea chini ya miaka miwili tangu tetemeko la ukubwa wa 6.3 lililotokea Herat upande mwingine wa nchi, lililoathiri makumi ya maelfu ya watu.