Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres ataka haki na "mabadiliko ya kweli" kwa watu wa asili ya Kiafrika

Mwanamke aliyevaa gauni la rangi amesimama jukwaani mbele ya bendera UN na jukwaa.
UN Panama/Javier Conte Raia wa Panama wenye asili ya Afrika wanatumia sauti zao kutokomeza ubaguzi wa rangi na ubaguzi.

Guterres ataka haki na "mabadiliko ya kweli" kwa watu wa asili ya Kiafrika

Haki za binadamu

Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Watu wa Asili ya Kiafrika, inayofanyika kila mwaka tarehe 31 Agosti, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametaka haki, heshima na usawa kwa watu wa asili ya Kiafrika kote duniani.

Katika ujumbe wake mahsusi kwa siku hii, Guterres ametambua mchango wa “kipekee” wa watu wa asili ya Kiafrika katika nyanja zote za jitihada za kibinadamu. Pia ametambua “kivuli cha muda mrefu” cha utumwa na ukoloni — kinachoendelea kuonekana kupitia ubaguzi wa rangi wa kimfumo, uchumi na jamii zisizo na usawa, pamoja na pengo la kidijitali kati ya wale wanaonufaika na teknolojia ya kidijitali na wale wasio na fursa hiyo.

Katibu Mkuu amesifu Mkataba wa Kidijitali wa Kimataifa  — ulioidhinishwa mwaka 2024 kama sehemu ya Mkataba wa Zama Zijazo  ambao amesema unalenga kukuza mfumo wa kimataifa unaoakisi hali halisi ya dunia ya sasa na kuhakikisha unawanufaisha watu wote, kila mahali. Amesema mkataba huo ni hatua muhimu mbele, hasa kwa kujumuisha ahadi za kukabiliana na ubaguzi na hotuba za chuki katika teknolojia za kidijitali.

“Ubabe wa watu weupe na simulizi zinazodhalilisha utu,” ameandika Katibu Mkuu, “vinaenezwa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii, na mara nyingi, ubaguzi wa rangi hujengwa ndani ya mifumo ya kimitambo.”

“Miaka 80 tangu Mkataba wa Umoja wa Mataifa ulipoahidi usawa wa haki na heshima ya asili ya kila binadamu, na miaka 60 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa aina zote za Ubaguzi wa Rangi,” amehitimisha, “ni wakati muafaka kurekebisha makosa ya kihistoria.”

Muongo wa pili wa kimataifa

Siku hii ya Kimataifa ya mwaka huu ni ya kwanza kuadhimishwa ndani ya Muongo wa Pili wa Kimataifa wa Watu wa Asili ya Kiafrika, ulioanza tarehe 1 Januari 2025 hadi 31 Desemba 2034.

Muongo huu unabeba kaulimbiu “Watu wa Asili ya Kiafrika: Utambuzi, Haki na Maendeleo.”

Lengo ni kuangazia umuhimu wa kutambua haki na mchango wa watu wa asili ya Kiafrika. Bwana Guterres ametoa wito kwa miaka 10 ijayo kuwa kipindi cha “mabadiliko ya kweli,” ikijumuisha juhudi za kuelekea Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu kuheshimu kikamilifu haki za binadamu za watu wa asili ya Kiafrika.

Katika Muongo wa Kwanza, zaidi ya nchi 30 zilirekebisha sheria na sera zao ili kukabiliana na ubaguzi wa rangi na kushughulikia changamoto mahsusi zinazowakumba watu wa asili ya Kiafrika — katika baadhi ya nchi, hii ilikuwa mara ya kwanza kabisa kuchukua hatua hizo.

Jukwaa la Kudumu la Watu wa Asili ya Kiafrika liliundwa, na siku mpya za kimataifa zilianzishwa ili kusherehekea mchango wa watu wa ughaibuni kutoka Afrika, wakiwemo wanawake na wasichana.

Kwa kujenga juu ya mafanikio ya miaka 2015 hadi 2024, Muongo wa Pili unalenga kuimarisha juhudi za kimataifa za haki na maendeleo kwa watu wa asili ya Kiafrika, na kuunda mustakabali wenye usawa zaidi, ambamo ndoto, haki, na mchango wao unatambuliwa, kuheshimiwa, na kusherehekewa kwa dhati.