Mashamba mbadala wa tumbaku yabadilisha maisha ya wakulima Kenya – WHO
Mashamba mbadala wa tumbaku yabadilisha maisha ya wakulima Kenya – WHO
Afya
Tangu kuzinduliwa kwa mpango wa Mashamba Mbadala wa Tumbaku mwaka 2022, zaidi ya wakulima 9000 nchini Kenya wameacha kulima zao la tumbaku na kuanza shughuli mbadala za kujipatia kipato.
Mpango huu una lengo la kuwapatia wakulima wa tumbaku maisha endelevu na yenye faida kwa kuwahamasisha kulima mazao mbadala ya chakula.
Hii ni njia ya kushughulikia si tu madhara ya kiafya yanayosababishwa na kilimo cha tumbaku, bali pia athari zake hasi za kijamii, kiuchumi na kimazingira.
Mpango huu umefadhiliwa kwa ushirikiano wa kimataifa kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), Wizara za Afya, na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa. Nchini Kenya, mpango huu unaungwa mkono kwa kiwango cha juu na serikali za kitaifa na kaunti.
Katika mwanzo wa utekelezaji, WHO Kenya iliwapatia mafunzo wahudumu 80 wa afya ya jamii kutoka kaunti ya Migori, magharibi mwa Kenya, ili kuwaelimisha wakulima kuhusu madhara ya kilimo cha tumbaku na njia mbadala zinazopatikana. Mwaka 2023, Kaunti ya Migori na mmoja wa wakulima wa mfano, Sprina Chacha, walitunukiwa Tuzo ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO ya Siku ya kimataifa ya kutokomeza tumbaku. Tangu hapo, wahudumu wa afya ya jamii 1500 wamefundishwa na mpango huu umeenea hadi kaunti nyingine tatu.
Shuhuda za wakulima waliotumikisha watoto wao kisiri
Dawin Sionyonyo Lusakia, kutoka Bumula, kaunti ya Bungoma, alikuwa mkulima wa tumbaku kwa zaidi ya miaka 20. Anakumbuka mzigo mzito wa kazi hiyo na jinsi alivyolazimika kuwatumia watoto wake kwenye mashamba.
Ameeleza kuwa msimu wa kufunga majani ya tumbaku ulikuwa mgumu zaidi kwa sababu ya masharti magumu ya kampuni za tumbaku. Mara nyingi aliwatumikisha kisiri watoto wake wamsaidie kwani hangeweza kumudu kuajiri wafanyakazi.
Kilimo cha tumbaku kinahitaji nguvu kazi nyingi, na mara nyingi familia nzima, wakiwemo watoto, hujitokeza kusaidia kwa kipindi cha karibu miezi tisa. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watoto milioni 1.3 duniani kote wanashiriki katika kilimo cha tumbaku na wengi wao hukosa shule.
Nchini Kenya, wakulima wa tumbaku hupata chini ya dola 110 za Marekani kwa mwaka, huku mashamba yote yakitumiwa kwa tumbaku badala ya chakula.
Moses Kikulesi, mkulima wa zamani kutoka Bungoma anakumbuka jinsi mjukuu wake akiwa bado mchanga sana alivyokuwa akisaidia katika ukulima.
Anasema mtoto wake Neema alipoanza shule, kwa wiki alikuwa akikosa siku 2 - 3 za masomo kusaidia shambani.
“Kabla hajajua kutembea tulikuwa tukimleta kwenye shamba la tumbaku na kumlaza chini ya majani ya tumbaku huku tukifanya kazi mashambani. Mke wangu alikuwa anaweza kunisaidia shambani lakini hakukuweko na mtu nyumbani wa kumtunza mtoto." anasema Kikulesi.
Madhara ya kiafya na mazingira: Shida ya kupumua
Mbali na athari hasi za kijamii na kiuchumi, kilimo cha tumbaku kinahusishwa na hatari kubwa za kiafya. Wakulima hupatwa na matatizo ya kupumua na dalili za ugonjwa uitwao Green Tobacco Sickness au (GTC) usababishwao na binadamu kugusa majani mabichi ya tumbaku yenye unyevunyevu na hivyo ngozi kuingia sumu ya tumbaku au nikotini. Pia, kilimo cha hutumia kemikali kali ambazo huleta maumivu ya kichwa, kikohozi na matatizo ya ngozi, hasawakulima wanapokosa vifaa vya kujikinga.
Watoto wanaojihusisha na kilimo hiki mara nyingi hukumbwa na utapiamlo na kudumaa.
"Tulilazimika kutumia kemikali kali kukuza tumbaku - dawa za kuuwa wadudu na mbolea ambazo zilikuwa ghali na zenye madhara. Zilisababisha maumivu ya kichwa, kikohozi na matatizo ya ngozi, hasa wakati hatukuwa na vifaa vya kujikinga," anasema Lusakia.
Faida za mazao mbadala:
Kwa kulima mazao mbadala, wakulima hupata mapato mara mbili au tatu zaidi ya tumbaku. Mazao haya hukomaa haraka, huhimili misimu zaidi ya mmoja kwa mwaka, na huuzwa kwa masoko yenye mpangilio kama vile shule, hospitali na magereza.
Lusakia anasema “sasa ninapata zaidi ya nilichowahi kupata kwa tumbaku, kazi imepungua, na watoto wangu hawalazimiki tena kwenda shambani. nimeweza hata kutumia baadhi ya maharagwe kuwapa chakula.”
Mabadiliko ya maisha na mafanikio:
Kwa kutumia muda kidogo shambani na safari fupi ya kuuza mazao yao, wakulima sasa wanaweza kuanzisha biashara ndogo au kujiunga na vikundi vya akiba. Pia wamekuwa na uhakika wa chakula na lishe bora kwa familia zao.
Gerald Eroto na mkewe Janet kutoka kijiji cha Ataba, Kaunti ya Busia, miaka saba iliyopita walibadilisha kilimo cha tumbaku kuwa cha maharagwe ya aina ya nyota. Eroto anasema maharagwe hayo humsaidia kulipa karo za watoto, na wakati mwingine hupeleka maharagwe moja kwa moja shule kama sehemu ya malipo. Ameweza pia kumlipia mwanawe karo ya Chuo Kikuu huko Embu.
Kuhamasisha wakulima wengine:
WHO na wadau wake huandaa mikutano ya kuelimisha wakulima kuhusu faida za kuacha kilimo cha tumbaku. Mikutano hayo huwapa nafasi wakulima kuuliza maswali, kuelewa faida za kiafya na kiuchumi za mazao mbadala, na kupanga mabadiliko yao.
“Mashamba mbadala wa tumbaku yameleta mabadiliko makubwa kwa jamii za wakulima. Yamewawezesha kulipa karo, kupata huduma za afya, na kuwekeza kwenye maisha bora ya familia zao.” anasema Dkt. Joyce Nato, Afisa wa kiufundi wa WHO nchini Kenya.